Mpendwa msomaji natumaini hujambo. Wiki hii nimejikuta kwenye mtanziko wa hali ya juu. Zimekuwapo mada nzito nzito, kwa kiwango nashindwa niandike juu ya ipi na kuacha ipi. Hata hivyo, mambo matatu nitayagusia. Mchango wa Waziri Mkuu wa zamani bungeni, Edward Lowassa, Mkutano wa Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye na hotuba ya mwaka ya Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Lowassa, wakati anatoa mchango wake bungeni wiki iliyopita alitaka nchi hii iwe na vipaumbele vya msingi vitatu — ajira, elimu na reli. Amezungumzia mambo haya bungeni na kwa uwazi, ila baada ya hapo ukaibuka mjadala mkubwa.

 

Hoja ya Lowassa ni kwamba Tanzania kwa hali yoyote haiwezi kupuuza suala la ajira kwa vijana ikabaki salama. Anataka Serikali iende mbali kidogo ilazimishe wawekezaji kutenga nafasi za ajira kwa vijana wetu. Pia suala la elimu, nadhani sina sababu ya kulisisitiza. Kama tumeamua kutawaliwa, basi tuchague kutokwenda shule.


Suala la reli nimelizungumza mara nyingi. Hatuwezi kuendelea kwa kusafirisha mzigo kwa njia ya barabara. Nchi zote zilizoendelea duniani zimeendelea kwa kusafirisha mizigo yake kwa kutumia reli. Mzigo unaosafirishwa na treni moja inayovuta mabehewa 30 unaweza kusafirishwa na malori yasiyopungua 70. Ukipita katika barabara za nchi hii utabaini athari za malori haya.


Sitanii, barabara zinajengwa na zinaharibika ndani ya muda mfupi. Malori yanaharibu barabara. Malori haya yanamilikiwa na wakubwa. Si ajabu hata kwenye mitandao ya kijamii wamo wamiliki wa malori, ndiyo maana wanayatetea na kupinga hoja ya Lowassa ya kuimarisha reli baada ya kusifia juhudi zinazofanywa na Dk. Harrison Mwakyembe kufufua reli.

 

Nasema ingewezekana, leo tungesafirisha mizigo yote kwa kutumia reli. Tungewekeza kwenye reli ya umeme. Treni ingeweza kutoka Dar es Salaam saa 12 asubuhi ikafika Kigoma saa 6 mchana.


Kwa kufanya hivyo, kasi ya usafirishaji mizigo ingeongezeka na uchumi ungekua kwa kasi kubwa. Inawezekana baadhi ya watu hawampendi Lowassa, lakini si busara kupuuza mawazo mazuri anayotoa. Nchi hii inahitaji maendeleo na si siasa za nani atakuwa Rais 2015. Tanzania kwanza.


Sitanii, suala la pili ni mkutano wa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, na wanahabari alioufanya Novemba 5, 2013. Sumaye alilalamika. Alizungumza mengi kuwa anahujumiwa na watu aliowaita mafisadi katika mialiko anayopewa. Akasema ilikuwa afungue Saccos Muleba akahujumiwa. Akasema Shirika la Faita Jogging Sports Clubs lilimwalika, kisha aliowaita mafisadi wakahujumu mwaliko wake, ambapo angepokea mbio eneo la Mnazi Mmoja.


Mwenyekiti wa Shirika hilo, Steven Kahema, amekana kumwalika Sumaye kwa kazi hiyo. Hata hivyo, Sumaye alisema anayo mialiko mingi kiasi anashindwa kuhudhuria yote. Najiuliza sasa nini kinamlalamisha?


Pamoja na hayo, maneno kuhusu mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Mwanza hadi Kahama, Shinyanga, Sumaye alisema: “Najua mhusika [Lowassa] ametumia sana mradi huu [wa maji Shinyanga] kisiasa na wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli kuhusu mradi huu, kwa sababu mimi nilikuwa Waziri Mkuu na mradi umetekelezwa chini ya uangalizi wangu.


“Kama waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi mkubwa hivyo peke yake, akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma? Mbona kuna sehemu Kanda ya Ziwa bado zina shida ya maji?” alisema Sumaye.


Sitachangia mengine, ila nukuu hii ambayo nimeisoma katika magazeti si chini ya sita, imenikumbusha kikatuni fulani kilichokuwa kikichorwa katika magazeti kwenye miaka 1995.


Simkumbuki jina la mhusika mmoja ila alikuwa anachorwa akizungumza na TINA, na kila swali aliloulizwa alikuwa akianza na jibu la ‘SIMPO’, kisha anafyatua jibu ambalo hukutarajia. Nikiri, sisemi Sumaye amekuwa kama mhusika huyo, ila kwa kiwango kikubwa nukuu hii imekuwa kinyume na matarajio yangu na pengine ya wengine wengi, hasa aliposema:

“Pamoja na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo mkavu, mhusika kama waziri mwandamizi wakati huo, na sasa anawinda nafasi kubwa katika nchi, hakutarajiwa kutoa siri za Baraza la Mawaziri, labda amediriki kufanya hivyo kwa sababu anajua anayosema siyo ya kweli, vinginevyo ni kosa la jinai na akishitakiwa anafungwa jela,” alisema Sumaye.

Kuna hoja usizotarajia zitolewe na Waziri Mkuu aliyetumikia nchi kwa miaka 10 katika wadhifa huu mzito. Suala la kwamba Lowassa alipokuwa Waziri Mkuu angeweza kufikisha maji Dodoma, basi ni masikitiko kusikia hoja ya aina hii ikitoka kinywani mwa mtu anayejua mfumo wa utendaji wa Serikali. Kwamba Lowassa aliusimamia mradi huu, hilo sina hata chembe ya shaka kuwa ni kweli.

Sitanii, mwaka 2004 nilikuwa jijini Cairo nchini Misri. Lowassa alikuja pale Cairo na Kamati ya Bunge. Ninaowakumbuka katika Kamati hiyo ni Said Nkumba, Thomas Ngawaiya, na marehemu Shaweji Abdallah. Najua walikuwapo wengine watanisamehe kwa kutowataja hapa kwani sikuwa nimetunza kumbukumbu hizi.

 

Kwa waliokuwapo pale kwenye Hoteli ya Conrad wanakumbuka alichosema aliyekuwa Waziri wa Maji wa Misri, Dk. Abu Zeid, na waziri mwingine ninayemkumbuka kwa jina moja, mwanamama, Dk. Atia. Hawa walisema Misri ilikuwa tayari kuipiga Tanzania vita iwapo ingechukua maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga na Kahama. Lowassa aliwaambia kitu kimoja tu: “Kama mnataka kutupiga vita kwa ajili ya sisi kuwachukulia watu wetu maji kutoka Ziwa Victoria, tuko tayari hata sasa hivi, njooni.”

Nakumbuka Mwandishi Lucas Liganga aliwauliza mawaziri hao wa Misri kuwa inakuwaje wao wanataka Tanzania isichukue maji kutoka Ziwa Victoria, wakati katikati ya Jiji la Cairo wanatumia maji ya Mto Nile yanayoaminika kutoka Ziwa Victoria kuendesha mitumbwi ya starehe (boat ridding). Baada ya msimamo huo wa Lowassa, Wamisri walinyamaza na mradi ukatekelezwa.

Sitanii, inawezekana mradi huu ulipitishwa na akina Pius Ng’wandu kama alivyosema Sumaye, lakini naamini walishindwa kuutekeleza kutokana na kuogopa vitisho vya Wamisri. Yeyote anayejifanya kuufumbia macho ukweli huu, anapaswa kuchunguzwa kwa kila hali. Inawezekana Sumaye anamchukia Lowassa, lakini basi tuazime msemo wa “Baniani mbaya, kiatu chake dawa.”

Kabla sijaandika makala haya, nimejaribu kuuliza nini kimemfanya Sumaye ajilipue kiasi hiki mbele ya Lowassa. Kwa watu wa Hanang’ nimepata majibu kuwa Sumaye anaamini Lowassa alimmwagia Waziri Dk. Mary Nagu fedha za uchaguzi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na kwa kutumia fedha hizo akambwaga katika uchaguzi wa mwaka jana.

Hilo limerudiwa na wengi na mara nyingi, ila mimi nasema Sumaye analaumu alipoangukia. Mwaka 2005 katika mchakato wa kumpata mgombea urais, Sumaye alikuwa mmoja wa watu waliobaki katika hatua ya tano bora. Mwanzo walikuwa 11, ila wakabaki Jakaya Kikwete, Salim Ahmed Salim, Mark Mwandosya, Abdallah Kigoda na Frederick Sumaye.

Kura zilipopigwa, Kikwete, Salim na Mwandosya wakaingia katika hatua ya tatu bora. Baadaye Kikwete aliwashinda katika mzunguko wa kwanza kwa kupata kura zaidi ya 1,800 kati ya 2,500 za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM. Baada ya matokeo haya, Sumaye alitangaza kuwa hataki tena siasa na atawashauri watoto wake milele wasiingie kwenye siasa, kwani siasa ni mchezo mchafu na watu si waaminifu.


Sitanii, kauli hii aliitekeleza kwa vitendo kwa kumwachia kiti cha ubunge Mary Nagu mwaka 2005. Baada ya mwaka 2007 si ajabu alipiga moyo konde akaenda kusoma Shahada ya Uzamili ya Uongozi. Hapa nilijiuliza Sumaye anasoma shahada ya uongozi kumwongoza nani? Familia yake, ukoo wao au nchi jirani, maana yeye alikwishatamka kuwa hataki tena siasa.

Sasa wiki iliyopita, amenivunja mbavu alipoulizwa iwapo atagombea urais au la akasema: “Nasema hivi, kama ni kugombea nina haki zote, kama ni uwezo ninao, kama ni imani ya Watanzannia kwa sehemu kubwa ninayo. Kilichobaki ni uamuzi tu wa mimi kutamka. Kwa hiyo, sijatamka msije mkasema nagombea urais. Nasema tu na mimi katika Watanzania wanaofikiriwa na mimi nimo. Kwani ninyi [waandishi] hamnifikirii? Sasa itakapofika huko mbele, si utaamua wakati huo?”

Nimejiepusha kurudia maneno mengi aliyosema dhidi ya Lowassa, ila mimi kwa tafsiri yangu, nisameheni kwa wanaoliangalia kwa jicho jingine jambo hili, mengi kati ya maneno ya Sumaye kwenye mkutano huo yalikuwa matusi dhidi ya Lowassa. Sasa najiuliza, je, matusi ya Sumaye dhidi ya Lowassa yatamsaidia kupata urais wakati wa kutangaza nia ukifika? Jibu ninalopata ni kuwa anajidhalilisha.

 

Bora anadi sera zake badala ya kupambana na majina ya watu. Watanzania tunahitaji kuelezwa ukichaguliwa kuwa Rais utalifanyia nini Taifa hili, na si kwamba uliwahi kumtukana nani mara ngapi. Inawezekana mbinu hii itasaidi, ila sitaki kuamini hivyo.

Jambo la tatu na la mwisho, si kwa umuhimu ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete bungeni siku ya Alhamisi ya wiki iliyopita. Maelezo aliyoyatoa Rais Kikwete yameendana na mtazamo wangu. Moyoni nilikuwa najiuliza sisi Tanzania tunazungumza nini juu ya haya yanayoendelea? Rais Kikwete amenena vyema.

Wapo watu wanaosema hotuba ya Rais Kikwete haikuwa kali, mimi nasema hawa hawafahamu. Katika diplomasia kauli aliyoitoa Rais Kikwete mbele ya Bunge ni mwiba mkali kwa nchi za Kenya, Rwanda na Uganda.

 

Narudia, nchi hizi zimeanzisha umoja wao ndani ya EAC si kwa sababu ya jambo jingine lolote, bali ni kwa sababu tu matarajio yao hayakutimia. Walidhani na wanatamani kuwa Tanzania yenye asilimia 52 ya ardhi yote ya Afrika Mashariki ingekuwa kimbilio lao. Wanatamani na wanadhani kuwa watu wao wangeruhusiwa kuja kuishi hapa nchini, hata kama hawana kazi ya kufanya.

 

Wanatamani na wengine wanafanya kila hila, kuona Rais Yoweri Kaguta Museveni anakuwa Rais wa Kwanza wa Afrika Mashariki, bila kujali faida na hasara ya haraka hii. Rwanda inatajwa na ndio ukweli, kwamba imechochea kwa kiasi kikubwa baada ya Tanzania kupeleka majeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kufurusha waasi wa M23, Rwanda haikufurahi.

 

Sitanii, kunaweza kuwapo uhusiano kati ya Tanzania kupeleka majeshi DRC mwezi Aprili, na nchi hizi kuamuza kuanzisha umoja wao mwezi Juni. Bila shaka walikereka. Tunakumbuka na maneno yaliyopita hapo katikati. Kwa vyovyote iwavyo, nasema inafaa tufuate utaratibu wa kisheria ambao Rais Kikwete ameueleza bayana.

 

Tusiruke ngazi, bali tuanze na umoja wa forodha, tukimaliza tukamilishe soko moja, kisha twenda sarafu moja na hapo ndipo twende kwenye mchakato wa shirikisho la Afrika Mashariki litakaloidhinishwa na wananchi baada ya kura ya maoni. Kwa hili nasema, Kikwete amefanya vyema, sasa tunasubiri kusikia hawa wenzetu watasemaje, baada ya kauli hii ya Rais Kikwete.

By Jamhuri