Soko la Chifu Kingalu ni ‘bomu’

*Vibanda zaidi ya 200 vyafungwa kwa miezi sita

*Biashara yadorora, kisa? Malumbano na Manispaa 

Morogoro

Na ALEX KAZENGA

Kutokuaminiana kati ya baadhi ya wafanyabiashara wa Soko Kuu la Chifu Kingalu na uongozi wa Manispaa ya Morogoro kunatajwa kuwa tishio kwa amani na usalama wa mji huo mkongwe nchini.

Hali hiyo imetokana na ‘mgomo baridi’ wa wafanyabiashara wanaojitambulisha kuwa ‘wa zamani’, kufunga vibanda vyao (maarufu kama vioski), wakidai uongozi wa sasa wa soko hilo umewekwa na manispaa kwa masilahi ya wakubwa, huku kodi ya upangaji ikidaiwa kuwa ni kubwa.

Tangu kuzinduliwa kwake Februari 11, mwaka huu, wafanyabiashara wenye vibanda katika soko hilo la kisasa hawavifungui na baadhi wamehamia kwenye masoko mengine.

Soko hilo limegharimu fedha za walipa kodi Sh bilioni 17.6, lakini waliopewa jukumu la kulisimamia wanaendelea na mivutano isiyo na tija.

JAMHURI limefika sokoni hapo na kushuhudia soko hilo lenye mwonekano mzuri likiwa na vioski chini na hata juu, ghorofani, huku wenyeji, wengi wakiwa ni wafanyabiashara walioomba kutotajwa majina gazetini, wakiulaumu uongozi wa soko na manispaa kwa kuwanyanyasa. 

“Hawajashindwa kulipa kodi, ila hawafungui kwa sababu wanapingana na manispaa kuwaletea bei za vioski zisizoendana na uhalisia wa mitaji ya wafanyabiashara tuliopo hapa,” anasema mfanyabiashara mmoja ambaye anamiliki kibanda cha kuuza dagaa sokoni humo.

Anasema mgogoro huo usipotatuliwa haraka, mbali na kusababisha biashara kudorora, pia  unaweza kuzusha uhasama mkubwa na hata vurugu kati ya wananchi na manispaa.

“Ni suala la muda tu. Ni ‘time bomb’. Sawa na bomu la kutega. Muda si mrefu kunaweza kuzuka tafrani hapa, hasa iwapo wanaolumbana hawatapatana au kupatanishwa,” anasema.  

Wakati akisema hivyo, wapo wanaokiri kufunga na kulikimbia Soko Kuu la Chifu Kingalu na kwenda kuanzisha biashara katika masoko ya Manzese na Mawenzi yaliyopo Mtaa wa Sabasaba, kwa hoja kwamba mitaji yao inakatika kwa kukosa wateja.

“Mauzo yangu kwa siku nikiwa sokoni hapa hayazidi Sh 5,000, ukiangalia gharama za upangaji na unachoingiza kwa siku unaona kabisa hakuna maana ya kuendelea kulipa kodi ya kibanda katika soko hili,” anasema Zaitun Miraji anayeuza juisi ya matunda.

Mbali na kulalamikia biashara kutokwenda vizuri katika soko hilo, wafanyabiashara hao wanasema kitendo cha manispaa kuwatoza ‘amana’ wakati wa kupangisha vioski hivyo kimewaondolea morali ya biashara.

Wanasema kitendo hicho si cha kiungwana, kwani kimelenga kuwakomoa na kuwanyima fursa ya kupata vioski vilivyo upande wenye biashara nzuri.

Aidha, kitendo cha manispaa kuwalazimisha walipe kodi mara baada ya kutoa amana hizo wanasema nacho kimechangia kuwanyong’onyeza na kushindwa kuendelea na biashara.

“Wafanyabiashara wadogo tuliohakikiwa kabla ya soko kuvunjwa tupo 349, lakini vioski vinavyofanya biashara tangu limefunguliwa havifiki 70,” anasema mfanyabiashara wa vipodozi aliyepanga ghorofani katika soko hilo huku idadi kamili ya vioski vilivyoko katika jengo hilo vikiwa 304.

Lawama za kuzorota kwa biashara sokoni hapo zinaelekezwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa, Sheila Lukuba, wakidai amesababisha biashara kuwa ngumu na hataki majadiliano ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.

Wanadai mkurugenzi amekosa mikakati thabiti ya kuliendesha soko, badala yake anatumia nguvu na vitisho.

“Mkurugenzi hataki kushirikiana na wafanyabiashara halali wa soko hili, kuna mamluki amewapa vioski hapa, hawa ndio hutangulizwa mbele kupinga hoja za sisi tunaolalamikia suala la vioski,” anasema mfanyabiashara mwingine.

Hata kitendo cha mkurugenzi kutofika sokoni hapo kunawafanya kuamini kuwa anaogopa kuhojiwa kuhusu njama zake za kutaka kuwapangisha watu wengine.

Kuna tetesi za uwepo wa matajiri kutoka Kilimanjaro, Mwanza, Arusha na Mbeya ambao wamepenyeza fedha ili wapate vibanda.

Mpango huo ni kinyume cha makubaliano ya awali ambapo wafanyabiashara wa zamani kabla ya soko kuvunjwa waliahidiwa kupewa kipaumbele wakati wa kugawa vibanda soko jipya litakapokamilika.

Sambamba na hilo, wanasema kitendo cha sasa cha manispaa kutangaza kupangisha vibanda vilivyoko kwenye mgogoro na wapangaji wa zamani, huenda kikasababisha vurugu.

Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wa zamani wa soko hilo kabla halijabomolewa na kujengwa kisasa, wanahoji kwa nini uongozi wa mpito uliopo madarakani usiondoke kwa kushindwa kutatua changamoto zinazowakabili?

Pia wanasema ili kufikia mwafaka na soko kujiendesha kwa tija, ni vema mkurugenzi wa manispaa akaitisha mkutano ndani ya siku 21 uchaguzi ufanyike na viongozi halali wapatikane kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Wafanyabiashara Soko Kuu Morogoro (UWASOMO), umoja wenye usajili No. 9702.

“Suala la vibanda lina changamoto nyingi ambazo hazijawahi kupatiwa ufumbuzi tangu soko linajengwa, Rais John Magufuli alipokuja kulizindua hakutembelea hata kibanda kimoja.

“Si kwamba alishindwa kuvitembelea vibanda! Wahusika walifanya makusudi asigundue madudu yaliyofanyika,” anasema mmoja wao akilalamikia pia kulazimika kukikarabati kibanda chake kwa gharama ya Sh milioni 1.9 kwa kuweka sakafu ya vigae na kubadili taa ili kibanda kiwe na mwanga wa kutosha na mvuto.

Anasema taa za umeme zilizofungwa zinatumia umeme mwingi wakati zina mwanga hafifu, hali inayosababisha biashara za wapangaji wa chini kudorora.

 “Wafanyabiashara wenye vibanda wanaojulikana kuwa wazungumzaji sana siku Magufuli amekuja walikamatwa na kuwekwa ndani hadi mkutano ulipokwisha ndipo wakatolewa,” anasema akibainisha kwamba viongozi wa manispaa walilazimika kutumia nguvu kuwanyamazisha baadhi yao wasitoe kero kwa Magufuli.

Kodi ya kibanda sokoni hapo ni Sh 300,000 kwa vibanda vya chini na Sh 200,000 vibanda vya ghorofani, ingawa kuna ukweli kwamba hata ujenzi wenyewe si rafiki, kwani vimejificha.

“Hatuwezi kusema soko lijengwe upya kama tunavyotaka, lakini ninadhani hata wewe unaona jinsi ambavyo ujenzi haukuzingatia wateja wanatokea upande upi,” anasema mfanyabiashara mwingine.

Wanakilalamikia kitendo cha milango ya vibanda hivyo kuwekwa kwa kutazamana na mingine kuwekwa uelekeo ambao si rahisi wateja kuiona kwa haraka na kuvutiwa na bidhaa.

Kwa uongozi kutotokana na katiba ya UWASOMO kunasababisha kuminywa kwa fursa ya kufikisha kero kwa wahusika, pia manispaa kujiamulia mambo hata yenye madhara kwa wengi.

Mwenyekiti wa kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2019 kutafuta suluhu ya migogoro katika soko hilo, Juma Silaha, anasema migogoro eneo hilo ni ya muda mrefu.

Anasema kikosi kazi kiliundwa kwa ajili ya kutafuta maridhiano na namna ya kumaliza migogoro, jambo ambalo halijafanikiwa mpaka sasa.

“Wanachama wa UWASOMO tulishituka kuona picha zetu zimetupwa kwenye dampo la taka na uongozi wa manispaa kukaa kimya,” anasema Silaha.

Picha hizo ni zile walizopigwa wafanyabiashara wote wa zamani mbele ya vibanda vyao kabla ya soko la zamani kuvunjwa mwaka 2019 baada ya manispaa kukutana nao na kuwapa taarifa juu ya maendeleo ya ujenzi.

Lengo la kupigwa picha ni kuisaidia manispaa kuzitumia siku ya kugawa vibanda kama ushahidi wa mfanyabiashara wa zamani anayestahili. 

“Lakini mpango huo ulivurugwa makusudi. Kwa nini Manispaa ya Morogoro isikutane na UWASOMO na kupanga bei kama yalivyofanya masoko kama Kisutu lililopo Manispaa ya Ilala, Soko la Njombe Mji, Soko la Manispaa ya Moshi, Soko la Arusha na Soko la Ndugai lililopo jijini Dodoma?” anahoji Silaha.

Anadai kwamba Soko la Kisutu wafanyabiashara waliomba kodi ya kibanda iwe Sh 75,000, baada ya mkutano na uongozi wa manispaa, wakakubaliana iwe Sh 119,500 kwa mwezi.

Utaratibu kama huo ulitumika katika masoko ya Njombe Mji, Moshi, Arusha na Dodoma ambako kodi ni Sh 100,000 kila mwezi.

“Dodoma wafanyabiashara wa zamani walikubaliwa kufanya biashara bila kulipa kodi kwa miezi minne,” anasema.

Mwenyekiti wa mpito wa uongozi wa soko hilo, Khalid Salum, akizungumzia hali ilivyo, anasema tatizo kubwa lilikuwa kwenye vizimba lakini limekwisha na kuongeza kwamba changamoto zimebaki kwenye bei za vibanda.

 “Ukitumia muda mwingi kulumbana unapoteza vitu vingi, sisi kama viongozi wa soko kwa kushirikiana na manispaa hatupo kwa ajili ya kulumbana, tupo kuelekeza watu namna ya kufanya biashara na kulitunza soko letu,” anasema Salum na kuongeza kwamba suala la kodi za vibanda limejadiliwa kwenye vikao vya Kamati ya Fedha ya Manispaa na kamati hiyo imetoa amri kodi iliyopo kwa sasa ipunguzwe kwa asilimia 50.

Kwa mujibu wa Salum, utekelezaji wa agizo hilo utaanza rasmi Julai mwaka huu.

Akieleza kiini cha migogoro, anasema ni milango 14 ya vibanda vilivyoko mbele ya soko.

“Kwa ndani vipo vibanda vya kutosha, lakini kila mtu anataka kupata eneo la mbele wakati tuko wafanyabiashara zaidi ya 300. Ukiambiwa kugawa vibanda hivyo utampa nani na umwache nani?” anahoji Salum.

Anaulaumu uongozi uliopita kwa kuongoza vibaya, na kwamba uliongoza njama za kuhujumu vizimba sokoni humo huku akiuonya kuacha chokochoko kwenye suala la vibanda.

Naye, Meneja wa Soko, Alatutosi Sanga, anasema wengi wanaolalamika kuhusu suala la vibanda si wafanyabiashara halali, bali walilenga kuchukua vibanda hivyo kwa ajili ya kuvikodisha kwa watu wengine.

Anasema idadi halisi ya wafanyabiashara alionao ni 170 na kwamba kwa asilimia 90 wafanyabiashara wa zamani walikuwa wanapangisha watu wengine.

“Wanaolalamika ukiwauliza mmoja mmoja biashara yako iko wapi hawawezi kukuonyesha, sasa unataka manispaa ianze kujadiliana na akina nani?

“Hao tunafahamu walikuwa wapangishaji, kama unawataka wafanyabiashara wa zamani nenda kibanda No. 23, 27,28 na 54 utawakuta wafanyabiashara wa zamani wakiendelea kuchapa kazi,” anasema Alatutosi.

Kuhusu suala la kufungwa kwa vioski anasema manispaa kuna watu inawadai kodi ya miezi mitano, hivyo ni lazima vibanda vyao vifungwe ili wahusika walipe kodi.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi, Ofisa Habari wa Manispaa ya Morogoro, Lilian Henricko, anasema lawama na malalamiko yanayoelekezwa kwa manispaa hayana msingi.

“Uhakiki wa wafanyabiashara wa zamani ulifanyika na uongozi wa soko ulishirikishwa. Hao wanaopinga wana masilahi yao binafsi,” anasema Lilian na kuongeza kuwa kodi za vioski zilizopo kwa sasa zilipitishwa na wafanyabiashara wenyewe.

Aidha, anahoji ni kwa nini kodi za maduka yaliyo karibu na soko hilo yanapangishwa kwa bei kubwa – Sh 400,000 hadi tano na watu hawalalamiki lakini wanataka kupunguziwa katika vibanda vya soko hilo.

“Wapo watu wachache wamegomea hiyo bei, hao tumefunga vibanda vyao na tenda tumetangaza upya ili watu waje tuwapatie,” anasema huku akisema waliokuwa wamevichukua mwanzo si wafanyabiashara bali walitaka kuwapangisha watu wengine kwa bei kubwa.

Aidha, anasema kodi inayolalamikiwa kuwa kubwa awali ilipangwa kwa kuangalia ukubwa wa soko, hivyo walitaka makusanyo ya kodi yatakayotokana na kodi za vibanda yatumike kwenye uboreshaji wa miundombinu ya soko.

Suala la lawama kuelekezwa kwa Mkurugenzi wake, Lilian, anasema haziepukiki kwa sababu yeye ni kiongozi, na kuongeza kuwa hawawezi kuacha kuwapokea wafanyabiashara wapya katika soko hilo, kisa wa zamani hawataki.

“Tumeshatangaza kwenye vyombo vya habari na hata kwenye mitandao ya kijamii, vibanda vilivyofungwa vichukuliwe na watu wengine,” anaeleza na kuongeza kuwa manispaa hawako tayari kufanya kazi na watu walioko nje ya soko.