Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Nairobi
Nimeandika makala hii nikiwa hapa Nairobi, Kenya muda mfupi tu baada ya kusikia kauli ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi, Dk. John Nchimbi, kuhusiana na umuhimu wa kupata Katiba Mpya kwa Watanzania.
Balozi Nchimbi alisema: “Nikiambiwa kama una jambo la kuwaambia Watanzania, moja tu, unapewa nafasi ya kusema sema moja, nitasema, pambaneni mpate Katiba Mpya.”
Huu ndio ulikuwa ujumbe mkuu wa hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, aliposhiriki ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Mwaka wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, siku ya Julai 24, 2026.
Sitanii, Balozi Nchimbi alifafanua zaidi akasema Katiba ndiyo sheria mama. Kwamba Katiba ndiyo sheria kuu na ikipata Katiba Mpya na kama Katiba hiyo itakuwa ni nzuri, basi sheria nyingine zote mbaya zinafutika.
Akasema kwa zaidi ya miaka 40 sasa nchi imepatambania upatikanaji wa Katiba mpya na akarejea uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Nne wa kuleta Katiba mpya ila akasema mchakato ulikwama na unahitaji kukwamuliwa.
Baada ya kauli ya Dk. Nchimbi, nikamsikia Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kwa mara ya kwanza akimpongeza kiongozi wa serikali kwa kauli hii aliyoitoa Dk. Nchimbi.
Nimesema kwa uwazi hili la kwamba Dk. Bagonza amepongeza kwa mara ya kwanza, maana amesema naye anafurahia kukosolewa, na ni kwa muktadha huo namwabia naye, asimamie ukweli, kwa maana akosoe au kupongeza panapostahili badala ya kugeuza mijadala kuwa kama imani!
Ibara ya 47(II) ya Ilani ya CCM ya 2025 – 2030 inasema: “Kuhuisha na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.” Rais Samia Suluhu Hassan amekaririwa mara kadhaa akisema bayana kuwa atahakikisha anakamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Na ndiyo maana wakati wa kampeni na baada ya kampeni amesema ataunda Tume ya Ukweli na Maridhiano, kisha baada ya tume hii, nchi yetu iende katika mchakato wa Katiba Mpya.
Sitanii, kauli ya Balozi Nchimbi imenikumbusha ahadi 10 za Mwana-TANU, zinazosema: 1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. 2. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote. 3. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma. 4. Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa. 5. Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

6. Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote. 7. Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu. 8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. 9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika. 10. Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.
Sitanii, kuna nyakati katika maisha ya taifa ambazo kauli ya kiongozi haiwezi kuchukuliwa kama maneno ya kawaida. Kauli ya Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, ya kuwataka Watanzania kuendelea kudai Katiba Mpya ni mojawapo ya kauli hizo.
Ni kauli ya ujasiri, uzalendo na utayari wa kulifikisha taifa katika hatua mpya ya kujenga misingi imara ya utawala bora.
Dk. Nchimbi amewataka Watanzania kuibeba kwa uzito ajenda ya Katiba Mpya, akisisitiza kuwa serikali ina dhamira ya kuendeleza mchakato huo. Hapa ndipo Watanzania wanapaswa kuiona kauli hiyo kama fursa ya kujenga hoja, si sababu ya kugawanyika.
Katiba si sheria ya kawaida. Ni mama wa sheria zote za nchi. Sheria nyingine hutungwa kwa kuzingatia mamlaka na misingi iliyowekwa na Katiba. Ndiyo maana Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaweka wazi kwamba kunapokuwa na mgongano kati ya Katiba na sheria nyingine, Katiba ndiyo inayotawala na sheria hiyo huwa batili kwa kiwango inachokinzana na Katiba.
Ibara ya 64(5) inasema: “Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo Mambo ya Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba itakuwa batili.”
Kwa hiyo, kudai Katiba Mpya si kudai sheria nyingine tu. Ni kudai msingi unaotengeneza mazingira ya sheria zote nyingine kuwa bora, zenye haki na zenye kulinda masilahi ya wananchi.
Katiba Mpya nzuri inaweza kuweka misingi imara zaidi ya kulinda haki za binadamu, kuimarisha utawala wa sheria, uwajibikaji wa viongozi, mgawanyo na udhibiti wa madaraka, uhuru wa taasisi, ushirikishwaji wa wananchi na uendeshaji wa uchaguzi unaoaminika. Pia inaweza kusaidia kuweka mfumo unaozuia mamlaka ya dola kutumiwa kinyume cha masilahi ya wananchi.
Sitanii, faida kubwa zaidi ya Katiba nzuri ni kwamba inalinda taifa dhidi ya kutegemea uzuri au ubaya wa mtu mmoja. Viongozi hubadilika; vyama hubadilika; vizazi hubadilika. Lakini Katiba imara huweka kanuni za mchezo zinazopaswa kuheshimiwa na kila anayeshika madaraka.
Ndiyo maana kauli ya Dk. Nchimbi inapaswa kuungwa mkono kwa hoja na utulivu. Watanzania wanapaswa kudai Katiba Mpya kwa njia za kikatiba, kwa majadiliano, ushirikishwaji na maridhiano. Katiba nzuri si mali ya CCM, si mali ya upinzani wala si mali ya kundi fulani. Ni mali ya Watanzania wote.
Sitanii, huyu ndiye Dk. Nchimbi nimjuaye. Anatamka lililo bora kwa taifa, si kwa masilahi yake binafsi. Taifa linapopata Katiba nzuri, halijengi tu sheria ya leo; linajenga kinga ya haki, amani, demokrasia na maendeleo kwa vizazi vijavyo.
Hivyo, ujasiri wa Dk. Nchimbi wa kuwataka Watanzania kuibeba ajenda hii unapaswa kupongezwa na kuungwa mkono kwa dhati.
Wakati umefika nchi yetu ipate Katiba Mpya. Nafahamu Rais anaipenda Katiba Mpya, llani ya CCM imeahidi Katiba Mpya, viongozi karibu wote wanataka Katiba Mpya, swali linabaki ni moja tu, nani anayekwamisha Katiba Mpya isije?
Wakati ni huu. Watanzania tuchukue hatua kwa njia ya nguvu ya hoja, tufikie mwafaka wa kupata Katiba Mpya tulimalize hili lililodumu tangu baada ya Uhuru. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827
