Na Mwandishi Wetu

Wakulima nchini wameanza kunufaika na kuwepo kwa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ambalo lipo mahususi kusaidia masoko ya mazao yanapatikana kwa wakati sahihi na mauzo yanafanyika kwa ushindani stahiki.

Na katika kuhakikisha kuwa faida za soko hilo zinawanufaisha wengi na kuchangia kikamilifu kwenye ujenzi wa taifa, uongozi wa TMX umeendelea kuwahamasisha wakulima kujiunga na mfumo huo wenye tija kubwa na ambao huendeshwa kwa njia ya minada.

Pia kampuni hiyo iliyoanza na mtaji wa Sh bilioni 50, inaendelea na majaribio ya kuuza mazao mbalimbali yanayolimwa nchini ili kuongeza idadi ya wakulima wanaotumia jukwaa la soko hilo lililoanzishwa mwezi Agosti mwaka 2014 na kuanza kufanya biashara kwa majaribio mwaka 2018.

TMX inasema kwenye tovuti yake kuwa Soko la Bidhaa ni eneo kuu ambapo wauzaji na wanunuzi wanakutana na kubadilishana bidhaa na fedha katika mtindo wenye mpangilio na utaratibu maalumu na kwa kanuni mahususi na zenye uwazi zilizoelezwa vizuri.

“Kuanzishwa kwa soko la bidhaa kutamwezesha mkulima kuweza kuuza mazao yake katika utaratibu unaoeleweka bila kulanguliwa. Ndiyo maana kabla ya kuanzishwa kwa soko hili ulianzishwa kwanza utaratibu wa stakabadhi ghalani ambao umefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” inafafanua na kuongeza:

“Ununuzi wa mazao ya wakulima kupitia Soko la Bidhaa unalenga kuongeza ufanisi katika mifumo ya masoko nchini ambayo imekuwa na changamoto kwa muda mrefu wa kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi ili kuleta ushindani kwenye bei, kupunguza gharama na kuweka uwazi.”

Mfumo huu ulizinduliwa rasmi mwaka jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane ambayo yalifanyika kitaifa mkoani Simiyu.

Waziri Mkuu alisema kuanza kufanya kazi kwa TMX ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II).

Wiki iliyopita, Wizara ya Fedha na Mipango ilisema kuwa jukwaa la Soko la Bidhaa limekuwa na mafanikio makubwa na linazidi kuwanufaisha wakulima wengi. Miongoni mwa faida hizo kwa mujibu wa taarifa ya Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 ni bei nzuri za mazao na kuongezeka kwa mapato ya halmashauri mbalimbali zikiwemo za Kondoa na Babati.

“Katika kuhakikisha ufanisi wa mfumo wa mauzo wa mazao ya kilimo kupitia Soko la Bidhaa, kuanzia Julai hadi Agosti 2019, Soko la Bidhaa Tanzania lilifanikiwa kufanya mauzo ya zao la ufuta kwa majaribio katika mikoa ya Dodoma (Kondoa) na Manyara (Babati) kwa njia ya kidijitali, ambapo wakulima walilipwa takriban Sh 3,000 kwa kilo ikilinganishwa na Sh 1,500 kwa kilo iliyokuwa ikilipwa kabla ya mfumo wa mauzo kwa njia ya mtandao – OTS,” Wizara ya Fedha na Mipango inasema kwenye taarifa hiyo ya mwezi Machi mwaka 2020.

“Kupitia mfumo huo, wakulima wa Kondoa na Babati walilipwa Sh milioni 1,405.26 na halmashauri za Kondoa na Babati zilikusanya mapato ya Sh 27,645,968.00 kutokana na mauzo ya zao la ufuta ikilinganishwa na Sh 4,936,780.00 kabla ya mfumo huo,” inaongeza.

Katika mwaka huu wa fedha, TMX ilifanya uhamasishaji kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na wakulima 3,200 katika halmashauri za wilaya za Bukoba Vijijini, Bukoba Manispaa, Missenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba.

Taarifa ya Hazina pia inasema TMX imeanza maandalizi ya kuuza korosho kupitia mfumo wa OTS katika msimu wa mwaka 2019/20 ambapo imetoa mafunzo kwa wadau wa zao hilo katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga.

“Vilevile, maandalizi ya majaribio ya kuuza pamba iliyochakatwa kwa maana ya nyuzi na mbegu yameanza kufanyika ambapo AMCOS 106 zilipewa mafunzo wakiwemo viongozi na wakulima 730 kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) na Chama cha Msingi Ordoy Babati, Manyara,” taarifa inasema.

By Jamhuri