Shirika la Kuboresha Mienendo na  Desturi kwa Ustawi (KUMIDEU) katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, linashirikiana na wadau mbalimbali kuandaa tamasha la Siku ya Mkerewe.

Kumideu inashirikiana na Haak Neel Production (T) Ltd ya Dar es Salaam na Idara ya Utamaduni na Michezo wilayani hapa, kuandaa tamasha hilo.

 

Mwenyekiti wa Kumideu, Makubi Paulinus, ameiambia JAMHURI mjini Nansio hivi karibuni, kuwa lengo la tamasha hilo ni kuikumbusha jamii ya Wakerewe umuhimu wa kuzithamini na kuzienzi mila, desturi na tamaduni zao.

 

“Tamasha hilo litaanza mwezi ujao [Juni] na litafikia kilele chake Julai, mwaka huu, katika uwanja wa Gertrude Mongela mjini Nansio. Tamasha hili linajikita katika tasnia ya sanaa za asili ya Mkerewe kama vile ngoma, kilimo, ufugaji, vyakula, zana za kale na mavazi ya asili ya Wakerewe.

 

“Kutakuwapo na mashindano mbalimbali yatakayohusisha vikundi tofauti katika ngazi za kata, tarafa na wilaya, ambapo waamuzi watakuwa wazee na walimu wa sanaa kutoka shule za Serikali wilayani hapa,” amesema Paulinus na kuongeza:

 

“Kupitia tamasha hilo, Wakerewe tutapata fursa ya kuonesha mila, desturi na mienendo mbalimbali kupitia ngoma za asili, ili hata jamii nyingine zielewe na kuthamini utamaduni wa Wakerewe.”

1526 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!