Mwanasiasa mkongwe nchini, Njelu Kasaka, amezungumza na JAMHURI na kueleza alivyopokea rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Marekebisho ya Katiba. Kasaka alikuwa kiongozi la wabunge 55 mwaka 1993 lililojulikana kama G55 likishiriki kudai Serikali ya Tanganyika. Yafuatayo ni mahojiano kati ya Kasaka na JAMHURI. Endelea…

JAMHURI: Umeipokeaje rasimu ya Katiba iliyotangazwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba June 3, mwaka huu?

NJELU KASAKA: Nawapongeza Tume ya Katiba kwa kutengeneza rasimu ya Katiba ambayo ni nzuri. Imezungukia mambo mengi tu. Nikisema nzuri si perfect (timilifu) bado kuna mambo ya kurekebisha. Nimefurahi kwamba suala la Serikali tatu katika Muungano wa Tanzania, hatimaye limekuja. Kwa zamu hii limekuja na mwelekeo mzuri, kuwa zamu hii linaweza kupita.

 

Tulilizungumza hadi mwaka 1993, sisi tulikuwa tunakwenda Zanzibar kwa passport ikiwa ni miaka 29 baada ya Muungano tunakwenda kwa passport Zanzibar. Sikupenda wazo kuwa kulikuwapo na Rais wa Zanzibar na Rais wa Muungano. Hili niliona halikubaliki, nikapigana likaondoshwa.

 

JAMHURI: Kwani tatizo la msingi lilikuwa nini?

NJELU KASAKA: Tatizo lilitokana na kutokuwapo mpaka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Serikali ya Muungano ilikuwa ndiyo inaokana kama mbia wa Zanzibar kwamba level (ngazi) yao ni moja, wakati Serikali ya Mungano haikuwa ngazi moja na ya Zanzibar bali inalingana na Serikali ya Tanganyika.

 

Zanzibar walikuwa wanaona Serikali inayotawala Muungano ni Serikali ya Tanganyika na kwamba ilikuwa inawadanganya. Niliwahi kwenda Zanzibar wanazungumzia ya Muungano wanaiita Serikali ya Tanzania Bara.

 

JAMHURI: Mwaka 1993 mlifanya uamuzi gani baada ya kuona hilo?

NJELU KASAKA: Sisi tuliona tupeleke hoja bungeni, ipatikane Serikali ya Tanganyika ambayo ingekuwa equivalent (sawa) na ya Zanzibar. Tuliandaa hoja, ikakubaliwa bungeni wabunge wakaiunga mkono, ila baadaye Mwalimu Julius Nyerere hakuipenda, akatafuta hoja tu ya kuiondoa. Tuliishakutana naye mara kadhaa, tukampa hoja zetu, alikuwa hawezi kuzipinga tunavyoongea. Na pia alikuwa anaheshimu sana Bunge kwa sababu kuwa hawezi kutumia mabavu kuzuia Bunge kujadili.

 

Bunge lilipopitisha akatafuta njia ya kulizima kwa kusema hiyo si Sera ya CCM. Akasema wabunge hawakutumwa na chama chao. Viongozi walikuwa wameanza utekelezaji. Baadaye waliitisha mkutano Dodoma Novemba 1993 akazungumzia hilo suala kuwa lisitekelezwe, lipelekwe kwa wanachama wa CCM kupata mawazo yao iwapo wanalikubali au la. Kama likikataliwa basi. Ikabidi liahirishwe hilo suala ikatengenezwa hoja, likapelekwa. Lakini unaifahamu mikutano ya CCM inavyokuwa.

 

Wanaopelekewa ni wanachama, wasiotaka ni viongozi wao, sasa unatarajia nini? Matokeo yake wakalikataa. Baada ya hapo CCM wakarudi na kusema chama kimekataa hivyo Bunge lisingeweza kutekeleza sera hiyo.

 

Katika nchi za demokrasia, Bunge likiishapitisha wanatekeleza, lakini katika nchi kama yetu na katika nchi za kikomunisti vyama vilikuwa na nguvu kuliko Bunge. Bunge wakati ule lilikuwa Kamati Maalum ya Chama. Wabunge wale wa G55 tuliendelea kutetea azimio letu hadi wakati wanalifuta.

 

JAMHURI: Unaweza kuwakumbuka baadhi ya wabunge mliokuwa nao kwenye G55?

NJELU KASAKA: Nawakumbuka hadi leo. Tulikuwa na akina Sebastian Rukiza Kinyondo, Said Nakua (marehemu), William Mpiluka (marehemu), Guntram Itatiro (marehemu), Jenerali Ulimwangu, Phillip Marmo, Charles Kagonji, Ismail Ivata, Alipiki Kasyupa, Ombel Mwamfupe, Polile Ombee, Maria Kham, Tabitha Siwale, Edith Mnuo, Pascal Degera, Evarist Mwanansao (marehemu), Pascal Mabiti (Mkuu wa Mkoa wa Simiyu) na wengine wengi tu.

 

JAMHURI: Ukiuangalia Muungano baada ya hoja ya G55 uliimarika zaidi au ulidhoofika?

NJELU KASAKA: Muungano haujakaa na kutulia. Umekuwa unakwenda lakini kibaya zaidi Zanzibar wakawa wanazidi kujivuta nje ya Muungano hatua kwa hatua. Wakawa wanasema, wanataka tupate bendera wanapewa, wimbo wa taifa, vitu vya pamoja wanajaribu kuvikwepa kwa mfano michezo mashindano ya Muungano yakavunjika hawayataki, Mamlaka ya Mapato Tanzania nao wanaunda ya kwao.

 

Ilivyofika mwaka 2010 wakarekebisha Katiba yao, wakaenda mbele zaidi wakatangaza mipaka ya nchi yao, Rais wakataka awe na hadhi sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vitu ambavyo vimekuwa vikitokea na watu wanavitazama tu.

 

Sasa ilipoundwa Tume ya Kurekebisha Katiba nimeshukuru kwamba imefanya hivyo. Nimefurahi kwamba hili suala limekubaliwa. Hili suala watu wasipingane  nalo. Kwa sababu huu muundo wa Serikali wa sasa kwa mazingira ambayo yametengenezwa na Zanzibar, huu muundo hautekelezeki tena. Hatuwezi kuwa na marais wawili wenye ngazi moja kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.

 

Tuna nchi moja inayotawaliwa na marais wawili wenye nguvu zinazolingana? Niliishaandika kuwa haiwezekani. Tumeruhusu, wanasema bila woga kuwa sawa hatutaki Muungano. Wanaanza ku-dictate mambo katika Muungano. Imefika mahali hautekelezeki tena.

 

JAMHURI: Unalizungumziaje wazo la Serikali tatu?

NJELU KASAKA: Wazo la Serikali tatu naliunga mkono 100 kwa 100. Watanzania walikubali. Wanaopinga, waelewe tulipofika tuna njia nne tu. Njia ya kwanza ni kuwa na Muungano wa Serikali moja, ambayo Serikali ya Zanzibar waliishakataa na wanaendelea kukataa.

 

Ya pili ni Serikali mbili ambayo haitekelezeki, njia ya tatu ni ya serikali tatu na njia ya nne ni kuvunja Muungano. Serikali moja hapa, mbili haitekelezeki, umebakiwa na kuvunja au Serikali tatu. The most convenient (isiyo na usumbufu) ni serikali tatu.

 

Wasioutaka Muungano wanasema itakuwaje nchi moja iwe na marais watatu. Wanashangaa nini kama tumekuwa na marais wawili katika nchi moja kwa miaka 50? Haiwezekani nchi moja ikawa na marais wawili, hakuna sababu ya kuanza kushtuka sasa. Cha ajabu nini kuwa na marais watatu?

 

Urusi ya nyuma na ya sasa ilikuwa ni Union of Soviet Socialist Republics (USSR), kulikuwa na marais wengi. Kiongozi wao wakawa wakati mwingine wanamwita Katibu Mkuu, baada ya Soviet kuvunjika kukabaki Soviet Republic, mpaka 2010 wamebadili Katiba yao, Rais atakuwa ni wa Soviet Federation na wengine watakuwa magavana.

 

Muundo unatengenezwa na sisi wenyewe. Bahati mbaya wanaolalamika ni viongozi. Unatarajia mtu atoke Chunya, atoke Tunduru aje kutengeneza muundo wa Muungano hapa? Viongozi wakubaliane wategeneze.

 

Canada walianza majimbo manne, leo kuna majimbo 10 yanayounda Shirikisho. Mimi anapolalamika kiongozi simwelewi. Mkiwa na Serikali tatu shirikisho si rahisi kuvunjika. Shirikisho linashikiliwa na vitu viwili – hiyari na nguvu.

 

Kuna nchi nyingine waliingizwa kwa nguvu kama Ujerumani na Marekani. Kuna nchi nyingi ziliingizwa kwa nguvu. Demokrasia imesambaa katika dunia nzima hiyari ndiyo msingi wa nguvu za Muungano wowote, inahitaji political maneuvers. Tuko Serikali mbili Zanzibar wanazungumzia kujitoa. Seif Shariff Hamad anasema wanataka madaraka kamili. Kina Jussa wanazungumza kujitoa. Hii ni nini? Mbona haidhibitiwi?

 

JAMHURI: Wanaokataa Serikali tatu wanatumia hoja ya gharama. Je, unalizungumziaje hili?

NJELU KASAKA: Suala la gharama halipo. Mimi sikubaliani na wanaosema kutakuwapo gharama. Ndani ya Serikali ya Muungano kuna wizara sita za Muungano. Waliobakia mawaziri wote ni za Tanganyika. Kwa sasa tunawalipa. Unaposema tutenganishe tuwaone, hapo tunasema kuna gharama. Tukisema Watanganyika wakae huku na wabara wakae huku kelele zinapigwa.

 

Inasemwa kutakuwapo bureaucracy (urasimu), Watanzania wengi hawajui kwamba Zanzibar haijawahi kuchangia Muungano. Gharama zote zinabebwa na Tanganyika. Mwaka juzi walitumia umeme hadi ikafikia Sh bilioni 50 bila kulipa, ikabidi Serikali ya Tanganyika ndiyo ifute hilo deni, ikabidi iliipe Tanesco. Haya yote kwa sababu hayawekwi wazi watu wanafikiri kuna gharama kubwa.

 

Unapotenganisha hizi bureaucracy, ni matukio ambayo si mageni katika ulimwangu huu. Nchi nyingi tu ambazo zina muundo wa Shirikisho haya mambo wanayo. Ukichukua kwa mfano Canada, inajitawala yenyewe lakini pia ni sehemu ya Uingereza, wanaye Gavana ndiye anayemwakilisha Malkia. Wana magavana, wanaochaguliwa na wananchi, yale majimbo yana mamlaka ya ndani, lakini pia nayo yana mwakilishi wa Malkia – Lieutenant Governor (majimbo).

 

Huwezi kusema utaendesha nchi bila gharama, njia rahisi ilikuwa ni Serikali moja. Katika dunia ya sasa tunapenda katika local level watu wajiendeshee mambo yao. Mambo ya elimu, kilimo wajiendeshee wenyewe, lakini masuala ya kimataifa hapana. Mimi naunga mkono Muungano uwepo, katika muundo huu wa Serikali tatu na ndiyo maana nawaambia Wazanzibari ni vyema wakajitambua hiyo.

 

JAMHURI: Je, suala la ardhi unalizungumziaje?

NJELU KASAKA: Ardhi ndiyo msingi mkubwa wa Muungano. Symbolically waliunganisha udongo. Watapata wapi fursa ya ku-sort out (kutenganisha) ule udongo uliounganishwa. Najiuliza viongozi hawa wakati Zanzibar inachukua hatua moja baada ya nyingine kujiondoa kidogo kidogo kwa nini walikuwa hawasemi? Mwaka 2010 ikarekebisha Katiba na ilikuwa inapinga Serikali ya Muungano isipanue mipaka ya bahari kwa madai kuwa ni eneo lao.

 

Watanganyika tunapenda kujidanganya. Mnakiona kitu kinaharibika mnasema kizuri tu, mpaka kitakapooza. Hawa wanajitoa kidogo kidogo tunawaacha, tunasubiri mpaka waseme kwaheri? Watatuacha kwenye chaos (mkanganyiko). Zanzibar wameunda uamsho, Nassor Moyo anaongoza Kamati ya Maridhiano, hakuna anayetoa sauti kusema wanachofanya ni batili.

 

JAMHURI: Unadhani mapendekezo ya rasimu ya sasa yako sawa?

NJELU KASAKA: Serikali ya Muungano kuna baadhi ya mambo ambayo imeyaacha lakini kimsingi yalitakiwa yawe kwenye Muungano. Maliasili, huwezi kuachia yote mambo ya gesi, petroli, uran yangeendelea kushughulikiwa na Serikali ya Muungano.

 

Marekani kuna wizara ya kilimo ya kitaifa, lakini kila jimbo lina Wizara yake ya Kilimo. Kuweka viwango vya mazao ni suala la Muungano, ku-control ni suala la Muungano. Huwezi ukasema kila jimbo au kila mwanachama atakuwa na sheria zake za disease control, mazingira, ardhi ilistahili kuwa suala la Muungano kwa nia ya kuhakikisha kwamba nchi inabaki kuwa moja.

 

Kungekuwa na maeneo yanayosimamiwa na Muungano mambo mengine ya kugawa viwanja wangeachiwa nchi za Tanganyika na Zanzibar.

 

Matumizi ya ardhi kwa mfano – Serikali ya Muungano ikitaka kujenga jambo lolote itabidi iende kuomba Zanzibar au iende kuomba Tanganyika. Kwa mfano, kama sasa hivi tuna matatizo ya ugomvi kati ya wafugaji na wakulima, ilitakiwa kuwe na chombo cha kitaifa ambacho kinasimamia ardhi kwa nchi nzima.

 

Uhusiano wa kimataifa naona ndilo litabaki kuwa jukumu la Serikali ya Muungano. Itaishia kwenye mambo ya nchi za nje, itabaki kupokea wageni, kupeleka mabalozi, mambo yote ya biashara yapo kwenye ushirikiano wa kimataifa kama World Trade Organisation itabidi iwe inakwenda Tanganyika na Tanzania, mahusiano kati ya nchi na nchi. Tukifika mahala Zanzibar ifanye la kwake na Tanganyika ifanye la kwake tumekwisha. Tutaichanganya dunia, haya yangekuwa mambo ya Muungano, ila ndani mnaweka utaratibu wenu.

 

Kwa mafano, Marekani Gavana wa Jimbo anatembelea nchi yoyote duniani, lakini anakwenda na Bendera ya Marekani haendi na bendera ya jimbo lake nje ya nchi. Ushirikiano wa kimataifa unapaswa kuwa wa kitaifa.

 

Leo Rais Barrack Obama anakuja na watu 700, anaokuja nao  hawatoki Washington wote. Wengine California, Texas, Minnesota, New York, lakini sisi tunataka kwenda kama Zanzibar na Tanganyika. Nasema hapana, tuwe Tanzania. Muungano ni mzuri, lakini tusipotekeleza mambo ya msingi utatushinda.

 

JAMHURI: Ikiwa mwaka 1993 CCM waliteka mchakato wa G55, hudhani hata rasimu hii CCM wanaweza kuiteka wakasema zinatakiwa Serikali mbili?

NJELU KASAKA: Tunapaswa kufahamu kuwa tunatengeneza Katiba ya Tanzania. Hatutengenezi Katiba ya kikundi chochote. Tunaangalia miaka 100 mbele. Katiba isifungwe na maslahi ya makundi, tuangalie kama taifa tutaingiaje kwenye mchakato huu.

 

Matumaini ya Zanzibar kurudisha ardhi kwenye Muungano ni madogo, ila inawezekana watu wanaopiga kelele ni kikundi kidogo, ingewezekana tuwape wananchi fursa ya kuulizwa. Unaweza kukuta wananchi wanapenda iwe hivyo wakapingana na mawazo ya kikundi cha wachache.

 

JAMHURI: Je, unadhani chini ya mfumo unaopendekezwa, kuna haja ya kuendelea kuwa na wakuu wa mikoa na wilaya?

NJELU KASAKA: Kuwa na Mamlaka karibu na watu ni vizuri zaidi, lakini kikubwa zaidi uwezo wa kifedha. Kama mnakuwa na Serikali kama hii lakini wakatoa mamlaka makubwa kwa local government (serikali za mitaa) na kukawa na usimamizi mzuri, financial discipline (nidhamu ya fedha), nidhamu matumizi ikawa makubwa, mambo yatakwenda.

 

Si kwamba nchi hii haina hela, mimi hilo siliafiki sana. Ni kwa sababu hela tunazozipata zinatumika visivyo. Hata nchi zilizoendelea wanalalamika kuwa bajeti zao ni ndogo, lakini wanahakikisha hicho kidogo walichonacho kinakwenda kwenye maendeleo ya nchi. Hawamruhusu mtu mmoja kwenda kujinufaisha.

 

JAMHURI: Umeichukuliaje hatua ya kufutwa kwa Takukuru kwenye rasimu?

NJELU KASAKA: Hakuwezi kuwapo maadili kama hakuna chombo kama Takukuru, chombo cha kudhibtii rushwa, haiwezekani. Binadamu kwa asili yake ni wabinafsi, wanataka ashibe kwanza kabla ya jirani. Zinawekwa sheria kwa ajili ya kudhibiti ubinafsi wa mtu mmoja mmoja na sisi kama kweli tunalenga kuleta maendeleo, kwanza lazima iwepo nidhamu ya viongozi wa watendaji.

 

Takukuru iwepo, tena ipewe na uwezo zaidi, wa kuwashughulikia wale wanaoonekana wana matatizo  kwa kuwapeleka mahakamani.

 

Wamesema Takukuru wamewekwa polisi. Polisi ni kitu kingine kabisa na chombo cha kupambana na rushwa ni kitu kingine. Lazima kiwepo kwenye ngazi ya Jamhuri na kwenye Serikali za Tanganyika na Zanzibar na ndipo utaleta nidhamu kwenye maadili na uongozi.

 

Najua kwa sababu ya ubinafsi kuna watu wanapinga chombo hiki, wanaona maslahi yao hayako salama kwa Takukuru kuendelea kuwapo. Pia nchi kuiweka pamoja itategemea nani mnamchagua kuwa Rais wa Jamhuri, lazima awe na uwezo wa kuiweka nchi pamoja. Hata mkiwa na Katiba nzuri kama hii itasambaratika. Kuiweka nchi pamoja awe na ujasiri wa kuwaambia wenzake hiki hapana, hiki ndiyo.

 

Nchi wanachama wanaounda Shirikisho anapaswa awe na uwezo wa kuwaambia hili hapana, hili ndiyo. Yaainishwe yapi wanaweza kufanya, na yapi hawawezi kufanya kwenye Katiba. Si kusema ambayo hayajatajwa, yawepo makatazo. Katiba iseme wazi kuwa nchi shirika hawawezi kufanya haya.

 

Katiba za nchi washirika haziwezi kuwa open ended (bila ukomo). Huwezi mtu leo kusema mimi napitisha sheria najitoa, kuwapo vitu vinavyotamkwa kuwa hiki na hakiruhusiwi.

 

JAMHURI: Je, huko kurejea kwa Tanganyika kutachochea ubaguzi, ukabila na majimbo?

NJELU KASAKA: Tukiwa wadhaifu kwenye Serikali ya Muungano mambo mengi yatajitokeza. Kwenye uongozi ukiwa imara hayatajitokeza. Viongozi watende haki. Kama wanakuwa wakweli sioni namna gani watu wengine wanaweza kwenda nje ya utaratibu. Wawe wakweli wanachokisema kiwe ndicho wanachokitenda.

 

JAMHURI: Je, ni kipi kingine kilichokufurahisha katika Katiba hii?

NJELU KASAKA: Nimefurahia wabunge kutokuwa mawaziri. Kwa sababu  sasa watafanya kazi ya ubunge. Watawawakilisha wananchi wao na wataisimamia serikali. Suala la wananchi kumwondoa mbunge kabla ya muda wake sikubaliani nalo. Kuna hujuma, kuna watu wanaweza kujenga hoja chafu kwa kutumia hela kiasi mpaka yule mbunge aliyepo akachukiwa. Tukiruhusu hilo tutaleta vurugu watu wenye hela watahonga watu na unaweza ukawaudhi wenye fedha wakakuadhibu kama mbunge.

 

Ujue mbunge anapambana na matajiri wanaopora ardhi ya wananchi, ukiwapinga watakufanyia mbinu wakuhujumu. Hili ni hatari sana. Ila wabunge wasipokuwa mawaziri hawatakuwa na tamaa ya kupeleka maendeleo majimboni kwao.

 

Hata hivyo, suala la wabunge wawili katika Jimbo sijalielewa. Wamelichukulia kuwa wanawake na wanaume wawe sawa kwa sawa, najiuliza faida zake sijaziona, ingawa sipingani na suala la wanawake kuwa katika mambo ya uongozi. Lakini kwamba lazima waje na wabunge wenye muundo wa wabunge wawili wawili silielewi.

 

Kwenye Katiba ya Tanganyika si lazima kufuata kila kitu cha Muungano. Si lazima kufuata neno kwa neno mambo ya Muungano, ilmradi isivunje sheria. Kwa mfano sheria za ardhi nchini Marekani jimbo hadi jimbo ni tofauti, lakini kila Mmarekani ana haki ya kumiliki ardhi katika Jimbo lolote.

 

JAMHURI: Yapo mawazo kuwa Katiba ya Tanganyika itumie maoni yale yale yaliyochukuliwa wakati wa kuandika Katiba ya Tanzania. Unalizungumziaje?

NJELU KASAKA: Itabidi tupate maoni ya upande wa Watanganyika, iwapo wanataka hao hao walioongoza Tume ya Katiba ya Muungano ndiyo waendelee kuandika na ya Tanganyika au waongezwe na watu wengine, na mimi ningefikiri wale waliopo waendelee ila waongezewe na watu wachache, ionekane ni Kamati nyingine imetengeneza Katiba ya Tanganyika.

 

JAMHURI: Je, unakubaliana na Tanganyika kuitwa Tanzania Bara?

NJELU KASAKA: Nchi zilizoungana ni Tanganyika na Zanzibar. Zinapobadili utaratibu wa Muungano wao, mnayoitoa pale ni Tanganyika tu. Tanzania Bara haikuwapo. Jina hili limetumbukizwa hapa katikati hapa. Hata mimi sijui kikao gani kilichopitisha jina Tanzania Bara, sijawahi kuona. Nchi ninayoijua ni Tanganyika. Tunazungumzia juu ya Zanzibar na Tanganyika hatuundi Tanzania Bara.

 

Wengine wamekuwa wakiona aibu kusema Tanganyika. Jana (wiki iliyopita) kulikuwa na kipindi cha watoto. TBC wanatembelea watoto, wanauliza mtoto anasema Tanzania ilipata Uhuru mwaka 1961, wanampotosha mtoto.

 

Tanzania ilipatikana mwaka 1964, huku nyuma ilikuwa ni Tanganyika. Wanaogopa kutamka neno Tanganyika iliyokuwapo mwaka 1961, ni Tanganyika hiyo sherehe ya tarehe 9 Desemba tunasherekea Uhuru wa Tanganyika, na Aprili 26, tunasherehekea Muungano wa Tanzania wa mwaka 1964. Mbona hatupotoshi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar tunasema wazi kuwa ni Januari 12, 1964?

 

JAMHURI: Suala la kodi kimsingi rasimu inaliondoa kwenye Muungano na kuiachia Serikali ya Muungano ushuru tu, hili limekaaje?

NJELU KASAKA: Serikali ya Muungano lazima iwe na uwezo wa kutoza kodi ili ijiendeshe kwa kodi zake yenyewe. Isitegemee kuchangiwa, iwe na vyanzo vya kutosha tu, ili ikiwa na hela nyingi nchi wanachama ikipata matatizo iwe na uwezo wa kwenda kusaidia.

Haiwezi kuwa Serikali ya Muungano, watu wamepata maafa isiweze kusaidia.

 

Tanganyika wamepata maafa au Zanzibar isiwe ni Serikali ya kutazama tu. Kuwepo kodi za Serikali ya Muungano vinginevyo ukisema wanachama wachangie Serikali ya Muungano haitadumu hata kwa miezi miwii. Inapaswa kugharamia mtumizi yake yenyewe na kutoa misaada kwa nchi wanachama.

 

JAMHURI: Najua leo umesema unajikita katika kuchambua rasimu ya Katiba. Je, unaweza kuzungumzia japo kwa ufupi, maisha yako ya kisiasa?

NJELU KASAKA: Nimekuwa mbunge wa Jimbo la Chunya kwa miaka mitano, baadaye tukaligawa likawa Lupa na Songwe, nikagombea Lupa nikawa mbunge kwa miaka 10 hadi 2005. Mwaka 2005 kura za maoni hazikutosha nikatoka CCM (akaenda CUF ila baadaye akarejea CCM). Nimepata kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Ushirika, nimekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa na Tabora na kabla sijaingia kwenye siasa nilikuwa mfanyakazi wa CRDB. Kwa sasa nipo nyumbani najitafutia maisha yangu mwenyewe.

 

JAMHURI: Mwisho, umepata kuwa mwanachama wa CCM, ukahamia CUF baadaye ukarejea CCM. Ndani ya CCM wenzako wanakuangaliaje?

NJELU KASAKA: Wanavyoniangalia. Ni wenzangu.

By Jamhuri