Lakini udhaifu wa wazee wa nchi hii kwamba hatuna Chama cha Wazee wa Taifa hili. Napenda kutoa mawazo yangu juu ya upungufu huu wa aibu katika Taifa kongwe kama Tanzania.

 

Mataifa yaliyopata uhuru nyuma yetu –  majirani wetu Kenya na Uganda – wana vyama vya wazee vya kitaifa na wameshatutangulia kulipa pensheni kwa wazee wa nchi zao. Nini kimetukwamisha sisi? Ni domo kaya letu! Tunaweza sana kuzungumza, kubuni mambo kinadharia, lakini tukifika kwenye utekelezaji Watanzania tunatoka kapa! Hatuwezi kitu!

 

Sasa huu ni wakati mwafaka kwetu wazee wa Tanzania kuwa na Chama kimoja cha Taifa cha Wazee wa nchi hii. Tujitambue na tujenge utamaduni wa kukubali kuwa na SAUTI MOJA ya WAZEE WOTE wa Taifa hili.

 

Najaribu kutoa historia ya wazee wa nchi hii tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipong’atuka mwaka 1985. Wazee tukajitambua nchi hii kuna ombwe la uongozi wa wazee kitaifa. Ombwe lile ndilo linalotuchelewesha kuwa na SAUTI MOJA YA KITAIFA YA SISI WAZEE.

 

Upo usemi wa kale kuwa uzee ni dhahabu (old is gold). Kwa nchi za Dunia ya Kwanza zile za Magharibi, usemi huo unaeleweka vizuri sana na wazee wanathaminiwa kweli. Hapa Tanzania, sina uhakika na hilo ila ninajua wazi kuwa Baba wa Taifa aliwathamini sana wazee na aliwasikiliza.

 

Kabla hajafanya jambo kubwa kwa Taifa aliwashirikisha wazee hasa wa Dar es Salaam. Alikuwa na mazoea ya kulitangazia Taifa jambo muhimu kupitia kwa wazee wa Mkoa (Jiji) wa Dar es Salaam.

 

Ninatoa mifano michache kuonesha Mwalimu alivyothamini wazee hawa. Je, tunakumbuka ule mkutano wake pale Diamond Jubilee  wa Novemba 4, 1985 wakati anang’atuka madarakani? Mimi nilikuwapo na kama sikosei aliongea namna hii “…Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam na wazee wa Tanganyika nzima. Nimeanza nao mapema sana, mapema kweli….Mwaka 1954. Wazee wakaniamini upesi sana”.

 

Maneno haya alitukumbusha sisi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa enzi za harakati za kuunda chama cha TANU mwaka 1954 katika kutafuta Uhuru wa Taifa hili alikuwa na wazee.

 

Si wazee wa hapa Dar es Salaam tu, bali alitukumbusha hata alivyopokewa na wazee wa Songea na wazee wa Mbeya mwaka 1955.

 

Simulizi zile za Mwalimu wakati anawaaga wazee wa Dar es Salaam zililenga sana kuwashukuru kwa namna walivyomwamini kijana wao, na walivyomsaidia katika zile harakati zake za kuunda chama cha kumkomboa Mtanganyika kutoka mikononi mwa mkoloni Mwingereza. Alitaka Taifa litambue umuhimu wa WAZEE na liwaheshimu na kuwaenzi ipasavyo.

 

Sote tunajua historia ya TANU kuwa ilianzishwa zaidi na vijana wenye umri wa kati ya miaka 30 na 35 hivi. Mwalimu mwenyewe alikuwa na umri wa miaka 32 tu. Mzee mashuhuri aliyemkaribisha Mwalimu katika chama cha TAA alikuwa Abdul Walid Kleisk Sykes ambaye alikuwa na umri wa miaka 30 mwaka huo wa 1954.

 

Mdogo wake Ally Kleist Sykes na mwenziwe Dossa Aziz walikuwa na umri wa miaka 28 hivi. Kumbe vijana hawa wenye nguvu na dhamira safi ya kujitolea kuanzisha chama cha siasa ndiyo wazee wetu waasisi wa Uhuru wa nchi hii.

 

Enzi zile wazee waliotambulika walikuwa kina Mzee John Rupia au Mzee Rajabu Diwani, na wengine. Hao walikuwa na umri uliozidi miaka 55! Wengine wote kama akina Jafet Kirilo walikuwa na umri wa miaka 36 mwaka ule wa 1954 na Oscar Kambona alikuwa na umri wa miaka 28 tu. Ndiyo kusema vijana walichemka na wakagangamala kukijenga chama. Hapakuwa na haja ya tawi la wazee, maana wale wazee wachache walikubalika kimapokeo hapa mjini Dar es Salaam.

 

Lakini Mwalimu katika mkutano ule wa kutuaga akijiandaa kung’atuka, alitumia muda kupiga stori kuonesha wazee walivyomsaidia na walivyomwezesha hapa Dar es Salaam.

Alitoa na ile hadithi yake ya kutambikiwa kule kwa Jumbe Tambaza usiku wa manane. Labda nikumbushie alivyotuhadithia yeye Mwalimu pale Diamond siku ile.

 

Alisimulia hivi, namnukuu; “Siku moja Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam) na kusema leo wazee wanakutaka.” Mwalimu aliuliza, “Wapi?” Dosa akajibu, kwa Jumbe Tambaza, wanakutaka usiku! Mwalimu aliendelea kutueleza. Nikasema ‘haya nitakuja’.”

 

Basi, akaenda kweli na kukuta wazee wameshakaa eti wamemwita kijana wao wamwombee dua. Sasa Mwalimu katika simulizi yake akatwambia, “Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani kwa Qur’an. Ile kumbe ilikuwa dua la kwanza tu. Kulikuwapo na dua la pili usiku ule.” Hapo Mwalimu alieleza huku akitabasamu. Wakamwambia ipo dua pia ya wazee wetu.

 

Wakatoka nje ya ile nyumba ya Mzee Tambaza wakamsimamisha mahali karibu na beberu ambapo mimi leo nasema kwa mantiki ya makabila ya Wabantu. “Wakamtambikia”. Maana wale wazee walimchinja yule beberu huku wakitamka “Twining umekwisha!” Damu yake beberu yule ikatiririkia katika shimo lililokwishaandaliwa na akaambiwa aliruke lile shimo yaani “atambuke”.

 

Akasema alitambuka, yaani aliruka shimo lile. Sasa Mwalimu ni msimulizi mzuri sana (kwa Kiingereza wanasema sarcastical) yaani ana lugha ya vijembe au kejeli hivi. Akatwambia, jamani mimi ni Mkristo hao (wazee) Waislamu na mimi mkorofi korofi katika mambo haya (ya kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee hao.

 

Mwishoni alituchekesha kwa ile hadithi yake ya yaliyompata Bagamoyo kwa Sheikh Mohamed Ramia, Mwezi Mtukufu wa Ramadhani miaka ile. Alisema walifikia nyumbani kwa huyo Mzee Sheikh Ramia wakafanya mkutano wao wa TANU. Mwalimu akajisikia kichwa kinamuuma sana mchana ule. Akamuliza, “Sheikh una Aspro?” Sheikh naye akamuuliza Mwalimu, “Kwanini unataka Aspro?” Mwalimu akajibu, “Kichwa kinaniuma kweli kweli.” Sheikh akajibu, “Subiri”.

 

Baada ya mkutano jioni watu wametulia jua limeshazama, swala imekwishasaliwa, basi kukawa muda wa kufuturu pale kwa Sheikh Mohamed Ramia. Mwalimu akisimulia huku anacheka kweli, alisema,“Tulifuturu vizuri. Mzee Ramia akaniuliza ‘bado unataka Aspro?” Mwalimu kiutani utani akatuambia, “Nikajibu kichwa sasa hakiumi” akamalizia kutuchekesha – KUMBE ILIKUWA NJAA!”

 

Kwa kumaliza hiyo stori yake akafunga kwa kusema, namnukuu; “Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa SHUKRANI KWA WAZEE NA IMANI YAO KWA VIJANA WAKATI HUO.”


Itaendelea

 

By Jamhuri