Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Brigedia Jenerali Mstaafu Wilfred Pome Mwalambile Kabunda, mmoja wa wanajeshi walioshiriki Vita ya Kagera ya mwaka 1978–1979, amesema kumbukumbu ya Mashujaa si tukio la kuangalia historia pekee, bali ni wito kwa kizazi cha sasa kuendeleza misingi ya uzalendo, uwajibikaji na kujituma katika kulijenga Taifa.

Akizungumza leo Julai 24,2026 kuhusu umuhimu wa Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, Kabunda amesema kizazi cha wanajeshi wa wakati huo kiliongozwa na mapenzi makubwa kwa nchi, jambo lililowafanya kukabiliana na mazingira magumu ya vita kwa dhamira ya kulinda mipaka ya Tanzania na usalama wa wananchi.

Amesema wakati wa Vita ya Kagera, yeye na wenzake walijitoa kwa moyo mmoja katika kuhakikisha uvamizi huo unazuiwa na kurejesha amani nchini, huku wakitambua kuwa jukumu lao lilikuwa kulinda uhuru na heshima ya Taifa.

Brigedia Jenerali Kabunda alikuwa sehemu ya vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vilivyoshiriki operesheni ya kuikomboa Kagera na kuendelea na mapambano hadi nchini Uganda, hatua iliyosaidia kuhitimisha utawala wa Idi Amin Dada.

“Mchango wetu umekuwa sehemu ya historia ya Taifa,tulilinda mipaka ya Tanzania na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani,” amesema Kabunda.

Amesema uzoefu wa mashujaa waliopigana vita hiyo unapaswa kuwa somo kwa Watanzania wa sasa, hususan vijana, kwa kuwataka kuthamini amani iliyopo na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

Baada ya utumishi wake wa muda mrefu ndani ya JWTZ, Kabunda alipandishwa hadi cheo cha Brigedia Jenerali kabla ya kustaafu kwa heshima, akiwa ameacha alama muhimu katika historia ya ulinzi na usalama wa Taifa.

Kwa sasa, Brigedia Jenerali Mstaafu Kabunda anaendelea kutambulika kama mmoja wa mashujaa hai waliobeba kumbukumbu ya mapambano ya Vita ya Kagera, akiwakilisha kizazi cha wanajeshi walioweka mbele uzalendo, ujasiri na kujitolea kwa ajili ya Tanzania.

Kila mwaka ifikapo Julai 25, Tanzania huadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwa lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi wote waliopigania uhuru wa nchi pamoja na waliojitolea kulinda amani, usalama na maslahi ya Taifa.

Maadhimisho hayo ni fursa ya kutafakari historia ya Taifa, kuthamini mchango wa waliotangulia na kuendelea kujenga kizazi kinachoamini katika misingi ya uzalendo, umoja na uwajibikaji kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.