Kampuni ya SportPesa Tanzania, inakamilisha mipango itakayowezesha kupanua wigo wa uwekezaji wake nchini kwa kugeukia michezo mingine, lengo ikiwa ni kuwapa nafasi vijana wengi zaidi kushiriki katika sekta ya michezo, huku ikisisitiza ushirikiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF).
Akizungumza na JAMHURI juu ya mipango yao ya siku zijazo, Mkurugenzi wa SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba, amesema kampuni hiyo ina mpango wa kupanua wigo kwa kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika michezo mingine hapa nchini.

“TFF ni wadau wetu wakubwa katika kuhakikisha nia yetu ya kusaidia ukuaji wa soka na michezo mingine inafanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa kwa manufaa ya klabu na timu ya Taifa,” amesema Tarimba.
Amesema kampuni hiyo haina uwezo wa kuingilia mambo ya ndani ya TFF kwa namna yoyote ile, kwa sababu mpira wa miguu  unaendeshwa kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni.
Amesema SportPesa kwa kushirikiana na wataalamu wa soka wa ndani na nje ya nchi, ipo mbioni kukamilisha programu na mipango endelevu ya  jinsi ya kuhakikisha uwekezaji wake katika michezo unakuwa na tija kwa nchi.
Mkurugenzi huyo ambaye amewahi kuwa Rais wa Klabu ya Yanga, amesema TFF haina budi kuja na kanuni kali itakayoweka ulazima wa klabu kuwa na timu za vijana wa umri wote.

“Dunia ya leo, vijana wengi wamekuwa mamilionea kwa ajili ya kushiriki katika michezo kutokana na serikali zao kuwekeza katika mchezo wa soka na michezo mingine,” amesema Tarimba.
Amesema SportPesa kwa kulitambua hilo imeamua kuja na mikakati ya kuhakikisha vijana wenye vipaji wanapata nafasi ya kuendeleza vipaji vyao kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Amesema huu ni wakati wa taasisi nyingine kujitokeza na kutoa udhamini katika michezo mingine kama ngumi, kuogelea, riadha, kurusha tufe na michezo mingine mingi.
“Katika miaka ya (1970) 1974 Tanzania ilikuwa inaogopeka kwa majirani na hata duniani katika michezo kama riadha, ngumi na michezo mingine iliyokuwa ikishiriki,” amesema Tarimba.
Amesema wana michezo kama John Steven Akhwari, Titus Simba, Wily Isangura, Filbert Bayi, Peter Tino na wengine wengi waliovuma miaka hiyo walitokana na utashi wa kuwekeza kwa vijana.

Tarimba amesema kampuni ya SportPesa, inawekeza katika soka na michezo mingine katika kipindi kifupi kijacho, lengo ikiwa ni kuona michezo hiyo ikianza kukua kuanzia ngazi ya chini kwa manufaa ya klabu na timu za Taifa.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, amesema kampuni ya Sport Pesa imekuja na mipango mizuri yenye lengo la kuhakikisha soka na michezo mingine inakuwa mkombozi wa ajira za vijana.
“Hii ni kampuni ambayo imekuja kuleta mageuzi ya soka katika ukanda huu kwa kuwekeza katika mchezo wa soka na michezo mingine ili kuchangia kutengeneza ajira kwa ajili ya vijana wasiokuwa na ajira,” amesema Madadi.
Madadi, ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, amesema katika miaka ya karibuni vijana wamekuwa wakikabiliwa na  vikwazo vikubwa zaidi wakati wa kutafuta ajira kiasi cha wengine kujikuta wakikata tamaa na kujitumbukiza katika matendo maovu kama ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.

Amesema Serikali kwa kulitambua tatizo la ajira, imelipa kipaumbele kwa kuanzisha Tume ya Taifa ya Ajira mwaka 2008 lengo ikiwa ni kuhakikisha mamlaka husika zinalishughulikia kwa kuangalia ukubwa wa tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Amesema wapenzi wa michezo kwa ujumla wanatakiwa kuziunga mkono kampuni kama SportPesa ambazo zimekubali kuja nchini na kuwekeza fedha nyingi kwa lengo la kusaidia michezo.
Mkurugenzi huyo amesema TFF ipo tayari kushirikiana na klabu au taasisi yoyote nchini, yenye nia ya dhati kuwekeza katika suala zima la mchezo wa soka na mingine kwa ujumla.
“Mfano Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ilitangaza uzinduzi wa programu ya Ligi za Vijana ya Azam (AYL), ambayo utaifanya klabu kuendesha ligi za vijana chini ya umri wa miaka 11, 13, 15 na 17 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, kitendo kinachopaswa kuigwa na klabu nyingine,” amesema Madadi.

Amesema katika msimu ujao wa Ligi, TFF itahakikisha soka la vijana linapewa kipaumbele kama ilivyokuwa msimu uliopita, kwa mechi za vijana kuanza kabla ya mchezo wa wakubwa kuanza.
Amesema mchezo wa soka na michezo mingine unahitaji watu au kampuni zenye mitaji mikubwa ya fedha kiasi cha kuwawia watu wengi kukubali kuwekeza, hali ambayo ni changamoto kubwa.
Naye mchezaji wa zamani ya Klabu ya Yanga na Timu ya Taifa, Mohamed Hussein Mmachinga, amesema juhudi zinatakiwa kuzishawishi kampuni nyingine kuiga mfano wa SportPesa.
Amesema mpira unahitaji uwekezaji wenye fedha ndefu na mipango yenye maono ya mbali juu ya mchezo wenyewe, hasa kwa kuwekeza kwa vijana wadogo wenye vipaji.

1907 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!