Taifa letu lipo katika mtikisiko mkubwa. Kuna mjadala mkubwa unaoendelea juu ya uanzishwaji wa kodi ya kumiliki simu. Kodi hii inatajwa na wengi kuwa ni kama kodi ya ‘Kichwa’ iliyobatizwa jina la kodi ya maendeleo baada ya Uhuru.

Hakika na zamu hii wanaiita kodi ya maendeleo kwa maana kwamba itasaidia kupeleka umeme vijijini. Kwa mtu yeyote mpenda maendeleo, hawezi kupinga kodi hii, isipokuwa kodi hii inapingwa kutokana na udhaifu wa Serikali katika kukusanya mapato.

 

Sitanii, leo ninavyoandika makala haya asilimia 90 ya biashara inayofanyika nchini ikiwamo madini na migodi hailipi kodi. Mimi niliasisi wazo la kila biashara kupewa namba ya mlipakodi mwaka 2003, bila kujali anauza kiasi gani.

 

Kwa bahati mbaya, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilichukua wazo langu nusu. Mwaka huu wanalenga wafanyabiashara 200,000 waingie kwenye mfumo wa kulipa kodi. Ni jambo, jema ila gharama ya kusimamia kazi hii ni kubwa.

 

Mimi naangalia nchi zilizoendelea na nakumbuka tukiwa pale Cassa Motel jijini Dar es Salaam, tulipata kujadiliana suala hili na Kamishna Mkuu wa TRA, Hary Kitillya, tukiwa wawili peke yetu. Atakumbuka kuwa tulijadili mfano wa Canada na kodi mwaka 2004.

 

Hapa nilikuwa napambana na mfumo wa kusajili magari kwa kutumia namba za mikoa. Mfumo huu ulikuwa unaruhusu wabadhirifu kusajili namba moja ya gari kwa mikoa zaidi ya sita. TRA walianza kwa kubisha, lakini siku nilipochapisha namba hizo waliniamini na matokeo yake mfumo wa namba za magari za kitaifa ukaanzishwa.

 

Sidai tuzo, ila nchi hii haina utamaduni wa kutambua mawazo ya watu na kukiri wazi kuwa wamechangia kuinua uchumi wa Taifa letu. Sawa na hilo la namba za magari, nilitoa wazo la kila biashara kulipa kodi.

 

Hapa nilimaanisha, iwe ni kwenye baa, Mama Ntilie, Machinga, dukani, kiwandani au kwenye ofisi ya huduma, kila malipo yanayofanyika yatolewe risiti ya elektroniki. Ulaya hata ukinunua sindano, unapewa risiti ya elektroniki.

 

Naunga mkono juhudi zinazofanywa na TRA, lakini kuweza kupanua wigo wa walipakodi, nasema mpango niliokuwa nikiupendekeza si kuweka kundi fulani ukaacha kundi jingine. Biashara zote zitoe risiti za elektroniki.

 

Sitanii, mfano ni kwamba mlipakodi anayepaswa kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) chini ya utaratibu mpya, ni yule anayefanya  biashara ya wastani wa Sh 40,000 kila siku kwa maana Sh 14,600,000 kwa mwaka.

 

Nilikwenda pale Kariakoo Mchikichini hivi karibu nilikonunua begi dogo la kuwekea mizigo ya mkononi ukiwa kwenye ndege. Begi hili niliuziwa Sh 80,000. Sikujua Machinga huyu, asubuhi hadi jioni alikuwa ameuza mabegi mangapi. Sikupewa risiti.

 

Sitaki kuamini kuwa Machinga huyu anauza begi moja kwa siku. Nilijaribu kumdodosa jirani yake, akasema chini sana kwa siku anauza mabegi 10 ikiwa hiyo ni siku mbaya. Maana yake, anapata kati ya Sh 800,000 na Sh 1,000,000. Hii ni sawa na Sh milioni 365 kwa mwaka. Halipi kodi. Mfanyakazi wa Sh 171,000 kwa mwezi anakamuliwa.

 

Nilisema na narudia, tunapanua wigo kwa kusema kila mmiliki wa biashara awe na mashine ya elektroniki na atoe risiti kwa kila mauzo anayofanya. Tukipata asilimia 40 ya biashara zote zinazofanyika hapa nchini, hakika tutakusanya kodi hadi tutashangaa.

 

Sitanii, ni uvivu wa kufikiri kuona kuwa njia rahisi ya kupata kodi ni kuanzisha kodi ya umiliki wa simu. Wanaomiliki simu ni makabwela. Wengi wanatumia 500 kwa mwezi na simu wanazo za kupokea misaada kutoka kwa ndugu zao.

 

Hofu yangu ni kuwa tukiruhusu kodi hii, tutakuwa tumerejesha kodi ya kichwa. Tuliifuta kodi hii mwaka 2003 na ilikuwa Sh 3,000 iliwashinda Watanzania. Leo tunaweka 1,000 kila mwezi, kwa maana ya 12,000 kwa mwaka. Haikubaliki.

 

Sitanii, mwelekeo ninaouona unaegemea zaidi katika wakubwa kutosumbua vichwa vyao. Si lazima kama Msumbiji wamefanya nasi tuige mkondo. Kwenye dhahabu, almasi, minofu ya samaki, mafuta na sehemu nyingine kodi nyingi mno zinakwepwa.

 

Kuna hii inayoitwa kodi ya majengo, kama leo kila mwenye nyumba angelipa Sh 50 kwa mwezi, na Serikali ikajipa jukumu la kuhakikisha kila nyumba iliyojengwa katika ardhi ya Tanzania inaongezewa thamani kwa kupatiwa hati, kila Mtanzania angejipeleka kulipa fedha hizo.

 

Yapo mambo yenye kushangaza. Inafika mahala unakuta watu wanawanyima Watanzania hati, ambazo zingewasaidia kuwekeza katika miradi mikubwa kwa kukopesheka, leo pale ardhi ni majanga. Hivi tumeishiwa fikira kwa kiwango hiki? Tumebweteka na kuona Watanzania wametajirika sasa tunataka tuvune utajiri wao? Tujipime.

Please follow and like us:
Pin Share