pg 12Kampuni ya Bia Tanzania (TBL Group) inayomiliki kampuni za Tanzania Distillers Limited (TDL), Tanzania Breweries Limited (TBL) na Darbrew Limited, yenye ubia na Kampuni ya SABmiller ya Afrika Kusini, inatumia udhaifu wa sheria nchini kukwepa kodi, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini.

Uchunguzi unaonyesha kuwa bidhaa za TBL (ikiwao Konyagi) zinazouzwa nje ya nchi zimeandaliwa mpango wa kushushwa bei, hivyo Serikali kuishia kupata kodi kidogo ikilinganishwa na bei ya soko ya awali.

Uamuzi huu umefikiwa baada ya uongozi wa juu wa TBL kuushinikiza uliokuwa uongozi wa TDL, chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, David Mgwassa ukiuke taratibu za kibiashara kwa kubuni mbinu za ‘kuficha’ sehemu ya faida inayotokana na mauzo ya Konyagi nchini Kenya. Konyagi ilishapaa hadi kuingizia TBL wastani wa dola milioni 16 za Marekani (Sh bilioni 35) kwa mwaka.

Kiasi hiki kilitokana na mauzo yaliyokuwa yamepanda na kufika wastani wa kontena 15 kwa mwezi, ambazo zilikuwa zinauzwa kupitia Kampuni ya Kapari Limited.

Baadaye TBL ilibadilisha masharti ya mkataba kwa Kampuni ya Kapari Limited ya Kenya na ikapunguziwa eneo la kusambaza kinywaji hicho kutoka nchi nzima ya Kenya hadi eneo la Nairobi pekee; hali iliyovuruga biashara zao. Kontena moja linachukua katoni 1,500 za Konyagi.

“Tulianza kuona tatizo mwaka 2013 Mkurungenzi alipokuja akamwambia bosi [Mgwassa] wetu kuwa mafanikio yaliyopatikana yasitangazwe yote, bali kiasi kingine kiwekwe akiba,” anasema mtoa habari wetu akilieleza JAMHURI kuwa maneno haya aliambiwa Mgwassa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TDL kabla ya mkataba wake kukatishwa katika mazingira yenye utata.

Taarifa zinaonyesha kuwa Mgwassa hakukubaliana na uongozi wa juu wa TBL kutaka faida inayotokana na mauzo ya Konyagi nchini Kenya isitangazwe yote, badala yake watangaze kiasi kidogo; na akahoji fedha zinazopatikana angezitoleaje hesabu au zingetumiwaje bila kuonyesha vyanzo na matumizi yake katika mizania ya hesabu.

“Uongozi wa juu ulimhakikishia Mgwassa kuwa asiwe na wasiwasi kwani fedha zinazopatikana zinaweza kupunguzwa kwa kuingizwa kwenye ununuzi kama wa sukari [ikaongezwa bei kuliko bei ya soko] na bidhaa nyingine zinazotumiwa na kiwanda hicho kuzalisha bia… Mgwassa alipohoji hilo inawezekanaje, Mkuguenzi huyo raia wa Afrika Kusini akamwambia, ‘Usiwe na wasiwasi, nitajua la kufanya’,” kinasema chanzo chetu.

Baada ya kauli hiyo, pale TDL yalianza mabadiliko ya ghafla ambako aliyekuwa Mhasibu Mkuu, Mustafa Nassoro aliondolewa na akapalekwa mwingine anayeitwa Justine.

Anthony Grendon, akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Crown Beverage ya Kenya, mwaka 2013 alifika Tanzania na kumwamuru Mgwassa awanyang’anye biashara Kapari Limited, kisha wapewe Crown Beverage, ambayo ni kampuni tanzu ya SABmiller.

Mgwassa hakutekeleza maagizo hayo, kwani yeye alikuwa anaripoti kwa Robin Goetzche, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TBL wakati huo. Grendon kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mtendaji wa Accra Brewery Limited ya nchini Ghana.

“Harakati zote hizi, zilitokana na Wazungu kutoka Afrika Kusini kuona kuwa TDL kupata faida ya dola milioni 16 wanapoteza fursa ya wao kupata chochote nje ya utaratibu halali,” kinasema chanzo chetu na kuongeza kuwa ilipofika Desemba, 2014 Robin aliondolewa kwani naye alionekana hatekelezi mpango wa ‘kuficha mapato’ kwa usahihi.

Desemba, mwaka 2014 aliletwa Mkurugenzi Mtendaji mwingine TBL, Roberto Jarrin aliyemwita Mgwassa ofisini na kumwagiza abadili wakala wa Kenya kutoka Kapari Limited, kwenda Crown Beverage bila kujali mkataba wa kibiashara uliopo. Baada ya agizo hilo, Jarrin akaandika barua pepe kwa Mgwassa akimtaka aanze kuuza Konyagi kwa Crown Beverage; na si vinginevyo.

“Tulimwonea huruma Mgwassa. Wakati anatafakari atamjibu nini Kapari Limited, kwani masharti ya mkataba yamebadilishwa bila kushirikishwa, makontena ya Konyagi yakaanza kupakiwa kupelekwa Kenya kwa kampuni ya Crown Beverage ambayo ni kampuni dada na SUBmiller… mbaya zaidi, Mkurugenzi wa Fedha, Michael Brown ndiye akaanza kufanya kazi za Mkurugenzi Mtendaji wa TDL, Mgwassa.

“Akawa anapokea oda zote na kupitisha malipo bila kushauriana na Mgwassa. Mbaya zaidi, wakati Kapari Limited alikuwa ananunua katoni moja ya konyagi kwa dola 24.78, Crown Beverage akawa anauziwa katoni moja kwa dola 15.52… hii maana yake ni kwamba Serikali imepoteza kodi kwa kiasi cha dola 9.26 kwa kila katoni, ambacho awali kilikuwa kinalipiwa kodi kwa kumuuzia Kapari Limited,” anasema mtoa habari wetu. Soma vielelezo Uk. 12

Uchunguzi unaonyesha kuwa kwa wastani wa kontena 15 kwa mwezi, ambazo kila kontena linachukua katoni za Konyagi 1,500, ukizidisha mara miezi 12 kwa kiwango cha dola 9.26 zinazopunguzwa kwa kuiuzia Konyagi kampuni dada ya Crown Beverage, Serikali inapoteza kodi ya makapuni kwa TBL kupitia Konyagi inayouzwa Kenya kwa wastani wa dola 750,060 kwa mwaka sawa na Sh bilioni 1.65.

Chanzo kingine kinasema Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) imefungua kesi kupinga hatua hii ya kupunguza bei ya Konyagi kupitia Kampuni ya Crown Beverage kwani kwa kufanya hivyo, fedha ambazo zingeingia serikalini kama kodi zinachukuliwa na SABmiller kupitia kampuni ya Crown Beverage kwa njia ya punguzo la bei ya Konyagi wanayonunua kutoka kiwandani Tanzania.

 

Kauli ya Mgwassa

 JAMHURI, limemtafuta Mgwassa kupata kauli yake juu ya upotevu huu wa fedha za umma, na yeye amesema kwa ufupi: “Kwa sasa nipo kwenye taratibu za kuwafungulia kesi TBL, kwa hiyo masuala hayo siwezi kuyazungumzia kwa hali yoyote. Naomba uutafute uongozi wa TBL kwani wanayo majibu kwa maswali yote unayouliza. Ukumbuke wameniondoa kazini, hivyo nikizungumza chochote, kesi yangu itakuwa hatarini.”

Habari lilizozipata JAMHURI zinaonyesha kuwa Mgwassa aliondolewa kazini baada ya kukataa mpango wa wawekezaji hao kutoka nchini Afrika Kusini kutumia udhaifu wa sheria unaoruhusu kampuni kufanya biashara na kampuni tanzu inazozimiliki katika nchi ile ile au katika nchi nyingine kwani aliona unaitia hasara Serikali kwa kupoteza kodi.

JAMHURI lilipowasiliana na maofisa wa Mamlaka ya Kodi Kenya, walisema Serikali ya Kenya inaendelea kulishughulikia suala hilo. “Hatuoni sababu kwa nini leo Konyagi iliyokuwa inaingia nchini kwa dola 24.78 kwa katoni, leo ishushwe bei na kuwa dola 15.52 tena iuzwe kwa kampuni dada ya Crown Beverage, ambayo hatuna udhibiti wa hesabu zake.

“Sisi tunaendelea na kesi, na hata kama wanauziana hiyo bei ndogo, kodi yetu tutaendelea kuidai kwa kutumia kiwango cha dola 24.78 kwani bajeti yetu tuliipitisha tukiwa na kadirio la kiasi hicho kama chanzo cha mapato kwa serikali yetu,” alisema ofisa aliyeomba asitajwe gazetini kwa maelezo kuwa yeye ni mmoja wa wasimamizi wa kesi hiyo.

 

Kapari Limited wazungumza

JAMHURI limezungumza na Kampuni ya Kapari Limited ya jijini Nairobi, Kenya inayokiri kuwa uamuzi wa TBL Group kuwabadilishia masharti ya biashara umewaumiza kwa kiasi kikubwa. Kampuni hiyo imesema ilianza biashara kwa tabu mwaka 2008 ikipigwa vita ya hali ya juu, huku viwanda vya Kenya vikifanya kampeni mbaya dhidi ya Konyagi vikiitangaza kama chang’aa (gongo) ikakosa soko, lakini baada ya kukubalika sokoni TBL Group ikabadilisha masharti ya mkataba.

“Kwa mwaka 2008, kontena moja tuliliuza kwa miezi sita. Tulikuwa na wafanyakazi, tumekodi maghala, lakini Konyagi ikawa inatangazwa vibaya kuwa hiyo ni chang’aa ya Tanzania. TBL wala hawakuwa na mpango wa kuiuza Konyagi nchini Kenya. Kulikuwa na ugumu wa aina yake.

“Tuliendelea kuiuza kwa tabu, na ilipofika mwaka 2012 ndipo biashara ikaanza kuwa nzuri. Mwaka 2013 na 2014 mwanzoni, tukaanza kuuza hadi kontena 15 kwa mwezi. Konyagi ikapendwa Kenya na ilikuwa inaelekea kuwa spiriti namba moja kwa mauzo. TBL walivyoona hivyo, wakaamua kuipa biashara kampuni yao inaitwa Crown Beverage.

“Crown Beverage wao waliangalia tunachouza, lakini hawakujua tunatumia mifumo gani kusambaza Konyagi na kama tulikuwa tunapata tasilimu kwanza au tunakopesha. Ghafla tukabadilishiwa masharti. Tukaambiwa tutauza Nairobi tu, na Crown Beverage watauza nchi nzima eneo lililosalia.

“Kwetu, hii haikuwa sahihi kwani tulikuwa tumeajiri watu wengi, tulikuwa tumefungua maghala, tulikuwa tumechukua mikopo benki na kununua malori 10 ya kusambaza Konyagi nchi yote ya Kenya, hivyo kilichotokea baada ya uamuzi huu biashara ikafa.

“Ninachokiona, sisi tumepoteza, Serikali ya Kenya imepoteza na Serikali ya Tanzania imepoteza. Tumepoteza wote kutokana na TBL kuwauzia Crown Beverage kwa dola 15 kwa katoni, wakati sisi walikuwa wanatuuzia dola 24. Hiyo kwa upande wa Serikali za Kenya na Tanzania wamepoteza kodi.

“Sisi kama wafanyabiashara tumevuruga soko. Crown Beverage wanajitangaza kuwa wao ndiyo wenye kuuza Konyagi kihalali, hali iliyoleta ushindani usio wa lazima katika soko, ikawaogopesha wateja na sasa biashara inashuka. Mimi naona sote tumepoteza, na wakati umefika sasa tukae chini tuzungumze, TBL iangalie ilikuwa inapata fedha kiasi gani kutoka Kenya na sisi tuonyeshe kodi tulizokuwa tunalipa turejee katika biashara. Tumepoteza asilimia 80 ya biashara,” anasema Meneja wa Kapari Limited, Peter Manga.

 

Crown Beverege wazungumza

Meneja Mkuu wa Crown Beverage Kenya, Ellis Muhimbise, amezungumza na JAMHURI akiwa jijini Nairobi na kusema yeye haoni tatizo kwa TBL kuamua kuwauzia Konyagi wao kwani ni kampuni dada.

Alipohojiwa kwa nini wanapewa bei ndogo ikilinganishwa na ya Kapari Limited, akasema: “Hii ni biashara kati ya kampuni na kampuni zenye udugu, hivyo usitaraji tutauziwa bei sawa na mteja wa nje.”

JAMHURI lilipomhoji kwa nini hawatumii kanuni ya biashara ya kimataifa inayozitaka kampuni zenye udugu kuuziana bidhaa kwa bei ya soko (arm’s length principle – ALP), akasema: “Hii ni mipango ya ndani.”

Muhimbise, alikiri Serikali ya Kenya kufungua kesi dhidi yao na kudai kodi kubwa, hata hivyo akasema: “Suala hili lilijitokeza, tumelishughulikia na sasa ni kama limefungwa.”

 

Mabilioni yapotea kupitia kampuni dada

 Wakati TBL wakifanya mbinu za kupunguza kodi itokanayo na mauzo ya Konyagi nje ya nchi, Kampuni hiyo pia inapunguza kodi inayopaswa kulipa kwa kuingiza gharama kubwa za uendeshaji katika hesabu zake.

Ununuzi wa bidhaa na huduma unaofanywa na TBL Group, malipo yake yanafanywa kutokea nchini Mauritius. “Mfano hai, unakuta chupa za kujazia Konyagi na bia zinauzwa chini ya Sh 200 hapa Kioo Limited, Dar es Salaam. TBL Group inazichukua hapa Dar es Salaam, lakini inapeleka invoice katika kampuni ya Mubex iliyopo Mauritius. Kampuni hii inapoleta invoice kwa Kioo Limited, inaleta imeongeza bei mara mbili ya bei halisi ya chupa.

“Kioo Limited wanaweza kufurahia kuwa wanapata dola, lakini kiasi wanachoonyesha kulipwa, kwanza sicho wanacholipwa, kwani invoice zinazoonyeshwa katika vitabu va Mubex ya Australia na vya Kioo Limited ya Dar es Salaam zinatofautiana, hivyo kinachotokea fedha nyingi zinapotea kupitia ununuzi na hivyo kuonyesha gharama za uendeshaji ni kubwa. Hali hiyo inapunguza kodi inayopaswa kulipwa serikalini. Hili serikali inavyo vyombo vya dola, ilichunguze mara moja,” anasema mtoa habari mwigine.

Mtoa habari huyu ambaye ni Ofisa Mwandamizi ndani ya TBL Group, anasema uongozi wa Wazungu ndani ya TBL Group, mara zote umejipanga kuipa vitisho Serikali kuwa wakiwabana watafungua kesi mahakamani au kujiondoa nchini na kutelekeza viwanda vya bia; kitu ambacho Serikali inapaswa kukipuuza na kuwadai kodi stahiki.

“Hivi kwa nini wasiilipe Kioo Limited moja kwa moja kutokea hapa Dar es Salaam?” Kwa nini invoice iende Mauritius, nchi inayofahamika kuwa ‘pepo ya kodi’, kwani hata kodi ya kampuni (corporate tax) wanatoza si zaidi ya asilimia 3 na wakati mwingine hawatozi kabisa? Huu ni mrija wa kupoteza fedha za umma,” anasema mtoa habari wetu.

 

Wafanyakazi wa kigeni

 Wakati mkataba wa TBL na Serikali ya Tanzania unaitaka kampuni ya SABmiller kuajiri wageni (expatriates) wasiozidi watano, uchunguzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa hadi sasa kuna wageni 43 walioajiriwa na wanafanya kazi zinazostahili kufanywa na Watanzania.

“Lengo lilikuwa kuwawezesha Watanzania kupata ujuzi na hivyo kusimamia uchumi wa nchi yao. Hata hivyo, unaweza kujua kuwa hawa wawekezaji wana mpango mahususi. Na ukitaka kujua hilo, asilimia 80 ya wananchi wa Afrika Kusini inakotokea kampuni ya SABmiller ni weusi, lakini kati ya wageni hao 43 waliowaleta hapa nchini, wachache wanatoka nchi nyingine, lakini wote wanaotoka Afika Kusini hakuna mweusi hata mmoja.

“Huu ni mpango maalumu wa kuendeleza ubaguzi wa kiuchumi katika taifa hilo wanaotaka kuhamishia hapa nchini. Kwa sasa nafasi karibu zote za juu wamezishika wao. Kila Mtanzania mwenye ngozi nyeusi, wanamwondoa haraka sana. Hata hao wanaoitwa Watanzania kwenye Bodi ya TBL, wapo kutumikia masilahi ya Wazungu hawa. Ukiangalia uteuzi wao hata Mwenyekiti wa Bodi, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (mstaafu- David Msuya) wameingia kwenye Bodi kwa kuteuliwa na SABmiller.

Ukurasa wa 10 na 11 wa Taarifa ya Hesabu za TBL Group unaonyesha kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo ina wajumbe 23; kati yao wakiwamo Watanzania 12 ambako mmoja anatajwa mara mbili kwenye Bodi hiyo kutokana na wadhifa wake. Kati ya Watanzania hao, Watanzania 10 wameteuliwa na SABmiller kusimamia masilahi yake; na wawili tu ndiyo walioingia kwenye Bodi kutokana na nyadhifa zao serikalini.

Wajumbe wa Bodi ya TBL Group Watanzania walioteuliwa na SABmiller wanaotajwa kupewa masilahi manono na kufumbia macho uozo wa kuajiri wageni wengi kuliko inavyotakiwa kisheria, kufanya ununuzi nje ya nchi, kuruhusu Konyagi kushushwa bei na hivyo Serikali kupata kodi kidogo, kuruhusu malipo ya tozo za uongozi nje ya nchi nao wametajwa.

Wajumbe hao wanaotumikia SABmiller kwa kuwa ndiyo iliyowateua ni: Mwenyekiti wa Bodi, David Msuya tangu mwaka 2005; Balozi Ami Mpungwe tangu mwaka 2001; Ruth Mollel, ambaye mwaka 1997 aliteuliwa na Serikali kuiwakilisha TBL, lakini mwaka 2002 SABmiller ikamteua kuiwakilisha kwenye Bodi na amestaafu ujumbe Septemba, 2014; na Anold Kileo aliyeteuliwa na SABmiller tangu mwaka 1999. Mwingine ni P. J. I. Lasway, Mshauri wa Biashara aliyeteuliwa mwaka 2010.

Watanzania wengine ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutokana na nyadhifa zao kama watumishi wa TBL Group wakati ripoti hii inachapishwa Machi, mwaka jana ni Mwanasheria wa TBL Group, S. F. Kilindo, Mkurugenzi Mtendaji wa TDL (aliyefukuzwa) Mgwassa, Mkuu wa Idara ya Vinywaji Baridi, K. Suma na Mkuu wa Utumishi, D. Magese.

Watanzania pekee wasio na uhusiano wa moja kwa moja na SABmiller katika Bodi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Uledi A. Mussa, aliyeingia kwa wadhifa wake; na E. Nyambibo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, anayeiwakilisha Serikali hadi sasa.

Wachambuzi wa masuala ya biashara za kimataifa wanasema kwa hali yoyote Watanzania walioteuliwa na SABmiller kuingia kwenye Bodi na wafanyakazi wa TBL Group wanaoingia kwenye Bodi kwa nyadhifa zao, kwa kila hali hawawezi kutetea masilahi ya Tanzania, bali ya SABmiller aliyewateua.

Wafanyakazi hao 43 kila mmoja analipiwa tozo ya usimamizi ya dola 88,000 za Marekani kwa mwaka sawa na dola 3,784,000 (Sh bilioni 8.3) zinazopelekwa kampuni ya Bevman Services International BV iliyoko Uholanzi; nchi inayotajwa kuwa pepo ya kodi (tax haven country).

Kiasi hiki kinachajwa kuwa ni njia ya kuchota fedha kutoka nchi zinazoendelea kwenda mataifa yaliyoendelea kwa kutumia kampuni tanzu na kinaweza kusitishwa kwa kurejea katika mkataba unaowataka kuajiri wafanyakazi wa kigeni watano tu.

Ukiacha tozo hiyo ya usimamizi, wafanyakazi hawa 43 wanalipwa mshahara kati ya dola 9,000 (Sh milioni 19.8) na dola 15,000 (Sh milioni 33) kwa mwezi. Ukizidisha mara miezi 12 ikiwa utachukua wastani wa dola 12,000 (Sh milioni 26.4) kwa kila mfanyakazi kati ya hao 43 inakuwa sawa na dola 6,192,000 (Sh bilioni 13.6) kwa mwaka.

“Kiasi hiki ukikichanganya na zile bilioni 8.3 nchi inapoteza mapato mengi mno,” kinasema chanzo chetu na kutaka nafasi za wageni zishikwe na wazawa.

 

Nembo ya Konyagi, Kibuku

 Uchungzui uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa hata vinywaji vilivyoanzishwa na Tanzania yenyewe vya Konyagi na Kibuku, tayari si mali ya Tanzania tena. Nembo ya Konyagi sasa imesajiliwa nchini Uholanzi chini ya Kampuni ya Sabmark, ambayo ni Kampuni tanzu ya SABmiller.

“Nchi hii inachezewa usipime. Konyagi ni bidhaa ya Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1970 kutokana na kitu kinachoitwa ENKONYAGI kule Bukoba, ndipo Mwalimu [Julius] Nyerere akasema tuiboreshe na Watanzania tuwe na bidhaa inayotokana na ubunifu wetu. Leo imehamishwa umiliki, nembo hii ya biashara imesajiliwa hakimiliki yake Uholanzi, na TDL kila mwaka tangu mwaka jana inalipa wastani wa dola milioni 1.0 (Sh bilioni 2) kwa kutumia nembo ya Konyagi.

“Kwa kweli nasema Serikali iingilie kati. Huu ni wizi wa mchana. Nchi haiwezi kuachwa ikaendelea kufanywa shamba la bibi kiasi hiki. Imetosha jamani. Tuna imani na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na tunaomba waliingilie kati hili kuepusha ukwepaji huu unaoumiza uchumi wa nchi changa kama yetu,” anasema mtoa habari wetu.

Awali, kabla ya ubia TBL walikuwa wakizalisha “Kibuku”, lakini sasa -kimyakimya TBL Group wamebadili jina la Kibuku na kuita “Chibuku”. Chibuku ni pombe inayozalishwa Zambia. Walichofanya, wamesajili nembo ya “Chibuku” katika kampuni ya Sabmark iliyoko Uholanzi, hivyo kwa “Kibuku” kubadilishwa jina kuwa “Chibuku” nayo sasa inalipa tozo ya mamilioni.

“Konyagi na Kibuku zinazalishwa Tanzania, zinanywewa Tanzania. Hivi inakuwaje tunalipia haki miliki huko Uholanzi na hizi ni bidhaa zetu tulizozianzisha sisi?” Mimi nadhani hapa haki haitendeki. Tunahitaji kukataa baadhi ya upuuzi,” anasema mtoa habari wetu.

 

ActionAid yaeleza nchi zinavyoibiwa

Utafiti uliofanywa na Kampuni ya ActionAid ya Uingereza na kuchapishwa mwaka 2014, umeishutumu Kampuni ya SABmiller kuwa inatumia udhaifu wa mianya ya kisheria katika Bara la Afrika kutolipa kodi inavyostahiki (Tax Avoidance).

Katika chapisho hilo, wanataja masuala kama tozo za usimamizi, kusajili nembo na haki miliki za vinywaji vilivyobuniwa Afrika vikizalishwa Afrika na kunywewa Afrika kisha vikatozwa tozo kubwa kuwa ni uchotaji wa uchumi wa nchi hizo.

Mwaka 2005 Kampuni ya SABMiller International BV ilinunua haki miliki mbalimbali zenye thamani ya paundi milioni 120 au dola milioni 200 sawa na Sh bilioni 450, kiasi wanachokitumia kuchota fedha kutoka Afrika wakidai wanalipa deni hili.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Kampuni ya SABmiller ambayo ni mbia wa TBL Group, inatumia udhaifu wa sheria za Tanzania kuhamisha fedha nyingi kwenda nje ya nchi kwa njia ya ununuzi bidhaa na huduma, gawio, haki miliki, tozo za uendeshaji na kujiuzia bidhaa kama Konyagi kwa bei nafuu kuliko bei ya soko.

 

TBL waweka mizengwe kuzungumza

 Pamoja na JAMHURI kuwasiliana na watendaji wakuu wa TBL Group na hata kupeleka maswali kwa njia ya maandishi kwa kutumia barua pepe na barua ya kawaida iliyopelekwa ofisini TBL, si Mkurugenzi Mkuu, Roberto Jarrin, wala Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TBL, Georgia Mutagahywa, waliokuwa tayari kuzungumza na JAMHURI juu ya suala hili.

Wakati hao wakigoma, mfanyakazi mwandamizi wa TBL, aliyesema yeye si msemaji, alithibitisha TBL kuwauzia Konyagi kwa bei nafuu Kampuni ya Crown Beverage, nembo ya Konyagi kuuzwa Uholanzi, Kampuni ya Mubex ya Mauritius kufanya ununuzi kutoka Kioo Limited kwa niaba ya TBL Group na kulipa tozo ya usimamizi (management fees).

“Hayo unayosema yote ni uamuzi uliofanywa kisera na Kampuni ya SABmiller kwa kampuni zake zote duniani. Ni rahisi kudhibiti ununuzi ukiwa na kampuni moja inayosimamia hayo, kuliko kutawanyika sehemu mbalimbali,” anasema.

Mfanyakazi huyo alimtuhumu Mgwassa kuwa yeye na wengine walioondolewa TBL kwa sababu mbalimbali ndiyo wenye kutoa taarifa hizo kuhusu TBL alizosema si za msingi. Alitamba kuwa tangu Mgwassa ameondola utendaji katika kiwanda cha TDL umeongezeka na wafanyakazi sasa wana uhuru kuliko wakati wowote.

“Mgwassa alilipwa haki zake zote, kwa maana ya mishahara yote hadi siku ya kustaafu. Wakati anaachishwa kazi alikuwa na umri wa miaka 57. Alilipwa hadi umri wa miaka 60. Sijui ana tabu gani huyu mzee,” anasema ofisa huyo.

JAMHURI lilipohoji kwa nini siku aliyotangazwa mfanyakazi bora wa TBL Group ndiyo aliyoondolewa kazini, alisema: “Huu ulikuwa uamuzi wa Kampuni na wala sipo kwenye nafasi ya kuuzungumzia.” Kwa upande wake, Mutagahywa, aliomba habari hii isubiri isichapishwe kwani Jarrin alikuwa na masuala muhimu ya kitaifa aliyopaswa kuyashughulikia kwanza.

Gazeti la JAMHURI limekwenda ofisini kwa Jarrin mara kadhaa, limempelekea barua pepe kwenye akaunti yake na ujumbe wa maandishi kwenye simu yake ya mkononi, lakini hakujibu hata moja.

 

Wafanyakazi wafukuzwa

 Wakati TBL wakisema hali ni nzuri, taarifa zilizolifikia JAMHURI muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni zinaonyesha kuwa hali ya mapato ndani ya TDL inazidi kuwa mbaya, kwani mauzo ya Konyagi nchini Kenya yameshuka na uzalishaji umeshuka; hivyo sasa wameamua kuanza kupunguza wafanyakazi.

Ukiacha Mgwassa; Mustapha Nassoro, Fauzia Hussein na Maneno Mbegu waliosimamishwa, wiki iliyopita wafanyakazi watatu wa Idara ya Masoko waliokuwa wanauza Amarula na mvinyo- Diana Balyagati, Gaudence Mkole na Godfrey Mandari- nao wametajwa kusimamishwa kutokana na TDL kutokuwa na uwezo kifedha.

 

Waandaa kikao cha kodi

 Katika hatua nyingine, TBL Group wameanza kikao kitakachokutanisha watendaji wa Serikali kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Fedha na Mipango, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Ushindani wa Haki (FCC), Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), wabunge wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Viwanda na Canbank, kampuni inayoongoza duniani kwa uchambuzi.

Mkutano huu unaelezwa kuwa unalenga kuishawishi Serikali ianze utaratibu wa kuitoza kodi TBL Group kwa njia ya kukadiriwa badala ya kuhesabiwa kura moja moja.

 

Serikali yazungumza

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile ameliambia JAMHURI kuwa taarifa za ukwepaji kodi TBL wamezipata, na wanazifanyia kazi kwa kina kuhakikisha kodi zote zinalipwa kwa nia ya kuongeza mapato na kuboresha huduma za jamii.

“Serikali haijalala. Wajue tu, tunayafanyia kazi na si muda jamii itaona majibu. Kila anayestahili kulipa kodi ni lazima alipe kodi,” anasema Dk. Likwelile.

 

Je, unajua mauzo ya TDL yameshuka kiasi gani? Je, unajua mpango walionao TBL dhidi ya kiwanda hiki? Usikose Gazeti la JAMHURI wiki ijayo.

By Jamhuri