Tanzania tunao wajibu wa kuziokoa Rwanda, Uganda

Fukuto la kutokea mfarakano na hata umwagaji damu linaendelea kati ya Uganda na Rwanda. Lakini pia kuna msuguano mkubwa wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Burundi.

Mataifa haya matatu ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hii ina maana kwamba jambo lolote baya katika mataifa hayo lina athari kwa nchi wanachama, hasa Tanzania.

Tanzania ni mwathirika mkuu kwa sababu tunapakana na mataifa yote hayo matatu. Hii ina maana kwamba vurugu za aina yoyote kwenye mataifa hayo zitasababisha wimbi la wakimbizi watakaokuja nchini mwetu, pia zitaathiri biashara katika Bandari yetu ya Dar es Salaam.

Sote tunatambua athari za wakimbizi nchini mwetu. Ongezeko la uhalifu na uharibifu wa mazingira ni miongoni mwa athari hizo.

Ni kwa sababu hizo na nyingine za kiutu, tunatoa mwito kwa serikali yetu kuchukua nafasi yake muhimu katika ukanda huu kuhakikisha inafanya kila linalowezekana ili kuepusha shari yoyote inayoweza kutokea.

Wiki iliyopita Rais Paul Kagame wa Rwanda alifika nchini kwa ziara ya siku mbili. Bila shaka rais huyo na mwenyeji wake, Rais John Magufuli, walipata wasaa wa kuzungumzia vuguvugu linaloendelea baina ya mataifa hayo.

Kwa miaka mingi nafasi ya Tanzania kwenye masuala haya ya usuluhishi imejulikana na kuthaminiwa. Ndiyo maana tangu zama za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hadi leo Tanzania imekuwa na imeendelea kuwa kimbilio la wote waliohitaji suluhu.

Tunaomba Serikali ya Awamu ya Tano iendelee kuhakikisha Tanzania inabeba jukumu halali na la kibinadamu la kuhakikisha migongano inayohatarisha umoja na usalama miongoni mwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inamalizwa mapema na kwa mafanikio.

Pia viongozi wa mataifa haya watambue kuwa zama hizi ni nzuri kuhamishia nguvu nyingi katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na maisha ya wananchi. Huu si muda wa kuanza kuwaza kununua silaha za kujihami.

Viongozi wetu wahakikishe kuwa umoja miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki unaendelea, kwa sababu umoja huu ni wa wananchi, si wa viongozi. Endapo vurugu zitatokea, watakaoumia ni wananchi, na kamwe si viongozi au watawala.

Tunatoa mwito kwa serikali yetu kutokaa kimya pindi kunapoanza kuonekana dalili za moshi wa mfarakano miongoni mwa mataifa, hasa yale yanayotuzunguka. Hatima ya Afrika tunayo sisi Waafrika wenyewe.