Na Cletus Sanga, WAF – Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Clinton Health Access Initiative (CHAI) imeendelea kuimarisha ubora wa huduma za wagonjwa mahututi nchini kwa kukamilisha kuandaa miongozo ya huduma za wagonjwa mahututi na mwongozo wa mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi.

Hayo yamesemwa Julai 23, 2026, mkoani Morogoro na Dkt. Michael Kiremeji, Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura na ajali kutoka Wizara ya Afya, wakati wa kikaokazi cha kuandaa miongozo ya idara ya wagonjwa mahututi( ICU), pamoja na mwongozo wa mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi.

“Tunaandaa miongozo hii ili kuhakikisha wataalamu wa afya wanatoa huduma zinazozingatia viwango vilivyowekwa, huku wakiendelea kuongeza ujuzi wakiwa kazini. Hii itaboresha ubora wa huduma na kuongeza usalama wa wagonjwa,” amesema Dkt. Kiremeji.

Ameeleza kuwa mwongozo wa mafunzo kwa vitendo utasaidia kujenga mfumo endelevu wa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kupitia usimamizi wa karibu, ufuatiliaji wa kitaalamu na kubadilishana uzoefu, ili kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza uwezo wa kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Taasisi ya Clinton Health Access Initiative (CHAI), Dkt. Leah Mtui amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za wagonjwa mahututi kwa kuwa na miongozo ya kutolea huduma kwa wagonjwa, mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa afya.

“CHAI itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miongozo hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kuboresha huduma za wagonjwa mahututi, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya na kuongeza matokeo chanya ya matibabu kwa wananchi,” amesema Dkt. Leah Mtui.

Miongozo hiyo inatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma za wagonjwa mahututi katika vituo vya afya nchini kwa kuhakikisha wataalamu wanatumia miongozo, hivyo kuongeza ubora wa huduma, usalama wa wagonjwa na uwezo wa kuokoa maisha.