Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, anatuhumiwa kutoa zabuni ya uchapaji wa nyaraka za Serikali kwa Kampuni ya Yukos Enterprises Ltd ya mkoani Pwani bila kufuata taratibu.

Kampuni ya Yukos imepewa kazi ya kuchapa mitihani ya kidato cha pili, darasa la saba na fomu za shule ya msingi namba tisa (TSM 9) bila kutangazwa ambavyo vilikuwa zikichapwa na kampuni tofauti katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Uchunguzi iliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Sagini ametumia wadhifa wake kuwazuia makatibu tawala wa mikoa kuchapa nyaraka hizo muhimu nje kwa kivuli cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.

Sagini alitoa zabuni hiyo kwa Kampuni ya Yukos kwa mtindo wa zabuni ya chanzo pekee (Single Source) ambayo kwa mujibu wa sheria ya ununuzi ya mwaka 2004  malipo yake hayatakiwi kulipwa kwa zaidi ya Sh milioni 200 kwa kampuni itakayopewa zabuni.

Pia kampuni inayopata zabuni hiyo inatakiwa kufanya kazi katika mkoa au wilaya na si nchi nzima kama inavyofanya Kampuni ya Yukos.

Kampuni hiyo kwa mwaka jana ilipewa kazi ya kuchapa fomu za TSM9 kwa kuchapa fomu 868,030 ambazo kwa mwaka jana ziligharimu Sh 3,298,514,000.

Pia ilichapa mtihani  wa darasa la saba kwa idadi hiyo hiyo ya wanafunzi na kulipwa kiasi kama hicho cha fedha.

Uchunguzi huo umebaini kwamba kampuni hiyo ilipewa kazi ya kuchapa mitihani wa kidato cha pili 531,457  kwa malipo ya Sh 2,019,536,600.

Hivyo, kampuni hiyo kwa mwaka jana ililipwa Sh 8,616,564,600 kinyume na masharti ya zabuni iliyotolewa ambayo ilitakiwa kulipwa malipo yasiyozidi Sh milioni 200.

Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya wizara hiyo vimelieleza gazeti hili kwamba kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa kusuasua katika kipindi chote ilichopewa zabuni hiyo.

“Mwaka jana ilitulazimu kusogeza mbele mtihani ya kidato cha pili kutokana na kampuni hiyo kushindwa kuchapa mitihani hiyo kwa wakati,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimesema kwamba  hata baada ya kuongeza muda wa kuchapa mtihani huo, Katibu Mkuu huyo aliwataka maafisa elimu wa mikoa kwenda kufanya kazi ya kuchomekea mitihani hiyo. Kazi hiyo waliifanya kwa siku 14 na kulipwa posho kwa gharama Serikali ilhali kampuni hiyo ililipwa kiasi chote cha fedha na Serikali.

Hata hivyo, mtoa habari huyo alishangaa kuona baada ya Kampuni ya Yukos kupewa kazi hiyo, gharama ya uchapaji kwa fomu au mtihani mmoja  nazo zimepanda ghafla kutoka Sh 2,500 hadi Sh 3,800.

Awali utaratibu wa zabuni za uchapaji wa TSM 9 na mitihani hiyo ulikuwa ukitangazwa na katika mikoa, lakini baada Sagini kuingia katika wizara hiyo alibadilisha utaratibu huo bila kuwataarifu makatibu tawala wa mikoa.

Hata hivyo, kutokana na ubabe huo wa kufanya kazi bila kutoka taarifa, makatibu tawala wa mikoa waliendelea kutangaza zabuni kama kawaida, hali iliyowafanya wenye kampuni za uchapaji kupata hasara.

Kampuni zilizokuwa zikifanya kazi hiyo ni Kisomo Limited ya Mwanza, CNG Printing  (Musoma), Makiresol Investment na Fifo  Enterprise, zilizopo Arusha, Pride Com Limited, Nite ways Co Ltd, Printways, Fifo General Supplies  zote za Dar es Salaam.

Amesema kwamba mwaka  2011 – 2012  Katibu Mkuu, Sagini, alichukua hatua ya kuandika barua kwa makatibu tawala wa mikoa nchini yenye kumbukumbu Na CDA 134/322/01 ya Februari 2011 kusitisha utaratibu huo.

Sagini alitoa sababu za zuio hilo kuwa ni kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali ambao unatokana na uchapaji wa nyaraka muhimu nje ya udhibiti wa mpiga chapa wa Serikali.

Waraka huo uliendelea kutoa maelekezo kuwa pamoja na zuio hilo, ipo baadhi ya mikoa iliyokuwa ikiendelea kuchapa nyaraka hizo za Serikali nje ya udhibiti wa mpiga chapa mkuu.

Hata hivyo, uchunguzi ulifanywa na JAMHURI umebaini kuwa zuio hilo la barua hiyo ilikuwa ni ‘danganya toto’ kwani ilikuwa ni kuitaka kuidhinisha Kampuni ya Yukos kuchukua kazi hiyo.

Aprili 4, mwaka huu, Sagini aliandika waraka mwingine wenye kumbukumbu namba CAB.134/332/01/67 ulioelekeza kwamba Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali anatakiwa kushughulikia suala hilo.

“Kwa kuwa nyaraka hizo ni classified document na zinatakiwa kuandaliwa kuchapishwa hatimaye kusambazwa kwa usalama mkubwa na kwa kuwa mitambo ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali imekuwa na tatizo la uharibifu uliotokana na Electrical Fluctuation, hivyo Mpiga Chapa Mkuu ameshauri kazi hizo kwa mwaka huu wa fedha 2013-2014 zikamilishwe na Kampuni ya Yukos Enterprises,” ilieleza sehemu ya waraka huo.

Baada ya waraka huo makatibu tawala  wa mkoa kwa nyakati tofauti waliwashauri wenye kampuni zilizoshinda zabuni  kupitia katika mikoa kwenda kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kupata maelekezo zaidi juu ya uamuzi huo.

Amesema katika Ofisi ya Mpiga chapa Mkuu walikutana na Mkuu wa Masuala aliyejulikana kwa jina la Komba, lakini alipoulizwa kuhusu jambo hilo naye alishangaa kusikia umuzi huo na kuahidi kulifikisha kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, baada ya JAMHURI kutaka kujua suala hilo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo bali aulizwe Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.

“Naam simu yangu kakupa nani, OK hilo lisiwe taabu, siwezi kuzungumzia jambo hilo naomba mpigie Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali,” amesema Komba.

Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Yukos aliyejulikana kwa jina la Magoma alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai ya kuwa anayetakiwa kuulizwa ni yule aliyempa zabuni hiyo.

“Muulize huyo aliyetoa zabuni na hata kama alikosea hizi ni nyaraka za Serikali si za kuchezea, nasema usirudie tena kunipigia simu kwa heri,” amesema na kukata simu.

Hata hivyo, Mpiga Chapa Mkuu alipopigiwa  simu yake ilikuwa ikiita bila kuwa na majibu, na JAMHURI inaendelea kumtafuta.

Naye Katibu Mkuu TAMISEMI, Sagini,  simu yake iliita bila kuwa na majibu hata alipopelekewa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.

1711 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!