Dawa za kulevya zinazidi kuchafua jina la Tanzania. Zimekuwapo taarifa za orodha ya watu wanaotumia au kuuza dawa hizo hapa nchini, lakini kadri siku zinavyopita tatizo linazidi kuwa kubwa kwa kiwango cha kutisha. Katika hali isiyo ya kawaida, Mtanzania aliyeko kifungoni nchini China ameamua kuanika ukweli wa kinachoendelea Tanzania.

Kijana huyu ameamua kuandika barua na kuisambaza katika vyombo mbalimbali nchini, akitaja wahusika wauza dawa za kulevya kwa majina na biashara wanazofanya. Barua hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Jamiiforum ina taarifa za kutisha. Kijana huyu anataja majina ya wafanyabiashara wakubwa, na wabunge wanaofanya biashara hii.

 

Kuna watu wenye majengo makubwa hapa nchini, fedha nyingi lakini kumbe kazi yao kubwa ni kuuza dawa za kulevya. Kijana huyu anaeleza uozo uliopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam, ambapo wafanyakazi wa uwanja huu na moafisa Usalama waliopo katika uwanja huu ndio wenye kufanikisha michongo ya dawa za kulevya kupitishwa katika uwanja huu.

 

Itakumbukwa katika siku za karibuni kuwa wanamuzika kadhaa wa Tanzania wamekamatwa nchini Afrika Kusini au sehemu mbalimbali duniani, wakiwa na dawa za kulevya. Inaelezwa kuwa kuna Watanzania karibu 300 katika magereza ya China pekee wanaotumikia hadi kifungo cha maisha kwa kosa la kukutwa wakisafirisha dawa za kulevya.

 

Rais Jakaya Kikwete mara kadhaa amekuwa akisema kuwa anayo orodha ya watu wanaouza dawa za kulevya hapa nchini, na JAMHURI limeona ni vyema wananchi mkasoma wenyewe jinsi vijana wanavyoingizwa kwenye biashara ya dawa za kulevya kwa malipo kidogo na kuishia kupata mateso makubwa.

 

Magari yenye vioo vya tinted hapa nchini inaelezwa kuwa mengi yanasafirisha dawa za kulevya na silaha, hali inayoifanya Tanzania kutokuwa mahala salama pa kuishi. Kinachosikitisha ni kuona kuwa viongozi waliopewa jukumu la kulinda usalama kama uwanja wa ndege, ndio wamegeuka mawakala wa kufanikisha upitishaji wa dawa.

 

Kashifa hii inaanza kuharibu sifa ya Tanzania nje ya nchi. Mwanzo ilikuwa inaelezwa kuwa Tanzania ni njia tu ya kupitishia dawa hizi, lakini kisichoingia akilini ni kwamba zinaingiaje na kutoka katika nchi hii. Wachunguzi wa mambo wanasema tuhuma nzito kama hizi zenye kuharibu heshima ya nchi, enzi za Mwalimu Nyerere zingefanyiwa kazi haraka na kudhibitiwa.

 

Kinachohitajika sasa ni kusambatarisha watumishi wote wa Uwanja wa Ndege na kuweka watumishi wapya, na kama hiyo haitoshi, vyombo vya dola vinapaswa kufanya uchunguzi wa kina na kubaini wafanyakazi wanaohusika wakakamatwa na kufunguliwa mashiraka kisha wakaozea jela.

 

Maelezo ya kijana huyu ni yenye kusikitisha na kama viongozi wa taifa hili wana moyo wenye nyama, wasingewaacha wahusika wakitamba. Ingawa sisi hatukuweka majina yao gazetini, lakini wahusika, biashara wanazofanya, nyumba wanazomiliki, mahali walipo na majina yao yametajwa kwenye Jamiiforum. Ni matumaini ya JAMHURI kuwa vyombo vya dola vitakwenda Jamiiforum na kuchukua barua hii, kisha wahusika wakamatwe na kuhojiwa.

 

Barua kama hii ikiachwa ikapita hivi hivi, bila wahusika kukamatwa angalau kuhojiwa tu ikafahamika kwa Watanzania, tujue kuwa nchi hii itakuwa inajenga taifa la wabwia unga. Serikali inapaswa kuchunguza na kubaini kwa nini yaandikwe majina ya hawa waliotajwa na yasiandikwe ya watu wengine?

 

Inakera na kutia kinyaa kuona Tanzania nchi iliyokuwa na heshima kubwa kimataifa, leo imegeuka dangulo. Tanzania imegeuka taifa la mihadarati na wanaofanya hivyo wanaishi maisha ya raha ajabu. Tunaamini polisi wa Tanzania katika hili watauonyesha ulimwengu kuwa wanapambana na uovu ukiwamo huu wa dawa za kulevya. Isome barua hii uone maajabu.

999 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!