Na Andrea Kadege, WAF-Arusha

Kambi ya Madaktari bingwa wa upasuaji inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha, Mount Meru, leo Julai 24, 2026 imefanikiwa kuondoa uvimbe kwa mtoto wa kiume mwenye miaka minne ambaye alizaliwa na tatizo hilo.

Akizungumza baada ya kufanikisha kwa oparesheni hiyo, Daktari bingwa wa upasuaji pamoja na saratani ambaye pia ni Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba Muhimbili Dkt. Larry Akoko amesema kuwa uvimbe huo huzidi kukua kadri mtoto pia anavyokua hivyo kumsukuma shingo na kufanya atembee akiwa ameinamisha shingo yake.

“Bila kufanya upasuaji, uvimbe huo ungeweza kusababisha matatizo makubwa ya shingo, kuumwa na mgongo na ingeweza kuathiri zaidi ukuaji wake, hivyo kwa kushirikiana na madaktari wengine tumefanikiwa kuundoa na ni matarajio yetu haoutojirudia tena”, amesema Dkt. Akoko.

Dkt. Akoko ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kushirikiana na ECSA HC na KIDS OR katika kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi akisisitiza kuwa uwepo wa kambi za kibingwa umesaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi na kupunguza gharama za kufuata huduma hizo katika maeneo ya mbali.

Kwa umoja wao wazazi wa mtoto hiyo, wameshukuru jopo la madaktari hao kwa kufanikisha matibabu ya mtoto wao, huku wakielekeza pongezi zao pia kwa serikali kwa kushirikiana na wadau kuratibu kambi hiyo iliyosaidia mtoto wao kurejea katika hali ya kawaida wakiwa na matarajio kuwa atarejea shule na kuendelea na masomo yake.

Kambi ya Madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha, Mount Meru imeratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA HC) na KIDS OR ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi.