Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
WATU nane wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya gari la abiria aina ya Toyota Coaster kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania katika eneo la Chumbi, Kata ya Chumbi, Tarafa ya Mohoro wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Protas Mutayoba, alisema ajali hiyo ilitokea Septemba 22, 2026 saa 9:15 mchana katika barabara kuu ya Lindi–Dar es Salaam.
Alifafanua ajali hiyo ilihusisha Toyota Coaster yenye namba za usajili T930ERF, iliyokuwa ikiendeshwa na Halifan Cosmas Madodo, mwenye umri wa miaka 44, na lori aina ya Scania lenye namba T511EPS, likiwa na tela namba T469EPL, lililokuwa likiendeshwa na Hassan Salum Goro, mwenye umri wa miaka 30.
Kwa mujibu wa Mutayoba, watu wanane waliokuwa ndani ya Toyota Coaster walifariki dunia, huku wengine 12 wakijeruhiwa katika ajali hiyo.
Alieleza kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Coaster, ambaye alishindwa kulimudu gari lake, likahamia upande wa kulia wa barabara na kugongana uso kwa uso na lori hilo.
Mutayoba alisema majeruhi wamehifadhiwa katika Kituo cha Afya Muhoro kwa ajili ya matibabu, huku baadhi yao wakitarajiwa kuhamishiwa katika hospitali kubwa kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Alitoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.



