url-3Miaka kumi iliyopita Serikali imetumia Sh bilioni 2.5 kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi, hasa nchini India. 

Takwimu kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinaonyesha kuwa kati ya Januari mpaka Juni 2016, Serikali imetumia Sh milioni 220, yaani wastani wa Sh milioni 22 kwa kila mgonjwa ($10,000) kupeleka wagonjwa 10 kwenda kupatiwa matibabu ya moyo nchini India.

Hali hiyo ya kutumia gharama kubwa kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi kupatiwa matibabu ya moyo imepatiwa ufumbuzi hapa nyumbani baada ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo kwa siku za karibuni imeonyesha mafanikio makubwa.

Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Taasisi ya Tiba za Moyo, Jakaya Kikwete Cardiac Institute Dk. Pedro Pallangyo anasema;

“Magonjwa ya Moyo (Cardiovascular Diseases), ni miongoni mwa magonjwa yaliyoko kwenye kundi la magonjwa yasioambukiza (NCDs). “Haya ni magonjwa yote yanayoathiri moyo na mishipa yake na kuhatarisha maisha ya binadamu.

“Magonjwa ya moyo yanajumuisha ugonjwa wa Kupanda kwa Shinikizo la Damu (High Blood Pressure Hypertension). Hili ni tatizo sugu la kiafya linalohusisha kuongezeka kwa mgandamizo wa msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu.”

Anasema magonjwa mengine  ya mishipa ya moyo (Coronary Heart Diseases) yanatokana na mafuta kuganda ndani ya mishipa na kuziba kwa kiasi fulani au kuziba kabisa mishapa ya moyo (coronary artery diseases), hivyo kufanya upungufu wa damu katika sehemu ya moyo ambao hupata damu kupitia mishipa hiyo.

Ugonjwa huu wa mishipa ya moyo hudhoofisha misuli ya moyo kiasi cha kufanya moyo kushindwa kusukuma kiwango cha kutosha cha damu na kuchangia ugonjwa unaofanya mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio wa kawaida (arthymias).

Kuna ugonjwa wa moyo unaoitwa Atherosclerosis hali hii ni kitendo cha mafuta kuganda kwenye mishipa ya damu (arteries). Inaweza kuchukua miaka mingi. Kadri miaka inavyosonga mbele, ndivyo mafuta haya yanazidi kuwa magumu na kuzuia msukumo wa damu yenye hewa safi (Oxygen) kwenye moyo.

Anaongeza kuwa ikiwa mafuta yataziba kabisa kwenye mishapa ya moyo (coronary arteries) na kufanya misuli ya moyo kukosa damu yenye hewa safi, huzaa maradhi mengine yanayoitwa Angina (aina ya mstuko wa moyo).

Aneurysm ni aina nyingine ya ugonjwa wa moyo ambapo mishipa ya damu (artery) huvimba kama puto kutokana na kuharibika kwa mishipa au kudhoofika kwa kuta za mishipa hiyo.

Ikitokea mishipa ya damu kupasuka, huvujisha damu kwenye ubongo, hivyo mtu kukumbwa na kiharusi (stroke).

Kiharusi ni ugonjwa wa kupooza unaotokana na kuingiliwa au kupungua kwa usambazaji wa damu kwenye ubongo hali inayozifanya seli za ubongo kukosa hewa safi na virutubishi.

Ugonjwa mwingine wa moyo hujulikana kwa jina Rheumatic Heart Disease, huu ni ugonjwa unaoharibu valvu za moyo (jumla zipo 4). Congenital Heart Diseases, haya ni magonjwa ya moyo ambayo mtoto anazaliwa nayo, na mara nyingi huzaa vifo kwa watoto.

Peripheral Vascular Disease ni ugonjwa mwingine wa moyo kwenye mishipa ya damu ambao mara nyingi  hutokea kwenye mfumo wa usambazaji wa damu nje ya ubongo na moyo.

Mara nyingi, ugonjwa huu huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, hasa wavutaji wa sigara na wenye kisukari.  Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza kama yalivyo magonjwa ya moyo, kila mwaka huua watu zaidi milioni 38 duniani. Vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na magonjwa ya moyo.

Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa hayo ya moyo, yakifuatia magonjwa ya saratani yanayoua watu takriban milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa yanauwa watu milioni nne na kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka. 

Kwa upande wa Tanzania, takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto nchini (PAT), zinaonyesha kwamba takriban watoto 13, 600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa aina mbalimbali ya moyo, huku watoto wastani wa watoto 3,400 kati yao, wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.

Kinachosikitisha hadi sasa katika tasnia ya magonjwa ya moyo, ni kwamba mtu anaweza asione dalili za moja kwa moja za magonjwa ya moyo, hadi wakati mishipa ya damu ya moyo inapokuwa imeziba kabisa au kushindwa kuruhusu damu kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.

Mara nyingi, hakuna dalili inayojitokeza moja kwa moja kwa wagonjwa wa aina hii, hadi pale moyo wenyewe unaposhindwa kufanya kazi ghafla (heart attack/sudden death) au mtu anapopata kiharusi (stroke).

 Zaidi ya maelezo hayo ya wataalam wa magonjwa ya moyo, dalili zinapojitokeza mapema hutofautiana kwa kutegemea aina ya ugonjwa wa moyo, ingawa dalili hizo nazo hazijitokezi mapema kama ilivyo kwa magonjwa mengine.

Hata hivyo, dalili kuu za magonjwa ya moyo ni pamoja na maumivu ya kifua upande wa kushoto (hii ni dalili kuu ya ugonjwa wa moyo); moyo kwenda mbio na kumfanya mtu akose pumzi au kushindwa kupumua; kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingoni kujitokeza nje.

Dalili nyingine ni maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya; tumbo kujaa, kichefuchefu, na kutapika; kukosa usingizi; kupoteza fahamu na kikohozi kisichokwisha.

Anasema, jambo muhimu ni kwamba hadi dalili hizo zijitokeze wazi, ni kwamba mtu huyo amekuwa akiishi na ugonjwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo, njia bora ya kugundua dalili ya ugonjwa wa moyo ni kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara angalau mara moja kwa mwaka.  Endapo mtu atahisi maumivu ya aina yoyote kifuani, hasa baada ya kufanya mazoezi, ni muhimu kuonana na daktari haraka.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) zilizotolewa mwaka 2011, vifo vilivyotokana na magojwa ya moyo nchini Tanzania vilifikia idadi ya watu 19,083 au asilimia 4.33 ya idadi ya vifo vyote.   Na takwimu hizo zilionyesha idadi ya wanaofariki ni watu 117.64 kati ya watu 100,000. Takwimu hizi zinaiweka Tanzania katika nafasi ya 87 duniani kati ya nchi karibu 200.

Magonjwa haya ya moyo huchangia  vifo vingi duniani kote. Hata hivyo, Shirika la Afya duniani limefanya jitihada za makusudi kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo na mambo yanayochangia kuongezeka kwa vifo hivyo.

Katika kuonyesha kukua kwa maendeleo ya kiteknolojia ya huduma za afya, Hospitali ya Apollo ya mjini Gujarat katika mji wa Ahmedabad, ilifanikiwa kufanya upasuaji unaojulikana kitaalam kama  ‘Bentall Surgery’ kwa mwanamke aliyekuwa na zaidi ya miaka 50.

Upasuaji wa aina hii mara nyingi ni adhimu kufanyika katika nchi ambazo ni maskini na zenye wataalamu wachache au zenye mfumo wa chini  wa huduma za afya.

Ni katika muktadha huo, Serikali ya Tanzania imeanzisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Lengo la Serikali kuanzisha taasisi hii ni kuboresha huduma za tiba za rufaa nchini kupunguza idadi ya rufaa za wagonjwa nje ya nchi hasa wagonjwa wenye matatizo ya moyo.

Dk. Pallangyo anasema  kati ya mwaka 2000 hadi 2014 wagonjwa 7,363 walipewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi hasa nchini India.  Pia, kati ya mwaka 2012 na 2015 wagonjwa 1,465 walitibwa nje ya nchi kwa gharama za Serikali hali iliyozaa usumbufu mkubwa kulingana na ufinyu wa bajeti.

Anasema karibu asilimia 50 ya wagonjwa waliotibiwa nje ya nchi kwa gharama za Serikali kati ya mwaka 2012 hadi Novemba, 2015 walikuwa wanaugua magonjwa ya moyo.

Anasema hali hiyo iliilazimu Serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutafuta matibabu nje ya nchi.  Kutokana na ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo mwaka 2008 Serikali iliamua kuanzisha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo na hatimaye kujenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambayo ilianza Septemba 5, 2015 ikilenga kukabiliana na tatizo hili.

Dk. Pallangyo anasema kuhakikisha wanafanya kazi kiufanisi, taasisi hiyo ina uhusiano na taasisi nyingine za kimataifa kwa lengo la kubadilishana ujuzi.

Anazitaja taasisi hizo kuwa ni taasisi ya Save the Childs Heart (SACH) kutoka nchini Israel, Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani, Al Muntada kutoka Falme za Kiarabu, Mending Kids International kutoka nchini Australia.

Anasema ushirikiano huu umewawezesha kama taasisi kutoa mafunzo hapa hapa nchini kwa wataalamu waliopo kwenye taasisi lengo ikiwa ni kuboresha utendaji na ufanisi kwa wataalamu wetu.

Anaendelea kusema kama taasisi inayojitegemea wamejipanga kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na ya kuridhisha kwa wagonjwa.

 Dk. Pallangyo anasema tangu kuanza kwa taasisi hii kambi maalumu za upasuaji moyo zimekuwa zikiendeshwa na wataalamu wa hapa nchini kwa kushirikiana na wataalamu  kutoka nje ya nchi ambapo jumla ya wagonjwa 197 wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa mwaka huu 2016.

Kambi za upasuaji zimesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa ambao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Hatua hii imepunguza gharama kwa Serikali kwani idadi ya wagonjwa wa moyo waliopata rufaa imepungua kutoka 198 hadi 89 kati ya mwaka 2013 na Novemba 2015.

Matibabu nje ya nchi yana gharama kubwa ambazo zinatofautiana kulingana na ugonjwa wa moyo husika.

Gharama za kumtibu mgonjwa mmoja wa moyo ni Sh 16,500,000 mgonjwa mmoja wa figo ni Sh 57,750,000 na mgonjwa mmoja wa saratani ni Sh 74,250,000.

Matumizi ya fedha kwa ajili ya matibabu nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka kulingana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa.

Kuongezeka idadi ya wagonjwa wa rufaa kumeifanya Serikali kuwa na limbikizo la deni lililofikia Sh 28, 743,586,356 hadi kufikia mwezi Desemba, 2015. Deni hili ni la nchi mbalimbali zinazotibu wagonjwa kutoka Tanzania.

Huu ni mradi mkubwa ambao bado unahitaji uwekezaji wa hali ya juu kwa lengo la kuhakikisha kituo kinakuwa ni kimbilio la wagonjwa wengi kutoka ndani na nje ya taifa letu.

 

Changamoto

Dk. Pallangyo anaeleza kuwa pamoja na mafanikio wanayoendelea kupata, taasisi bado inakabiliwa na chamgamoto mbalimbali zinazohitaji kutafutiwa ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu.

Anasema taasisi bado inakabiliwa na upungufu wa madaktari na wauguzi sehemu mbalimbali ndani ya taasisi hiyo.

Kwa mfano kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO daktari mmoja anatakiwa kuhudumia wagonjwa wapatao 4,000 hali ambayo ni tofauti kabisa na hapa kwetu 1:25,000.

Anasema kukabiliana na changamoto hiyo ya upungufu wa wataalamu ndani ya taasisi Serikali kupitia Wizara ya Afya imepeleka madaktari mafunzoni katika nchi mbalimbali kama Autralia, Marekani na Afrika Kusini.

“Lengo la jitihada hizi ni kukabiliana na upungufu wa wataalam uliopo ndani ya taasisi,” anasema Dk. Pallangyo.

Anasema changamoto nyingine ni pale anapotokea mgojwa mwenye matatizo ya kuwekewa kifaa tiba katika moyo kitwacho Pacemaker.

Anasema gharama ya kifaa hiki ni kikubwa kiasi kwamba mwananchi wa kawaida hawezi kumudu garama zake. Pacemaker moja inauzwa Dola za kimaremaki 7500 (Sh 16,500,000).

“Kwa Mtanzania wa kawaida hawezi kumudu gharama hizi, labda kwa wale waliojiunga na Bima ya Afya,” anasema Dk. Pallangyo.

Anamalizia kwa kusema kuna ongezeko la wagonjwa waliochangia kutokea upungufu mkubwa wa nafasi. Jitihada zinafanywa kujenga jengo la pili hususan kwa ajili ya watoto pembeni ya jengo hili.

 

 Je, unafahamu wagonjwa waliopata matibabu katika Taasisi hii ya Moyo ya Jakaya Kikwete na ikaokoa maisha yao? Usikose nakala ya Gazeti la JAMHURI ijayo.

By Jamhuri