Serikali isisaidie shule za watu binafsi

Wazo limetolewa la kuitaka Serikali isaidie shule za watu binafsi na tayari wazo hilo limeanza kupigiwa debe serikalini.

Akizungumza mjini Dar es Salaam kwenye Mahafali ya Darasa la Saba katika Shule ya St. Anne Marie Academy, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema kwamba baadhi ya shule za watu binafsi zinafungwa kutokana na kushindwa kujiendesha na hiyo ni kwa sababu ya kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Naibu Waziri Simbachawene aliendelea kusema kwamba lengo la wazo la Serikali la kusaidia shule za watu binafsi, ni kutanua wigo wa kutoa ruzuku hadi shule zinazomilikiwa na watu binafsi.

Tukizama kwenye historia ya Tanganyika tutaona kwamba ilikuwa mwaka 1927 Serikali ya Mwingereza Tanganyika ilipoanza kutoa ruzuku kwa shule binafsi. Huo ulikuwa wakati wa Donald Cameron, Gavana wa Pili wa Tanganyika.

Wakati Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa Rais wa TANU na kuhutubia Umoja wa Mataifa Desemba 20, 1956, alikiri kuwa katika utawala wa Kiingereza Tanganyika, magavana wengine wote walitawala kana kwamba ni koloni isipokuwa Gavana Donald Cameron.

Cameron alitambua kuwa Tanganyika haikuwa koloni bali ilikuwa Nchi ya Udhamini na jukumu la Serikali ya Kiingereza lilikuwa kuwatayarisha Watanganyika kwa kujitawala wenyewe.

Cameron, ambaye aliingia Tanganyika mwaka 1925 akitokea Nigeria, ndiye Gavana wa Tanganyika aliyeleta mabadiliko makubwa zaidi katika mambo ya utawala Tanganyika.

Kwa mfano, mwaka 1926 alianzisha Baraza la Kutunga Sheria lililozaa Bunge la Tanganyika mwaka 1961. Mwaka huo huo (1926) Cameron alianzisha majimbo yaliyozaa mikoa mwaka 1962.

Mwaka 1927 Cameron alianzisha mfumo wa utawala ulioshirikisha viongozi wa jadi (Serikali za Mitaa). Mwaka huo huo pia Serikali yake ikaanza kutoa ruzuku kwa shule za misheni. Wakati ule ni shule za misheni tu zilizotambulika kuwa zitatumia vyema ruzuku kwa manufaa ya watoto Waafrika.

Binafsi nilisoma wakati wote shule za misheni na ni shahidi wa kuthibitisha wamisheni walivyotumia ruzuku vizuri. Kwa mfano, mwaka 1947 niliingia shule ya bweni kwa masomo ya darasa la nne. Ada waliyotozwa wazee wetu ilikuwa shilingi tatu kwa mwaka. Shilingi hizo tatu zilituwezesha kupata kitanda, shuka, blanketi, sare, chakula mwaka wote wa shule, madaftari na vitabu vya masomo yote.

Wakati ule wamisheni hawakuendesha shule au elimu kibiashara. Lakini leo karibu shule zote za watu binafsi zinafanya biashara. Na sasa Serikali inatafakari kuzipa ruzuku hizo! Tuanzie hapo.

Hapana shaka shule za watu binafsi zinazofungwa ni za watu walioshindwa kufanya biashara ya elimu. Kwa hiyo, kwa nini wasaidiwe?

Watu hao wameshindwa kuendesha biashara ya elimu kwa sababu wamekosa mipango mizuri ya kuwasaidia kuendesha elimu kwa ufanisi. Kwa hivyo, kwa nini wasaidiwe?

Ufanisi katika jambo lolote hautokani na fedha. Unatokana na umakini. Kwa hivyo, kwa nini Serikali iwasaidie watu waliokosa umakini? Si itakuwa inapoteza tu fedha ya umma? Halafu si siri karibu shule zote za watu binafsi zinafanya vizuri. Kwa upande mwingine karibu shule zote za Serikali zinafanya vibaya.

Kwa nini shule za watu binafsi zinafanya vizuri? Kampuni ya Mtembei Holdings Limited inayomiliki Shule za St. Mathews, Victory na Ujenzi zilizopo Mkuranga Mkoa wa Pwani, pia ya St. Marks iliyopo mkoani Dar es Salaam ina majibu. Shule zote hizo za kampuni hiyo zinafanya vizuri sana katika masomo na mitihani kwa sababu hazina upungufu wa jambo lolote, kwani mazingira ya shule hizo yako vizuri kuanzia maabara, walimu wanapewa mishahara mizuri na motisha, na vifaa viko vya kutosha kiasi cha kutokuwa na mwanya kwa wanafunzi kufanya vibaya katika masomo yao.

Wakati huo huo, mwaka huu peke yake kwa upande wa motisha walimu 25 wa shule hizo walipelekwa ziara ya mafunzo Dubai, na kila mmoja alipewa fedha ya kununulia gari ili awahi shuleni pia alipewa fedha ya kununulia kompyuta mpakato (laptop). Kwa upande wa shule za Serikali hakuna ziara zozote za mafunzo za walimu kwenda nchi za nje.

Juu ya yote hayo, hata wanafunzi wa shule za Serikali hawapati masomo yao ipasavyo. Mbali na udogo wa mishahara yao, walimu wengi wamepandishwa madaraja miaka mingi iliyopita lakini hawapewi mishahara inayolingana na madaraja yao.

Vyumba vya madarasa havitoshi; hakuna nyumba za walimu, madawati hayatoshi, na kadhalika.

Katika mazingira hayo Serikali itakuwa imefanya kosa kubwa ikitoa ruzuku kwa lengo la kuboresha elimu katika shule za watu binafsi, ambayo tayari ni bora badala ya kuboresha elimu katika shule zake.

Kwa upande wa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN) ukweli ni kwamba mpango huo ulianza kutekelezwa shule za watu binafsi siku nyingi tena kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande wa shule za Serikali, bila Serikali kutumia fedha ya kutosha kuongeza kipato cha walimu itakuwa vigumu kupata matokeo makubwa sasa.

Na hapana shaka walimu wa shule za Serikali walipata habari kwamba Serikali imeamua kuboresha shule za watu binafsi badala ya kuboresha shule zake, hilo peke yake litawavunja sana moyo walimu hao.

Kibaya zaidi Serikali ikianza kutoa ruzuku kwa shule za watu binafsi kila mwenye uwezo mdogo wa kifedha ataanzisha shule yake ya msingi. Halafu utakapokuja mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba nafasi zote za kidato cha kwanza shule za Serikali zitazibwa na wanafunzi kutoka shule za watu binafsi.

Inavyoonekana wazo la Serikali limetokana na watu waliopo serikalini ambao ama tayari wana shule au wanataka kuanzisha shule. Bunge lisithubutu kupitisha wazo hilo.