Tumbo la mtu mzima lina urefu wa takriban inchi 10 (sentimeta 25) na linaweza kutanuka kwa urahisi kiasi cha kubeba robo lita ya (chakula). Chakula hukaa katika tumbo kwa karibu saa nne.

Kuta za tumbo hutoa maji tumboni yanayojulikana kama gastric juice. Kuta hizo ni misuli inayotanuka na kusinyaa ili kukichanganya chakula kwa majitumbo, ambayo sehemu yake husaga protini.

 

Chakula kinapowasili, kunyanzi za tumbo huanza kuzalisha asidi ili kuvunjavunja chakula na kukifanya kiwe rahisi kusagika. Asidi ina nguvu sana na kama ingekuwa peke yake bila kuwapo tabaka la mnyunyizo uliogandamana unaoitwa ute telezi (mucus), ambao huzifunika kunyanzi kuilinda kutokana na asidi, basi ingeweza kulimong’onyoa tumbo lote.

 

Utumbo mdogo

Utumbo mdogo ni mwembamba, mrefu; una urefu wa futi 22 hadi 25 (meta 6.7 hadi 7.6) na ni tyubu/mrija uliyojiviringisha. Ugiligili (fluid) kutoka tumboni, kwa pole pole huingia katika utumbo mwembamba kwa mafungu madogo madogo. Na usagaji wa chakula huendelea kufanyika katika utumbo mdogo.

 

Ini na kongosho huingiza ndani mnyunyizo wao. Nyongo kutoka katika ini huanza kuyafanyia kazi mafuta (fats) wakati maji ya kongosho (pancreatic juice) kutoka kwenye kongosho husaga sehemu ya protini na wanga ambayo haikusagwa.

 

Kuta za tumbo pia hutoa maji (juice) ambayo husaidia kukamilisha usagaji wa wanga, protini, na mafuta. Chakula kilichosagwa hufyonzwa kwenye damu; na damu hukipeleka kwenye sehemu zote za mwili.

 

Utumbo mpana

Chakula kilichobaki ambacho hakikusagwa na pia hakikufyonzwa, huingia katika utumbo mpana kwa pole pole na kwa mafungu madogo madogo. Utumbo mpana ni mfupi zaidi na ni mpana zaidi kuliko utumbo mdogo.

 

Utumbo mpana hufyonza sehemu kubwa ya maji na kuyapeleka katika damu. Mabaki magumu ambayo hubaki bila ya kusagwa huunda kinyesi (faeces). Kinyesi huhifadhiwa kwa muda katika rektamu na kisha kutolewa kupitia utupu wa nyuma (anus).

 

Ufyonzaji hufanyika mara tu chakula kinapoyeyuka ndani ya maji. Kwa hiyo ni muhimu sana kunywa maji mengi kila siku.

 

Ugonjwa wa vidonda vya tumbo ambao hujulikana kitaalamu kama “Peptic Ulcer Disease” (PUD) ni kidonda ambacho kwa kawaida hukaa katika eneo la mfuko wa chakula (tumbo) au sehemu ya awali ya utumbo mdogo (duodeni) au umio na kuleta maumivu kwa mgonjwa. Kwa tafsiri rahisi ni shimo au mmomonyoko katika kunyanzi za tumbo, duodeni, au umio.

 

Majina maalum yanayopewa vidonda vya tumbo hutambulisha makazi ya vidonda hivyo au hali zilizosababisha.

 

Kidonda cha tumbo kinapodhuru tumbo, kidonda hicho huitwa kidonda cha tumbo (gastric ulcer); kinapodhuru sehemu ya awali ya utumbo mdogo inayojulikana kama duodeni kinaitwa kidonda cha duodeni (duodenal ulcer), na kinapodhuru umio kinaitwa kidonda cha umio (esophogeal ulcer).

 

Vidonda ambavyo huweza kutokea sehemu ya tumbo inapokuwa imeondolewa kwa upasuaji huitwa Marginal ulcers. Na vinapotokea kutokana na msongo mkali wa ugonjwa huitwa Stress ulcers.

 

Ukubwa wa kidonda cha tumbo kinaweza kutofautiana kuanzia inchi moja ya nane (1/8) hadi robo tatu (3/4) ya inchi. Kama utaweza kuona ndani kabisa ya matumbo yako, kidonda cha tumbo huonekana kama ‘volcano’ nyekundu iliyo ndani ya kunyanzi za matumbo.

 

Vidonda vya duodeni

Duodeni (duodenum) ni sehemu ya mwanzo ya utumbo mdogo. Baada ya chakula kuchanganyika na asidi ya tumbo, huingia ndani ya duodeni, mahali ambapo huchanganyika na nyongo inayotoka ndani ya kibofunyongo na maji ya mmeng’enyo yanayotoka ndani ya kongosho. Ufyonzaji wa vitamini, madini na virutubisho vingine huanzia ndani ya duodeni.

 

Mara nyingi vidonda vya tumbo hutokeza katika duodeni, sehemu ya mwanzo ya utumbo mdogo. Vidonda hivi ambavyo huwapata watu wengi hasa wanaume; hutokea inchi chache za kwanza za duodeni.

 

Vidonda vya tumbo

Tumbo (stomach) ni kiungo cha mmeng’enyo wa chakula. Tumbo lina umbo kama mfuko na liko kati ya umio na utumbo mdogo. Takriban kila mnyama ana tumbo.

 

Tumbo hukaa upande wa kushoto wa uwazi au uvungu wa fumbatio.  Neno ‘tumbo’ humaanisha ‘tangi la chakula.’ Ndani yake kuna gesi au hewa, kuta za pailori (Vali baina ya tumbo na duodeni), viunganishi vya umio, sehemu ya awali ya duodeni, n.k.

 

Tumbo lina asidi sana ambayo pamoja na vimenge’enya, husaidia kuvunjavunja molekuli kubwa za chakula kuwa ndogo zaidi, kiasi kwamba chakula muhimu kinaweza kufyonzwa na kusagwa.

 

Vidonda vinavyokaa katika mfuko wa chakula au tumbo (gastric ulcers) ambavyo haviwapati watu wengi, mara nyingi hutokea kwenye mpindo wa juu wa tumbo, kidonda hiki kina tabia ya kuwapata wanaume na wanawake.

 

Itaendelea

Please follow and like us:
Pin Share