Home Michezo Lazima tuwe tayari kujifunza

Lazima tuwe tayari kujifunza

by Jamhuri

Ujio wa Klabu ya Everton na juhudi za Serikali za kurudisha michezo mashuleni hauwezi kuwa na maana kama viongozi wa michezo hawatakuwa na mipango madhubuti na kuwa tayari kujifunza toka katika nchi ambazo zipo juu kisoka.

Wakizungumza na JAMHURI kuhusu uongozi ujao wa TFF na michezo mingine na ujio wa Klabu ya Everton wamesema hakutakuwa na mabadiliko yoyote kama viongozi wataendelea kuwa na mawazo na fikra zilezile za miaka yote.
Wamesema bila ya mikakati yenye mwelekeo wa kimaendeleo katika uongozi wa michezo hata kama wakiletwa Man United, Barcelona, Real Madrid na vilabu vingine vikubwa duniani hakuwezi kuwa na mabadiliko.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Soka Tanzania (FAT) ambaye pia ni mjumbe wa kudumu wa FIFA, Said El Maamry amesema mafanikio ya kweli ya soka na michezo mingine yanahitaji ubunifu na kuwa tayari kujifunza kila siku.
“Pamoja na michezo kurudishwa mashuleni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma lakini, kuna mambo ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi kama tunahitaji maendeleo,” amesema El Maamry.
Amesema ukosefu wa viwanja na mchezo wa soka kutumiwa na wanasiasa kama mitaji ya kufikia malengo yao na kukosekana kwa mipango endelevu ni baadhi ya changamoto za michezo nchini.
Amesema kuna umuhimu wa serikali kurejesha maeneo ya wazi yaliyokuwa yakitumika kama viwanja vya michezo miaka ya nyuma ili watoto wapate mahali pa kuchezea.
“Hata kama serikali na vyama vya michezo vitahamasisha michezo kuchezwa kuanzia ngazi ya chini bila ya uwepo wa viwanja vya michezo ni kazi bure,” amesema El Maamry.
Hata hivyo, matatizo mengine aliyoyataja kama moja ya vikwazo vya michezo nchini ni maeneo mengi ya wazi yaliyokuwa yakitumiwa na vijana kama viwanja vya kuchezea kuvamiwa na kugeuzwa kuwa makazi ya watu binafsi na kusababisha mpira usichezwe.

Kuhusu uwepo wa Klabu ya Everton, amesema kutakuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa nchi yetu, lakini kwa upande wa soka bila ya marekebisho ya msingi yanayotakiwa itakuwa ni kazi ngumu.
“Ni kweli Everton ni klabu kubwa na kongwe nchini Uingereza iliyoanzishwa mwaka 1878 na inawachezaji wenye majina makubwa duniani lakini ni lazima tujifunze jinsi walivyoweza kufika hapo kuliko kuendelea kupiga makofi.
Pia tunapaswa kujifunza jinsi klabu hiyo ilivyopata mafanikio katika soka kwa kutwaa mataji ya ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza mara tisa na ubingwa mara tano wa Kombe la FA. Ni wazi kwamba ubingwa huo umechangiwa na mipango mizuri na endelevu ndani ya Klabu na uongozi mzuri,” amesema El Maamry.
Naye Rais wa Shirikisho la Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBO) Yassin Abdallah amesema watanzania ni watu wanaopenda michezo ndio maana walijumuika kwa wingi kwenda Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi kati ya Everton na Gor Mahia, lakini tatizo ni ukosefu wa uongozi thabiti.

Amesema kitendo cha serikali kuingilia kati kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kulivunja Baraza la Michezo la Taifa ni ishara kuwa michezo kwa ujumla haiko salama.
Amesema juhudi za dhati zinahitajika kuhakikisha vyama vyote vya michezo vinakuwa na mipango endelevu ya muda mfupi na mrefu ili kuisaidia sekta hiyo kuwa na mafanikio makubwa.
“Tusijidanganye na uwepo wa Everton, hiyo haitoshi kabisa, lazima tujiulize wamefikaje walipo na kwa nini sisi tumeshindwa kufika waliko wenzetu hao walioko mbele?” amesema Abdallah.
Amesema bila jitihada za makusudi tutaendelea kuzishangilia timu za mataifa mengine huku tukiendelea kuwa wasindikizaji katika kila mchezo katika ukanda wa Afrika na duniani kote.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mechi hiyo nahodha wa zamani wa klabu ya Everton, Leon Osman amesema ujio wa vilabu vya kigeni nchini hautakuwa na maana kama soka litakosa mipango endelevu.
“Sio mbaya kama TFF na wadau wengine watajifunza kutoka katika ligi kama Ligi ya Uingereza na nyingine ambazo tayari zimepiga hatua kubwa kuliko kujifungia vyumbani,” amesema Osman.
Amesema ni wajibu wa wahusika kuwekeza katika soka kuanzia ngazi ya chini na kuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi kwa faida ya vilabu na timu za taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala wa SportPesa, Abbas Tarimba akizungumza mara baada ya mchezo huo, amesema wachezaji wa Everton wanatarajiwa kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwa baiskeli kwa lengo la kutangaza utalii nchini.

You may also like