Katikati ya Machi mwaka huu, nilikuwa nikisikiliza kipindi cha Sayansi na Ubunifu kupitia redio moja inayorusha matangazo yake kutoka Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho, mtangazaji alikuwa akimhoji mtu mmoja aliyefanya ugunduzi wa lami kwa kutumia mti wa mnyaa. Ugunduzi wa teknolojia hiyo ni wa kwanza duniani na kama huyu atasaidiwa, huenda Tanzania ikapata bahati ya kuweka lami barabara zote na kuuza teknolojia hiyo hadi nje.

Mtu huyu amegundua lami hiyo tangu mwaka 2009 lakini hadi leo hakuna kasi ya kuitumia fursa hiyo, ingawa alisema wataalamu wa Tume ya Sayansi wameshaanza kuifanyia utafiti na wamemuahidi kumtumia katika Tume.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kusikia habari za Watanzania kugundua mambo mbalimbali ya kisayansi; ila kilichonitafakarisha ni namna taifa linavyochangamkia fursa za ugunduzi unaofanywa na watu wake.

Tanzania ilikuwa ni nchi ya pili kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika baada ya Ethiopia, kuandaa sera mwanana kuhusu sayansi na teknolojia.

Sera hii iliundwa mwaka 1985 ikapitiwa upya mwaka 1995 na kisha kuchapishwa rasmi Aprili 1996. Malengo makubwa ya sera hiyo yalikuwa ni kuliwezesha taifa kujitegemea kupitia matumizi ya nyenzo za sayansi na teknolojia katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Sera hii inaainisha maeneo takribani 16 ya kupatiwa kipaumbele kwa matumizi ya sayansi na teknolojia. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kilimo, chakula na mifugo, viwanda, elimu na maendeleo ya rasilimali watu katika ngazi zote; kuwawezesha wanawake kutumia sayansi na teknolojia; urasmishaji wa sayansi na teknolojia pamoja na mawasiliano na uchukuzi.

Ikiwa ni takribani robo karne moja tangu kuundwa kwa sera hii nzuri, Tanzania bado inajikongoja katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hata baadhi ya nchi nyingine zilizounda sera za sayansi na teknolojia baada ya Tanzania, zimepiga hatua kadhaa ikilinganishwa na Tanzania.

Bado Tanzania haijafanikiwa kutumia sayansi na teknolojia ipasavyo katika kilimo ili kuzalisha chakula cha kutosha. Ndiyo maana bado tunakumbwa na majanga ya njaa karibu kila mwaka.

Maendeleo ya viwanda nayo yamekuwa ya kusuasua sana kiasi kwamba hadi sindano tunalazimika kuagiza kutoka nje! Kasi ya urasimishaji wa hii sayansi na teknolojia kwa wananchi umekuwa ni ndogo mno na kujikuta hadi leo ni asilimia chini ya 15 ya Watanzania ndiyo wanaotumia umeme!

Robo karne bado mawasiliano na uchukuzi hayana mfumo wa kisayansi na kiteknolojia, foleni za kukera mijini, barabara zisizopitika majira yote ya mwaka, mfumo wa reli licha ya kuwa ni wa kizamani lakini kuuendesha tu unatutoa jasho. Viwanja vingi vya ndege tulivyonavyo ni duni mno na unakosa hata ujasiri wa kuviita viwanja vya ndege.

Kasi ya kukua na kupanuka kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia inaambatana na mambo mengi, lakini kuna jambo kubwa moja ambalo ni msingi wa sayansi na ugunduzi wote duniani. Jambo hili ni ubunifu wa kina (serious creativity).

Ubunifu ni uwezo wa watu kuja na mambo mapya, kuyafanya yaliyokuwapo kuwa na namna nyingine ama kuongeza thamani kwa vitu ama mambo yaliyokwisha kuwapo.

Kuwa na sera nzuri katika nyanja ya sayansi na teknolojia ni suala moja, na kuitekeleza sera hiyo ni hatua ya pili ambayo ni ngumu zaidi. Na hapa ndipo taifa linapokuwa likikwama si tu kwa sera hii ya sayansi na teknolojia, lakini hata kwa sera nyingine zinazoshindikana ama zinazotekelezwa kwa kusuasua.

Taifa linatakiwa kufahamu kwa umakini vyanzo na haja ya ubunifu na kuchukua hatua za makusudi kuviendeleza na kuvisimamia. Ubunifu katika taifa hili unahitajika sana kutokana na sababu kuu mbili.

Mosi, tumekuwa na matatizo ya midororo ya kiukuaji ambayo kwa kutumia mbinu tulizozizoea tumeshindwa kujikwamua kwa miaka mingi – hapa tumaini pekee linalobakia ni ubunifu.

Pili; ingawa tunaweza kuwa hatuoni umuhimu wa ubunifu, lakini mawazo mapya ya kiugunduzi yanatoa fursa, faida na tija kwa maendeleo ya sekta ya sayansi na teknolojia.

Pengine suala la kulitazama ni namna gani tutawawezesha Watanzania kuwa wabunifu.

Suala hili linahusisha wadau wengi. Serikali kwa upande wake inapaswa kuwa na utashi wa kisiasa katika suala hili, Watanzania wenyewe lazima tuuone umuhimu wa kuwa wabunifu, watoto wanaozaliwa nao ni lazima waandaliwe mazingira yatakayowawezesha kuwa wabunifu.

Kama taifa tunapaswa kujiuliza, tunawaandaaje wananchi wenye vipaji kuwezesha mawazo yao kuwa na tija? Shule zetu (msingi, sekondari, vyuo na taasisi) zina mifumo gani yakinifu inayozalisha ubunifu, ugunduzi na uvumbuzi wa kisayansi?

Kuna sumu tumejitengenezea katika mifumo yetu ya elimu. Sumu hii ni ‘kufaulu mitihani’. Kuanzia elimu ya chini hadi ya juu msisitizo unawekwa kwa watoto kufaulu ‘maswali yanayoitwa mitihani’.

Mifumo ya elimu na utamaduni wetu wa kimakuzi hautoi nafasi kwa mtu (hasa watoto) kujaribu, kukosea ama kukisia ili kubuni, kuvumbua na kugundua. Tumejifanya ‘ma mr. super smarts’ kila kitu tunataka kiende kama ilivyozoeleka. Hatupendi kubeba gharama za makosa ya kujaribu, ambayo huzaa ugunduzi.

Tumesahau kuwa ukiwa unafanya mambo yale yale kila siku, utabaki kuwa yule yule kila siku! Hatujui kabisa kuwa ukipita njia wanayopita wengi utafika walipo wengi! Tunahitaji kuwa tofauti, tunahitaji namna mpya za kufanya mambo ya kiubunifu katika nyanja hii ya sayansi na teknolojia kupitia ubunifu.

Kuna maeneo mengi ambayo ni chanzo cha ubunifu (sources of creativity) ikiwamo kuhamasisha (motivation), uzoefu wa kiutendaji (working experience), kukisia (innocence), makosa (mistakes), nasibu (chance), ajali (accident) na uendawazimu wa sayansi ya majaribio bila kujali vikwazo vya kimazingira (creative madness).

Taifa linatakiwa kuwatazama kwa umakini sana na kuwaendeleza watu wenye uwezo wa kuja na mawazo mapya ya kiubunifu kupitia njia hizi.

Kuna mifano mingi duniani inayojumuisha umuhimu wa mawazo mapya yaliyokuja ama kwa bahati mbaya, kwa nasibu, kwa makosa kwa ajali ama kwa uzembe au vinginevyo. Mvumbuzi wa kihistoria Columbus aliweza kuvumbua nchi mpya ambayo ni Marekani ya sasa, kutokana na makosa ya matumizi ya vipimo vya baharini.

Badala ya kutumia vipimo vya Eratostlienes akajikuta anatumia vipimo vya Ptolemy (bila kujua kama amekosea), na bila kutarajia akajikuta analifikia bara America ingawa kufika huko kulitokana na ajali aliyoipata baharini!

Kukisia ni ule uwezo wa mtu kujaribu vitu vipya ambavyo havijapata kutokea, huku akiwa hana uhakika wa nini hasa kitakuwa. Kule nchini Ufaransa, kuna ndugu waliojulikana kama Montgolfer Brothers. Hawa walifanikisha kurusha puto linalotumia hewa joto angani (first hot air balloon).

Taarifa hizi za kusisimua zikamfikia mfalme ambaye kwa haraka haraka aliona jambo hili linaweza kuwa na fursa nzuri kwa maendeleo ya kijeshi. Mfalme akamuita ofisa mkuu wa masuala ya sayansi, M. Charles, na kumwamuru atengeneze puto kama alilolisikia.

Mwanasayansi huyu alipata wakati mgumu sana, na kujikuta akijiuliza swali kuu moja, “Wamefanyaje wale?” Jibu alilojipa ni hili: “Huenda wametumia gesi ya hydrojeni ambayo ni nyepesi kuliko hewa ya angani ndiyo maana puto lao limeruka”.

Charles akavumbua puto bora duniani linalotumia gesi ya hydrojeni (hydrogenic balloon), ambalo ni tofauti kabisa na lile la Montgolfer Brothers. Hydrogenic balloon sasa linatumika kama chombo cha masafa mafupi angani kwa shughuli za burudani, chenye uwezo wa kupakia watu!

Hapa viongozi wetu wanatakiwa kujipa changamoto kuhusu nia, uwezo na utamaduni wao, wa kuwabaini Watanzania wenye vipaji tofauti katika ubunifu.

Jingine ni uwezo wa viongozi wetu kubaini fursa zinazokuwapo ndani ya mawazo ya kiugunduzi, wakati wanapofikiwa na taarifa za kiugunduzi.

Ili tupige hatua katika sayansi na teknolojia, kuna umuhimu wa viongozi wetu kuiga mfano kama ule wa Ufaransa na ugunduzi wa puto. Viongozi muda wote wanahitajika kuwa na hamasa ya kuwaongoza wananchi, hasa hasa waliopo katika mifumo ya kielimu na kiutendaji kuwa wabunifu.

Tuonane wiki ijayo
stepwiseexpert@gmail.com 0719 127 901

2013 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!