Watu wengi wametia mikono yao magazetini kuandika habari za vurugu zilizoendelea kutokea Mtwara kuhusu suala la gesi.

Wananchi wa Mtwara wanaonekana hawataki gesi ipelekwe mahali pengine bila wao kujua faida watakayopata.

 

Katika suala hili la Gesi ya Mtwara, baadhi ya watu huwaangalia wananchi wa Mtwara kama watu wakorofi tu wasiotakiwa kusikilizwa.

 

Lakini kuna baadhi ya watu wanaotaka wananchi wa Mtwara wasikilizwe kwa umakini. Mmojawao anayetaka watu wa Mtwara kusilizwa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana.

 

Sina sababu ya kuficha kitu, namvulia kofia Kinana. Siku nyingi alipotaka Serikali iwasikilize wananchi wa Mtwara.

 

Kinana anajua fika kwamba wananchi kwa ujumla wao wameuchoka utawala wa CCM kutokana na kuiendesha nchi kibabe. Hali hiyo imesababisha mikoa ya Kusini kuamua kuondokana na CCM wakati Kusini ilikuwa ngome ya kuaminika ya CCM.

 

Katika kutambua hilo Kinana amepiga kelele zinazotaka wananchi wa Mtwara wasikilizwe na Serikali, lakini nani anajali? Hakika sikio la kufa halisikii dawa. Kama tujuavyo Serikali ya Tanzania ni Serikali ya wananchi, jukumu la kwanza la Serikali yoyote ya wananchi ni kutimiza matakwa ya wananchi.

 

Tufike mahali Serikali ya wananchi inajitofautisha kabisa na Serikali ya Mwingereza aliyekuwa akifanya chochote anachotaka huku akidai kuwa “Serikali ya Malkia haikosei”.

 

Vurugu zilizoendelea kutokea Mtwara, nionavyo mimi, ni matokeo ya ubabe wa Serikali. Badala ya kuona ukweli wa mambo Serikali inaweza ikadai kuwa wapinzani wanawachochea wananchi wa Mtwara kufanya vurugu, kumbe vurugu hizo zinachochewa na ubabe wa Serikali, nami kwa kuwa sikuja gazetini kuleta uzushi nithibitisha ulipo ubabe wa Serikali.

 

La kwanza kabisa, mkataba wa gesi haupo wazi kwa wananchi wa Kusini.  Swali linakuja; kama suala la Gesi ya Mtwara si la mtu binafsi ni suala la umma, kwanini Serikali haitaki kuwaonesha viongozi wa Kusini wakiwamo wabunge mkataba huo? Je, Serikali haijui kwamba uchochezi hupewa nafasi ya kufanya kazi pale panapokosekana uwazi?

 

Tazama! Pamoja na Tanzania kuwa na mazingira mazuri ya uwekaji, imepata alama ya chini katika utawala wa sheria, hali inayowataka na kuwapo kwa vitendo vya rushwa katika mikataba mbalimbali na kukosekana kwa uwajibikaji.

 

Tazama! Mwaka 2010 Sheria ya Madini ilifanyiwa marekebisho na mrabaha ukaongezeka. Lakini bado mikataba ya kampuni za madini imeendelea kuwa siri. Ni kwa maslahi ya taifa?

 

Tazama! Mwaka 2012 Tanzania ilitia saini mpango wa uwazi katika shughuli za madini. Huo uwazi uko wapi wakati mikataba ya madini inafichwa na Serikali?

 

Tunataka kusema kweli na ni la lazima tuseme kweli wabunge wa Kusini wameachwa njia panda. Kwa kuwa hawaujui mkataba wa gesi wamekaa kimya wameshindwa kuutetea mkataba ambao hawaujui. Lakini pia wanashindwa kuunga mkono madai ya wananchi wanaowawakilisha bungeni.

 

Ni katika mazingira hayo Mbunge wa Mtwara, Hassein Murji, ameamua kusimama upande wa wananchi wake.

 

Serikali inawona Murji kama mchochezi lakini mbele ya wananchi Murji ni mtetezi na shujaa, kwa hiyo kitendo cha Serikali kumdhalilisha Murji kwa kumweka mahabusu, kimempandisha chati na kuchochea uhasama kati ya wananchi wa Mtwara na wabunge wanaoendelea kukaa kimya. Wanaonekana ni wa saliti.

 

Ubabe mwingine wa Serikali ni huu. Wananchi wa Mtwara walimkataa siku nyingi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, lakini kutokana na kuendesha nchi kibabe Serikali haioni kama wananchi wana haki ya kumtaka mkuu wa Mkoa.

 

Na wakati huo huo kwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Mtwara anajua kuwa wananchi hawamtaki, hapana shaka anaendesha Serikali kibabe. Hali hiyo haiwezi kusaidia kuleta amani, uhasama unaendelea kuwapo Mtwara kati ya mkuu wa mkoa na wananchi kwa ridhaa ya Serikali, unaendelea kuchochea vurugu.

 

Si kweli kwamba akihamishwa mkuu huyo wa mkoa wananchi wataendelea kumkataa kila mkuu wa mkoa watakayeletewa. Kwani tangu tupate Uhuru wamewakataa wakuu wa wangapi wa mikoa huo? Lakini pia ni kweli wananchi wataweza kumkataa mkuu wa mkoa mwenye tabia zinazofanana na mkuu wa sasa wa mkoa.

 

Ubabe mwingine wa Serikali kule Mtwara ni huu. Maeneo mengine ya nchi hii wananchi wanapofanya vurugu Serikali huwakamata watu wanaokutwa eneo la vurugu, lakini kule Mtwara baada ya kutuliza vurugu, polisi waliingia kila nyumba kusaka wananchi wasio na hatia na kupora mali zao. Wengine waliwachomea nyumba. Kama huu si uonevu wa wazi kwa wananchi wa Kusini serikali ituambie ni kitu gani!

 

Kwa kila hali ubabe wa Serikali hautafanikiwa kuleta hali ya amani na utulivu wa kweli Mtwara. Kinachotakiwa hapa ni Serikali kuuleta mkataba wa gesi Mtwara mbele ya wabunge na viongozi wa siasa badala ya kuwakamata na kuwafungulia mashitaka mahakamani kwa uchochezi. Uchochezi ni matokeo ya kuwaficha wananchi mambo wanayotakiwa wajue. Nani anabisha?

By Jamhuri