NA MTANDAO

Jitihada zinazofanywa na jumuiya za kimataifa kukomesha mapigano nchini Sudan Kusini zinaonekana kukwama, hali inayoashiria huenda nchi hiyo ikajikuta ikiwekewa vikwazo vya silaha.

Timu inayofuatilia suala la usitishwaji mapigano na inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa nchini humo, imesema kuwa imeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa amri ya kuweka vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

Taarifa hiyo imekuja siku chache baada ya Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, kuliomba Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo vya silaha Sudan Kusini kutokana na kushindwa kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

Balozi Haley ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kuwa Serikali ya Rais Salva Kiir imezidi kujidhihirisha kwa kile alichoeleza kama ‘mshirika asiyefaa’ katika juhudi za kurejesha amani na kuomba viongozi wa Afrika kuiwajibisha.

Sudan Kusini imekabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013, baada ya makabiliano kati ya wanajeshi wanaomtii Makamu wa Rais wa zamani, Riek Machar, na Rais Salva Kiir.

Mapigano hayo yalisababisha mauaji ya maelfu ya raia na kusababisha baa la njaa huku theluthi ya raia wakiyakimbia makazi yao, hali iliyosababisha raia wengi kupoteza maisha hasa wanawake na watoto.

Wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Henrietta Holsman Fore, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba hali nchini humo si ya kuridhisha.

Msemaji wa Serikali ya Sudan Kusini, Michael Maueli Lueth, ameliambia Shirika la Habari la Uingereza (Reuters)  kwamba timu ya  kufuatilia usitishwaji wa mapigano haikuzingatia haki na ilitegemea taarifa kutoka vyanzo vingine.

Amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutakiwa kusikiliza ripoti ya mitaani, badala yake inapaswa kwenda nchini humo na kujionea  kama hayo yanayosemwa yana ukweli wowote.

Kaimu msemaji wa waasi, Lam Paul Gabriel, amesema watakaribisha uingiliaji wowote kutoka jumuiya ya kimataifa ili kutekeleza hatua ya kusimamisha mapigano, lakini akatoa wito wa kuwapo kwa hali ya kuheshimiana.

1905 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!