Na Deodatus Balile, Jamhurimedia, Nairobi
Nimekuja hapa Nairobi kufanya mafunzo yanayohusiana kwa kiasi kikubwa na maendeleo ya jamii.
Tunafundishana haki za wanawake, watoto na uthamini wa jinsia. Katika jamii tunayoishi kuna urithi wa nyumba, mashamba na fedha. Lakini kuna urithi mwingine ambao hauonekani kwa macho – urithi wa maneno na tabia. Huo ndio huamua taifa litakuwa la amani au la misuguano.
Naingia kwenye mitandao hapa Kenya, nashuhudia kitu tofauti kabisa. Nadhani tunatofautiana katika malezi. Kuna utetezi mkubwa wa matusi kugeuzwa sawa na chai ya asubuhi.
Karibu kila mtandao unaoingia, hakuna nguvu ya hoja, bali kuna hoja ya nguvu. Kuna mvua ya matusi. Wanatushangaa Watanzania kwa nini hatuwaigi.
Sitanii, mtoto akizaliwa anakuwa hajui maandamano, hajui siasa, hajui wizi wa kura, hajui kuzuia mikutano ya hadhara, hajui kuna CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CUF, wala chuki.
Anajifunza kutoka kwa watu wazima. Anachokisikia leo ndicho kinachoweza kuwa sehemu ya maisha yake kesho. Ndiyo maana wazazi, walimu, viongozi wa dini, wanasiasa na jamii kwa ujumla wanapaswa kuwa waangalifu kuhusu lugha wanayoizungumza mbele ya watoto.
Si kosa watoto kujua kwamba katika demokrasia watu wanaweza kutofautiana kimawazo. Lakini ni kosa kubwa kuwaacha wakiamini kwamba tofauti hizo hutatuliwa kwa hasira, matusi au uadui wa kudumu.
Taifa lolote lenye busara huwafundisha watoto kwamba hoja hujibiwa kwa hoja, sheria huheshimiwa, na mazungumzo hubaki kuwa daraja muhimu la kutafuta mwafaka. Tusishibishe akili za watoto kwa chuki na hasira, watadhani ndio utamaduni sahihi.
Sitanii, leo mtoto anapomsikia mzazi akizungumza kwa kejeli na hasira dhidi ya mwenye mawazo tofauti, kesho anaweza kufanya vivyo hivyo shuleni, kazini au katika jamii. Tusishangae kuona kizazi kisichojua kusikiliza, ikiwa sisi wenyewe tumekizoesha kusikia sauti za mabishano kuliko sauti za busara.
Mtoto akikua akijua kuonea watu ndiyo njia sahihi ya kubaki au kuingia madarakani, sauti hiyo ataichukua kama ufunguo wa maisha yake.
Amani ya Tanzania haitalindwa na vyombo vya dola peke yake. Italindwa pia na malezi tunayowapa watoto wetu. Umoja wa taifa hautajengwa na sheria pekee. Utajengwa na maadili tunayowafundisha watoto mezani, nyumbani, darasani na kwenye maeneo ya ibada. Haki za binadamu nazo zitaendelea kuheshimiwa pale tutakapowalea watoto wanaojua kwamba haki zao zinaambatana na wajibu wa kuheshimu haki za wengine.
Ni wakati wa kujiuliza: tunawajengea watoto kumbukumbu gani? Je, tunawaachia lugha za hasira au lugha za hekima?
Kama taifa tunawafundisha kushindana kwa hoja au kugombana kwa maneno? Majibu ya maswali haya ndiyo yatakayoamua sura ya Tanzania ya miaka ishirini ijayo. Tanzania ilivyo sasa, haikutokea kwa bahati. Ukiona vinaelea, vimeundwa. Sisi wazazi tujiulize, lugha tulizokuwa tunazisikia kutoka kwa wazazi wetu, ndizo tunazoendelea kunena kwa watoto wetu?
Hivi tunafahamu kuwa wakati wafinyanzi wanatengeneza vyungu kwa kufinyanga udongo, watengeneza magari wanatumia vyuma, mafundi ujenzi wa nyumba wanatumia nyundo, wajenzi wa barabara wanatumia magreda na mengine… wajenzi wa umoja, amani, haki na mshikamano wanatumia maneno.
Ninachoandika hapa kinaweza kukukera kutokana na yale uliyoelezwa mwanzo yakakujenga ukawa hivyo ulivyo, lakini piga moyo konde.
Jiulize, unataka miaka 50 ijayo tuwe na taifa la namna gani? Zana ya kujenga taifa hilo ni maneno unayowaeleza watoto wako na majirani. Tafakari.
Sitanii, kila kizazi huandika historia yake. Kizazi cha leo kina wajibu wa kuandika historia ya malezi yanayozalisha raia wenye nidhamu, uvumilivu, uzalendo na utetezi wa haki kwa hoja. Kizazi kinachobishana bila kupigana na kinachobadili upepo kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu.
Tukiwalea watoto wetu tukiwasihi kuheshimu tofauti za maoni, kupenda mazungumzo na kuthamini umoja wa taifa, tutakuwa tumewaachia urithi mkubwa kuliko mali yoyote. Hata hivyo, kwa kusema hivyo, simaanishi washuhudie haki zinaporwa, wao wakae pembeni wakidhani ndiyo njia ya kulinda amani.
Wazazi Watanzania wenzangu tujiandae. Tusirithishe kizazi chetu dhana ya kupaza sauti pekee. Turithishe kizazi chetu kiwe kinachojua kusikiliza, kufikiri na kujadiliana kwa hekima, bila kuacha haki iponyoke kama Mwalimu Julius Nyerere alivyopigania uhuru wa nchi yetu ukapatikana bila kumwaga damu. Hapo ndipo tutakapokuwa tumelinda amani ya Tanzania kwa njia ya kudumu. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827


