Sasa tusichezee tena madaktari

Ulimwengu wa mtandao ni kitu kizuri sana. Watu wanawasiliana kwa masafa marefu katika muda mfupi kabisa. Wazungu walikuwa wanasema nasi tukawa tunashangaa, lakini nasi tunaitikia leo kiukweli kweli, kwamba dunia imekuwa kijiji.

Aina ya kijiji kinachozungumzwa si kwa udogo wa kijiografia, isipokuwa kufikika haraka kama kwenye kibapa cha mkono. Hii ina uzuri na ubaya wake.

Ubaya ni kwamba mambo hasi yaani yasiyokuwa mazuri ndiyo habari kubwa. Wanahabari huyachangamkia haraka na jamii huyakimbilia kuyasoma, kusikiliza na kutazama.

Kwa hiyo, hata madaktari walipogoma hapo nyumbani, tulifuatilia kwa karibu na kulia pamoja na waliokuwa wakilia na kuhuzunika na waliokuwa wakifanya hivyo.

Somo moja tulilopata na ambalo labda linatakiwa libaki daima akilini mwetu kwa muda wote tutakaojaaliwa kuwa hapa duniani, ni umuhimu wa madaktari. Sisemi hivyo kwa vile nami napata heshima ya kuwa kwenye klabu hiyo, hata kama sistahili, lakini nasema haya kwa sababu wameitikisa nchi yetu pendwa.

Dunia ya sasa inaokoteza na kusambaza magonjwa ya kila aina, na kama si wataalamu wetu hawa – kuanzia madaktari wa kawaida na wale bingwa, shuka chini hadi wasaidizi wao wote – kweli kifo tutakiona umbali wa kurusha jiwe.

Sitaki kuwakumbusha machungu hayo, japokuwa najua wengi wanatembea nayo kwenye sakafu ya vifua vyao na katika mitima yao, kwa sababu bado mambo hayajaisha na sijui kama yataisha kwa furaha ya wadau wote.

Tatizo kubwa hapa ni jinsi madaktari wasivyothaminiwa nchini mwetu – iwe ni kwa sababu ya udhaifu wa waliotengeneza mfumo wetu wa utumishi na mafao au kwa sababu ya wanasiasa wanaovutia maslahi yote kwao, zikiwamo posho. Kwa hiyo, kiliponuka juzi, kama watoto wa mjini ninavyowasikia wakisema, kila mtu akaanza kuuliza kulikoni.

Wagonjwa waliendelea kugumia maumivu, wengine ikabidi waiage dunia na wengine kuzidiwa na maumivu yao, hadi madaktari walipotulizana baada ya kukutana na mkuu wan chi. Waliyozungumza na kuafikiana sitajadili hapa, lakini neno moja lizingatiwe kwamba lazima umuhimu wa madaktari uzingatiwe.

Umuhimu huo usipozingatiwa, matokeo yake huwa ni kama tuliyoona na tunayoendelea kuona; madaktari wameikimbia nchi yao na kuwaacha wagonjwa wao.

Kusema kweli wanashindwa kumudu mahitaji yao muhimu na kuishi maisha ya hadhi yao, jambo ambalo ni muhimu. Hata wakija wanasiasa na kuhubiri eti udaktari, unesi na uuguzi ni wito. Je, watakula huo wito na kuutumia kwenye mahitaji yao yote?

Hatuwatendei haki na kwa hiyo wapo walioamua kuitafuta haki – na utafutaji huo umegawanyika. Wengine wamefungua maduka ya dawa baridi, wengine wameanzisha zahanati na hospitali zao, wengine wanaomba na kupokea hongo, wengine wanadunga watu ‘sindano za maji’ na wengine wamekimbilia kwenye nchi zinazowajali.

Uongo mbaya, moja ya nchi zinazotoa kipaumbele kwa watu hawa, wawe wageni au wazalendo ni Uingereza. Nesi ni mtu mkubwa sana hapa, lakini hapo kwetu ndiye anaonekana kama kinyamkera fulani hivi cha kuchoma sindano na kubeba ‘kinyesi’ cha wagonjwa.

Nesi wa Ulaya ukimsikia mwogope kabisa. Kaa pembeni maana atakukanyaga na mgari wake mkubwa! Daktari acha kabisa, na wapo madaktari kutoka hapo nyumbani na maeneo yanayotuzunguka wanakula bata kama hawana akili nzuri.

Na hili limezua mjadala tayari kwa wadaku na mapaparazi wa hapa, waliohoji wingi wa madaktari hao wa ‘Kiswahili’, ikilinganishwa na mahitaji ya huduma yao hapo nyumbani.

Mfano ukatolewa katika eneo dogo tu kati ya mengi ya Ulaya, mashabiki hasimu wa timu mbili ‘vidume’ zilizopo hapo sijui watakuwa na lipi la kusema. Ni Manchester. Sasa katika jiji hilo, inasemekana kuna madaktari wengi zaidi wa kutoka Nyasa kuliko ilivyo kwa Malawi nzima.

Hili linawakilisha mambo yetu sote hapo nyumbani. Madaktari wamekimbia kutoka Malawi na kujazana Manchester hadi wakawazidi walio nchini mwao! Wangekimbilia nini Ulaya kama mambo yangekuwa mazuri Unyasani na Bongo? Wangebaki wayafurahie maisha na ndugu zao, lakini wamefunga safari ndefu kwa ajili ya ‘kuokota’ mipauni.

Haya si madai ya kuokoteza njiani, yametolewa na watu wengi wenye heshima zao, ikiwa ni pamoja na waandishi wa tafiti za kimataifa kuhusu wafanyakazi wa sekta ya afya.

Waafrika wengi wananufaika na fursa za kazi kwenye sekta ya afya. Hata wenye ujuzi mdogo tu wanaheshimiwa, wanapewa nafasi ya kuanza kazi kama wanafunzi na katika muda mfupi tu wa wiki kadhaa hadi miezi na miaka, wanakuwa wafanyakazi kamili kwa ngazi tofauti, wakiendelea na mafunzo ya mara kwa mara na kupandishwa ngazi. Huo ndiyo uzuri wa Uingereza.

Kinyozi anafika anasema anataka awe msaidizi kwenye huduma ya afya, anachunguzwa uwezo wake wa kuelewa, anapewa makabrasha, anapewa mtu wa kuwa naye kwa muda, analipwa pesa ya kueleweka na baada ya muda kama ana wito kweli, anaula. Kama hana wito anagundulika na kuondolewa kwa upole.

Sasa kwa rafiki zangu wanaofanya kazi kwa mazoea hapo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na taasisi zinazojitegemea zinazosimamia afya, watakuwekea ukiritimba wa ajabu. Kwamba hadi uwe na digrii sijui ngapi, lakini baada ya hapo uwe na uzoefu. Sasa huo uzoefu utaupata wapi bila kuanza kazi? Na wa kutoa uzoefu ni wao hao hao.

Wanaposema hadi wawe na uzoefu ndiyo maana madokta walio hapa Uingereza waliokimbilia huku, kabla hawajafikia cheo hicho na sasa wakirudi hawalipiki tena, kwa sababu noti wanayotaka ndefu na sisi kama kawaida tunasema hali ni mbaya, nchi yetu changa, uchumi haujatengamaa. Halahala, ukizubaa wakuta mwana si wako. Alamsiki!