Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi ni mradi wa kimkakati unaotekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi imara, shindani na shirikishi, sambamba na kufikia Dira ya Taifa ya 2050 na kuongeza fursa za ajira.

Akizungumza, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea mradi huo mkoani Morogoro, Mhe. Sangu aliipongeza kamati hiyo kwa ufuatiliaji wake, akibainisha kuwa maelekezo 11 yaliyotolewa awali tayari yameingizwa katika utekelezaji, hatua inayoimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya Bunge na Serikali.

Aidha, alisema mradi huo umeanza kurekodi mafanikio kwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 2,176 katika msimu huu, huku ukitarajiwa kufikia ajira 2,315 za moja kwa moja na 9,000 zisizo za moja kwa moja kadri uzalishaji unavyopanuka. Uzalishaji wa tani 50,000 za sukari unatarajiwa kupunguza nakisi ya bidhaa hiyo nchini kwa takribani asilimia 20.

Katika kuongeza tija, Serikali imepanga kupanua mashamba ya miwa kutoka hekta 4,156 hadi 6,000, hatua itakayoongeza uwezo wa uzalishaji hadi tani 75,000. Alisisitiza kuwa uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF, unaelekezwa kwenye miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na uchumi wa taifa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu Chakoma, alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia NSSF kwa kushirikiana na SHIMA katika mradi huo, akieleza kuwa umeendelea kuleta tija kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya kamati, Mhe. Kafiti Kafiti alisema mradi huo ni ushahidi wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, akibainisha kuwa viwanda vina mchango mkubwa katika ajira, kipato na ukuaji wa uchumi. Aliongeza kuwa zaidi ya wakulima 3,500 wanaonufaika na mradi huo wanachochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya vijijini.

Mhe. Kafiti alibainisha kuwa matarajio ni kiwanda kuanza kupata faida katika mwaka wa fedha ujao, jambo litakaloongeza mapato ya Serikali na kulinda uwekezaji wa fedha za wanachama wa NSSF, huku kamati ikiendelea kusimamia mradi huo ili kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa.

Akihitimisha kikao hicho, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Aveline Munisi alihakikishia kamati hiyo kuwa ushauri na mapendekezo yao yataendelea kufanyiwa kazi kwa maslahi mapana ya mradi huo.

Wajumbe wa kamati walimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, kwa uongozi wake thabiti, wakieleza kuwa amefanikisha kufufua na kusukuma mbele miradi iliyokuwa imesimama, huku mafanikio ya Mkulazi yakidhihirisha maono yake ya kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kupanua fursa za ajira.

Walisisitiza umuhimu wa kuendeleza nidhamu, uwazi na uaminifu ili miradi hiyo iendelee kuleta manufaa mapana kwa wananchi na uchumi wa taifa.