Mheshimiwa Spika, awali ya yote tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa Bunge lako tukufu kwa kutambua uwepo wetu hapa bungeni leo hii.

Ni dhahiri kwamba sisi wanyamapori hatuna kambi rasmi hapa bungeni lakini tunapenda kuwasilisha taarifa yetu rasmi kuhusu Operesheni Tokomeza iliyoanzishwa nanyi kupitia Wizara yenu ya Maliasili na Utalii.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Wanyamapori inatambua mipaka tuliyowekewa na binadamu na ndio maana siku zote tumekuwa tukiheshimu hilo. Hakika kama tusingeliheshimu hilo, hakuna binadamu ambaye angeendelea kupeta katika uso huu wa dunia. Kwani pamoja na matumizi yenu ya silaha za moto dhidi yetu bado tungeweza kuwaangamiza. Lakini uvumilivu wetu umekuwa ndio chimbuko la maafa yetu.


Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza inayoendeshwa chini ya usimamizi wa Jeshi     la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ilikuwa wapi siku zote? Tunauliza hivyo kwa kuwa kwa muda wa miongo kadhaa iliyopita, tumekuwa tukiuawa ovyo ovyo eti kwa kuwa sisi tuna thamani kubwa kwenu kimaslahi.


Jeshi lenu siku zote limekuwa ni jeshi la kulinda mipaka ya nchi lakini si mipaka yetu mliyotuwekea sisi Wanyamapori. Matokeo yake askari wachache ambao mmewapa jina la Kikosi cha Kupambana na Ujangili, wamekuwa ndio chanzo kikuu cha maafa yetu, wakishirikiana na baadhi ya Maafisa mbalimbali wa Wizara yenu ya Maliasili na Utalii, baadhi ya viongozi wa kisiasa wakiwemo Wabunge na kundi lingine ni la wafanyabiashara haramu, ambao wao ndio wameshikilia mtandao mzima wa ujangili dhidi yetu.


Mheshimiwa Spika, sisi wanyamapori tunasikitika kwa nyinyi kuamua kuitangaza Operesheni Tokomeza hadharani. Kwani kwa kufanya hivyo, majangili wengi wamejificha na kuficha ngozi zetu, pembe zetu, meno yetu, kucha zetu na hata nyama zetu. Mlichoambulia na mtakacho endelea ni kuwakamata hao maafisa wachache ambao wengine mmewakuta na silaha na risasi za serikali yenu majumbani mwao, pamoja na baadhi ya viungo vyetu.


Hao wana visingizio vingi hamtaweza kuwatia hatiani. Watawaambia viungo vyote mlivyovikamata si vyao bali wameamua kuvihifadhi kwa kuwa hawana maghala ya kutosha.

Viungo vyetu wamevipata baada ya kuwakamata majangili ambao nao baada ya kuwazidi maarifa- baada ya kuwapa hongo, wakaamua kuwaachia. Si mmesikia wenyewe RCO wenu wa Arusha anatuhumiwa kwa kutorosha majangili wawili. Kutoka Saudi Arabia; Alhassana Alli Anwayship na Nadaar Ali Mbooh. Sasa hili mmelibaini hivi karibuni, miaka yote mlikuwa wapi? MaRCO wangapi wamepita Arusha na kwingineko tulipo sisi? Si inawezekana huyo alifuata nyayo za waliotangulia? Kwani mnapokabidhiana ofisi za serikali si mnapeana na mikakati yenu binafsi ya maisha, nje ya utumishi wa umma?


Mheshimiwa Spika, kila mara Serikali yenu kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inapoteua Maofisa Wanyamapori, wateule hao baadhi yao hufanya sherehe kabambe, wakijua wameshaukata, wamepata “ulaji”. Kama hamwamini hilo angalia orodha ya Maofisa Wanyamapori waliokamatwa hivi karibuni na ambao bado wanahojiwa. Hata mkiwahoji na kuwaondoa kazini, bila kuwa na mipango na mikakati yenye kulenga kuendelea kuuenzi “unyama” wetu tulionao, sisi Wanyamapori tutaendelea kutoweka tu, na kuuachia nyie “utu” wenu.


Mheshimiwa Spika, sisi wanyamapori tunaomba Bunge lenu tukufu ligeuke kuwa kamati ili lisikilize mapendekezo yetu kwa Serikali yenu sikivu na imara, si legelege kama wasemavyo wapinzani wenu wakuu kisiasa. Sisi hatuwezi kulisema hilo kwa kuwa bado tuna imani nayo.


Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya wanyamapori, inayowakilishwa na Tembo na Faru kwa niaba ya wanyamapori wote, tunaliomba Bunge lako tukufu kuanzisha kikosi maalumu kutoka JWTZ ambacho kitakuwa kikijihusisha moja kwa moja na ulinzi wa mipaka yetu. Kikosi hiki kiwe ni cha kudumu. Na tunapendekeza kiitwe “Okoa maisha ya wanyamapori”.


Kwa kuwa binadamu tunajua hulka zenu ili kikosi hiki kisirithi maovu ya kikosi kilichotangulia, basi tunaomba kiwe na Katiba yake itakayoelezea umuhimu wetu kama wanyamapori, wajibu wetu ni kuwaingizia pato kubwa la taifa lenu kutokana na kuwaleta wenzenu kuja kutushangaa hususan watu weupe. Sasa ili tuendelee kutimiza hilo ni lazima haki yetu ya kuishi iheshimiwe.


Mnaweza mkaunda Operesheni lukuki na mkajikuta mnapoteza mamilioni ya shilingi na tatizo likawa pale pale.


Aidha Katiba yenu hiyo itatakiwa ioneshe wanyama ambao hata sisi tumeridhia muwawinde kwa ajili ya chakula chenu. Na vitalu vyote mlivyogawa kiholela vifutwe na ianzishwe sheria nyingine ya umiliki wa vitalu hivyo. Tunashauri iundwe kamati maalumu ya kudumu itakayoundwa na wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na wajumbe wengine kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kupitia Wizara ya Ulinzi. Kamati isiusishe wanasiasa hata kidogo.


Mheshimiwa Spika, aidha kambi rasmi ya wanyamapori, inashauri Maofisa wanyamapori wawajibike moja kwa moja kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira. Hatuna uhakika hilo kama ndivyo lilivyo. Tunashauri hivyo kwa kuwa utendaji wao unaweza kuimarika kwa maana ya kuwekewa uangalizi wa hali ya juu. Watatakiwa wawajibike moja kwa moja kwa Makamu wa Rais. Ripoti zao zote zipitie Ofisi ya Makamu wa Rais, Kitengo cha Mazingira kwani imeonekana idadi kubwa ya watumishi katika Wizara ya Utalii na Maliasili wanatiliwa shaka katika suala zima la kupambana na ujangili.


Aidha tunapendekeza kuwa yeyote atakayekamatwa na viungo ambavyo nyie ni nyara zenu, basi aende jela maisha. Tatizo lenu adhabu mnazozitoa ni ndogo mno kiasi wakati mkijua majangili ni mijitu yenye ukwasi mkubwa. Na atakayebainika kula rushwa adhabu iwe ni hiyo hiyo.

 

Mkiwafanyia watu kumi tu mtatufuata porini kutueleza. Aidha kesi zenu zinachelewa mno, mathalani mtu anakamatwa leo na viungo vyetu lakini kesi itachukua muda wa miaka mitatu. Hapa mnategemea nini kama si kupotezana ushahidi. Si mmeona wenyewe mtu akikamatwa na kilo mathalani 20 za pembe za ndovu, wajanja wanaziuza halafu wanatafuta vipembe “kiduchu” wanageuza ndio ushahidi wenyewe. Si hatari sana! Mnatuua sisi halafu bado mnaendelea kudanganyana wenyewe kwa wenyewe. Kweli binadamu mna mambo, si utani.


Mheshimiwa Spika, baada ya Operesheni Tokomeza kukamilika, tunaomba tuje tena hapa bungeni tuelewe kwa kina idadi ya wenzetu waliouawa tangu mpate Uhuru wenu mwaka 1961. Ni viungo vya wanyama gani vilivyopatikana na viko wapi na wahusika waliokamatwa ni wangapi na wangapi miongoni mwao wanatumikia vifungo hadi sasa. Na wangapi waliachiwa huru na kwa nini. Sisi hatutalipiza kisasi, kwa sasa tumewasamehe. Ila hatutaki kuona Operesheni Tokomeza  inaondoka na minofu ya wenzetu kama kitoweo japo wana kazi ngumu wanazozifanya kuhakikisha uhai wetu unalindwa lakini na wao lazima wawe na vibali halali vya uwindaji.


Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya wanyamapori inategemea Bunge lako tukufu litapokea taarifa hii na kuipitia vipengele vyote kabla ya kutolewa maamuzi. Naomba kuwasilisha hoja.


Asanteni kwa kunisikiliza japo wengine walikuwa wanauchapa usingizi wakati nilipokuwa nikisoma taarifa hii.

0763 – 400283

E-mail: [email protected]


 

By Jamhuri