Tanzania kushiriki Reggae Ethiopia

Bendi ya muziki wa Reggae ya mjini Arusha ya ‘The Warriors From the East’ inarajia kushiriki katika tamasha maalum la Muziki wa Reggae, litakalofanyika nchini Ethiopia mwishoni mwa mwezi huu.

Tamasha hilo linalofahamika kwa jina la ‘Reggae in the Rift Valley Festival’ limekuwa likifanyika kila mwaka kwa kushirikisha makundi mbalimbali, yanayofanya muziki wa aina hiyo kutoka katika nchi mbalimbali duniani.

 

Kutokana na ushiriki huo, bendi hiyo ambayo maskani yake ni jijini Arusha (Geneva of Africa), tayari imeanza maandalizi kwa ajili ya safari hiyo ili kuhakikisha inafanya vizuri ili kupeperusha bendera ya Tanzania katika anga za muziki wa Reggae.

Msemaji wa bendi hiyo, Blackgzas Dadi, aliiambia JAMHURI hivi karibuni Dar es Salaam kuwa lengo lao ni kutaka kutangaza jina la Tanzania kupitia muziki wa Reggae.

 

Amesema kuwa hiyo itakuwa ni mara ya pili kushiriki katika tamasha hilo kubwa la muziki wa Reggae, ambalo amesema kuwa limewapa umaarufu kwa kiasi fulani tangu waliposhiriki mwaka jana.

 

“Hii ni mara ya pili kwa sisi kushiriki katika tamasha hili kubwa la kimataifa, mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka jana, na mwaka huu wametualika tena, kwa hiyo hii inatupa nguvu kwamba bendi yetu sasa inakubalika kimataifa,” amasema.

Bendi hiyo ya muziki wa Reggae imejipatia umaarufu zaidi hapa nchini Tanzania, baada ya kutwaa tuzo za Muziki za Kilimanjaro. Mwaka jana bendi hiyo ilitwaa tuzo ya bendi bora ya Muziki wa Reggae. Hali kadhalika, mwaka huu katika tuzo hizo bendi hiyo imetwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Muziki wa Reggae.

 

Blackgzas Dadi amesema kitu kingine kilichowapatia mafanikio ni kufanya muziki wa jukwaani, ambao amesema kuwa unapendwa na watu wengi na pia umekuwa ukionekana ndani na nje ya nchi kupitia vyombo vya habari.