1Wiki tatu tangu gazeti hili limeanza kuchapisha taarifa za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL Group) inayomiliki Kampuni za Tanzania Distillers Limited (TDL), Darbrew Limited na Tanzania Breweries Limited (TBL) zinazomilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania (38%) kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Kampuni ya SABmiller yenye hisa asilimia 62, watendaji na wajumbe wa kampuni hiyo sasa maji yamewafika shingoni.

Taarifa za uchunguzi zilizochapishwa na gazeti hili la JAMHURI kwa kubainisha mbinu chafu zinazotumiwa na kampuni hiyo kukwepa kodi na kuhamisha faida waliyostahili kupata TBL wakalipa kodi kubwa ya kampuni, watendaji waliokuwa na dharau kubwa kwa gazeti hili awali, sasa wanahaha.

Kuhaha kwao kunatokana na hatua ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvamia ofisi za TDL moja ya kampuni zinazomilikiwa na TBL Group ambako walichukua kompyuta tatu zenye taarifa nyeti na kuondoka nazo kwenda kuzifanyia uchunguzi.

Hali hiyo imewafanya watendaji na wajumbe wa Bodi wa TBL kuwa na mikutano ya mara kwa mara, ambapo walikubaliana awali kutoa tishio la kwenda Mahakamani kwa nyakati tofauti.

“Tumepata taarifa za ukwepaji kodi kwa kampuni ya TBL kwa masikitiko makubwa. Hatuwezi kuwahumu moja kwa moja kabla ya kuwapa nafasi. Nimeanzisha uchunguzi wa kina, tutawakagua wanachofanya sasa, walichofanya na wanachopanga kufanya kuona kama kinaendana na matakwa ya kisheria.

“Chini ya Serikali hii ya Awamu ya Tano, Mhe. Magufuli amesema wazi. Hatutamuogoma mtu au kampuni na wala hatutamuonea mtu au kampuni. Tutawasiliza TBL, na tunasema ndiyo wanalipa kiasi kikubwa cha kodi, lakini katika uchunguzi unaoendelea tutataka kujiridhisha iwapo wanalipa wanachostahili kulipa,” Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki.

Amesema wakikuta TBL wanalipa kodi inavyostahiki, watawapongeza, lakini wakikuta wanalipa pungufu, watatumia sheria kuwadai tofauti ambayo watakuwa hawakulipa na ikithibitika vinginevyo, kama watabaini mchezo mchafu wanaohusika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu makosa ya jinai.

Kifungu cha 35 cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinasema bayana kuwa ikithibitika katika uchunguzi kuwa mtu au taasisi iliandaa utaratibu wa kuepuka kodi, basi Kamishna wa TRA atamwandikia mtu huyo au taasisi na kufanya marekebisho (kumtaka alipe) kiasi cha kodi alichokwepa.

 

Vitisho vyagonga mwamba

Machi 3, 2016 TBL kupitia kampuni ya Law Associates Advocates, ilililetea gazeti la JAMHURI barua ya madai wakitaka kulipwa Sh milioni 500 na ikitaka kuombwa radhi kwa maelezo kuwa gazeti hili linachapisha kashfa dhidi yao. Walitoa muda wa siku 7 zilizopaswa kuisha Machi 10, 2016. Katika barua hiyo, walieleza nia ya kumshitaki Mhariri Mtendaji wa JAMHURI, Mhariri wa JAMHURI na mwandishi wa habari hizi za uchunguzi; Deodatus Balile.

Kwa mpangilio uleule na maneno yanayofanana kwa ukaribu, Machi 4, 2016 wajumbe wa Bodi ya TBL, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (mstaafu), Cleopa David Msuya, Balozi Ami Mpyungwe na Arnold Kilewo, nao walileta barua ya madai ya Sh milioni 600 na kuombwa radhi.

Hawa kwa kutaka kuonyesha wametokea kampuni tofauti za wanasheria, waliwasilisha madai yao kupitia kampuni ya uwakili ya NexLaw Advocates, wakidai wameaibishwa kuwekwa picha zao ukurasa wa mbele wa JAMHURI wakihusishwa na utendaji mbovu na ukwepaji kodi kwa TBL.

Katika matoleo mawili yaliyotangulia; Na 231 na 232, JAMHURI lilichapisha habari za uchunguzi zikionyesha jinsi TBL wanavyotumia udhaifu wa sheria kukwepa kodi. Sheria inatumia maneno tax avoidance, yenye maana ya kuepuka au kukwepa kodi katika Kiswahili.

Wanachofanya, walikuwa wakiuza katoni ya Konyagi kwa Kampuni binafsi ya Kapari Limited ya Kenya kwa gharama ya dola 24.78, baadaye wameamua kuuza Konyagi hiyo kwa Kampuni yao tanzu ya Crown Beverage kwa dola 15.52. Uamuzi huu unawafanya TBL kupata dola 9.26, ambazo hazitozwi kodi kwa kila katoni ya konyagi inayouzwa nje ya nchi. Mwisho wa mwaka, wataonekana kupata faida kidogo na hivyo kulipa kodi kidogo ya kampuni.

Suala jingine lililoandikwa na JAMHURI, ni kuwa TDL kwa sasa inalipia gharama za haki miliki ya nembo za Konyagi na Kibuku kilichobadilishwa jina kuwa Chibuku, kwani imehamishwa kutoka hapa nchini na kupelekwa kampuni tanzu ya TBL/SABmiller iitwayo Sabmark yenye makao makuu nchini Uholanzi. Konyagi hadi sasa si mali tena ya Tanzania, hivyo kiwanda cha Konyagi kinalipa dola milioni 1 kila mwaka kupata ruhusa ya kutumia nembo inayotaniwa na wengi kuwa ni ‘Mzaramo’ aliyekunja mikono.

Gazeti hili liliandika kuwa chupa za konyagi zinanunuliwa kutoka Kioo Limited Dar es Salaam, lakini malipo yake hati ya madai inatolewa katika kampuni tanzu nyingine ya SABmiller iliyoko nchini Mauritius iitwayo Mubex, ambako inatozwa bei zaidi ya uhalisia. JAMHURI limechapisha taarifa ya mwaka ya TBL ambayo Mkurugenzi Mkuu, Roberto Jarrin na Mwenyekiti wa Bodi, Msuya walitoa taarifa inayotofautiana juu ya kiwango cha mauzo kushuka mwaka uliotangulia, faida iliyopatikana na kiasi cha kodi ilicholipa TBL.

Jambo jingine lililoandikwa na gazeti hili ni kwamba TBL inanyofolewa fedha nyingi kwa kuajiri wageni wanaolipwa mishahara kati ya dola 9,000 na 15,000 kwa mwezi, ila mbaya zaidi kila mgeni analipiwa dola 88,000 kila mwaka zikiwa ni tozo ya usimamizi. Fedha hizi zinalipwa kwa kampuni ya Bevman Services iliyopo nchini Uswisi. Mkataba wa ubia unawataka TBL kuajiri wageni watano, ila taarifa za uchunguzi zinaonyesha wameajiri wageni 43 hadi sasa. Katika barua yao, Msuya, Kilewo na Mpungwe wanasema wageni waliopo ni 26 tu.

Viongozi hawa walitafutwa, kampuni ya Kapari Limited ilijibu, Kampuni ya Crown Beverage ilijibu ila TBL pamoja na kupelekewa maswali, walijifanya hawana muda na kwamba wanazo shughuli nyingi za kufanya hivyo mwandishi asubiri hadi watakapopata muda. Mwandishi alielezwa maneno hayo na wasaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Roberto Jarrin.

Baadhi ya wakurugenzi wenye hisa katika TBL na kiwango kwenye mabano ni Msuya (8,000), R. O. S. Mollel (3,600), A. R. Mpungwe (7,000), A. B. S. Kilewo (37,641) na P. J. I. Lasway (36,162). Viongozi hawa sasa wanamiliki jumla ya hisa 84,403, lakini vitabu rasmi vya TBL kwa uzembe vinaonyesha kuwa wanamiliki hisa 92,403, wakati Serikali ya Tanzania haina hata hisa moja baada ya kuziuza zote siku chake kabla ya uchaguzi.

 

Wafungua kesi mahakamani

Siku moja baada ya muda wa siku 7 kuisha ilizotoa TBL, JAMHURI lilipata taarifa za harakati na vikao vilivyotokana na mshituko wa jinsi gazeti hili linavyoendelea kuchapisha taarifa za kampuni hiyo kukwepa kodi kwa ujasiri hata baada ya kutishwa.

“Nakwambia hapa ofisini kazi zimesimama. Wanaona mnachoandika sasa kitafumua kila kitu. Wamejadiliana kila mbinu za kufanya, wakaamua waende kufungua kesi Mahakama Kuu, yaliyowakuta huko hawawezi kusimulia. Ukipata fursa waulize,” mmoja wa wafanyakazi aliliambia JAMHURI.

Baada ya taarifa hizo na katika hali ya mshangao, kampuni ambayo awali ilidai ilipwe Sh milioni 500, iliwasilisha Amri ya Zuio (Court Injunction) kulitaka gazeti la JAMHURI lisiendelee kuchapisha walichokiita KASHIFA dhidi ya Kampuni ya TBL kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 Kifungu cha 40(2), ikisomwa kwa pamoja na Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mwaka 2002, Mahakama ya Hakimu Mkazi yoyote nchini ina uwezo wa kusikiliza shauri la madai lisilozidi Sh milioni 100 kwa mali inayohamishika.

Hivyo, TBL kwa kwenda Kisutu, ni wazi inathibitisha alicholidokeza gazeti hili mmoja wa wafanyakazi wa TBL kuwa wamegonga mwamba Mahakama Kuu, hivyo wakaona kuliko kukosa yote, bora washuke na kuacha madai yao ya milioni 500 waweze kuomba angalau kiasi hicho kisichozidi Sh milioni 100.

Katika kesi ya msingi wamemshitaki Mhariri Mtendaji wa JAMHURI na Kampuni ya JAMHURI Media Limited. Amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, T. K. Simba, huku akisema kesi ya msingi itasikilizwa Machi 17, 2016.

 

JAMHURI latoa taarifa

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kampuni ya JAMHURI Media Limited mwishoni mwa wiki, ilieleza masikitiko yake, kwa TBL kutokuwa waungwana na kukiri ukweli wakawaomba radhi Watanzania kwa kutolipa kodi stahiki. Kampuni ya JAMHURI, imeeleza kusikitishwa na Amri ya Mahakama, iliyodai kuwa gazeti la JAMHURI limezuiliwa kuchapisha uongo na kashfa dhidi TBL.

“Amri hii ni matusi kwa uongozi wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, Msajili wa Magazeti Idara ya Habari Maelezo, wahariri, waandishi na wafanyakazi wa Kampuni ya Jamhuri. Kampuni hii haikusajiliwa kuandika uongo, matusi au kashfa kwa mtu au taasisi yoyote. Tukithubutu kufanya hivyo kwa kutumia gazeti hili linaloheshimika, tungekwishafutiwa usajili siku nyingi.

“Sisi tunayachukulia maneno yaliyomo kwenye Amri ya Zuio kuwa ni juhudi za makusudi za TBL kuharibu heshima ya gazeti la JAMHURI, ambalo Februari 13, 2016 limesifiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kutokana na kazi nzuri ya uchunguzi wa kina na kuandika habari za kweli juu ya matumizi ya Mita za Kupimia Mafuta (flow meters) na nyingine nyingi tulizoandika kama hizi za TBL.

“Tunao uzoefu wa watu wanaokiuka sheria kukimbilia mahakamani na kutoa hukumu kwa vyombo vya habari kwa nia ya kujificha nyuma ya pazia la sheria. Tulipoanza kuandika habari za Bandari akina Madeni Kipande walifanya hivyo, na wengine wengi. Katika hili tunasema TBL waache mchezo mchafu. Walipe kodi inayostahiki, wauze bidhaa zao kwa bei ya soko na waache kuhamisha fedha kwenda nje ya nchi kwa kutumia kampuni tanzu na kwa njia za ujanjaujanja.

“Tutalinda heshima ya gazeti hili kwa gharama yoyote. Tunaisubiri kwa hamu siku ya kwenda Mahamamani, maana ukiacha Amri ya Zuio la kosa tusilotenda, hatujaletewa wito wa kwenda mahakamani, wala kupewa Hati ya Madai kujua tutakwenda kujibu nini. Tumezungumza na jopo la wanasheria wetu, na tunajiandaa kuifungulia kesi TBL tutoe fundisho kwa watu au taasisi zinazotenda maovu na kujificha nyuma ya mwavuli wa sheria, kisha wakatoa vitisho kwa vyombo vya habari. Tuna imani na Mahakama na tunajua katika hili, haki itatendeka.

“Tunajua akina Msuya, Kilewo na Mpungwe, nao wanaweza kushawishika kufungua kesi baada ya siku 14 walizotoa na kwa kurejea historia ya walivyoleta barua ya madai, mawasiliano ya karibu wanayofanya na uongozi wa TBL na taarifa tunazopata za hofu iliyowajaa. Hawa nao tunawasubiri kwa hamu, na tunasema watimize wajibu wao kuisaidia nchi isipoteze mapato eti tu, kwa sababu wameteuliwa na SABmiller. Wakumbuke ni Watanzania na kwao Tanzania inapaswa kutangulizwa mbele.

“Tumaamini wakati umefika kwa Wanahisa kusimama na kudai haki zao, na kuhoji kama wajumbe wa Bodi wanatetea masilahi yao au wanatetea masilahi ya aliyewateua kuingia kwenye Bodi.

“Tunaomba Watanzania waendelee kuliamini gazeti la JAMHURI, lililojitolea kutetea haki za wanyonge. Tunaamini tukiwabana wakwepa kodi nchini kulipa kodi stahiki, huduma za jamii kama elimu, afya, maji, umeme, mama na mtoto, miundombinu ya barabara, reli, meli na mashirika ya ndege vitaimarika.

“Nchi zilizoendelea zilidhibiti ukwepaji wa kodi na ndiyo maana zinatoa misaada kwa nchi maskini. JAMHURI limejitolea kupambana kulitoa taifa letu katika unyonge wa kuomba misaada. Tunawashukuru Watanzania kwa kutuunga mkono katika adhima hii na tunaiishi kaulimbiu yetu kuwa TUNAANZIA WANAPOISHIA WENGINE,” ilisema taarifa ya Kampuni ya Jamhuri Media Limited.

 

Wafanyakazi wadai mikataba

Baadhi ya wafanyakazi waliowasiliana na JAMHURI, wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya TBL kutowapatia mikataba ya kazi na hivyo kuwaacha wakiwa vibarua kwa muda mrefu.

Wamelieleza JAMHURI kuwa baadhi ya wafanyakazi wamefanya kazi hadi miaka 10 kama vibarua bila kupewa mikataba, na hivyo wanadhani habari zinazoandikwa na JAMHURI zinaweza kuwa ukombozi kwao.

“Hata hela tunayolipwa ni Sh 5,700 kwa siku, kula kwako, usafiri kwako, je, kama una familia utaishije, au wanataka watu wawe wezi mjini? Tunajituma lakini tunadharauliwa ebu njooni siku moja mje mjionee wanahitaji kutumbuliwa hawa TBL ni jipu kweli… wabongo tunaonekana hatuna thamani kwao,” alisema mmoja wa vibarua.

Mwingine aliliambia JAMHURI kuwa wapo vibarua zaidi ya 30 waliopo kazini kwa zaidi ya miaka 10, lakini wanafika kazini watu wasio na uzoefu wanaajiriwa, ambao bado kazi zao zinaendelea kufanywa na hao wanaoitwa vibarua, kitu alichosema ni kero kubwa.

“Zikitokea nafasi wanakuja wageni wanapita kiurahisi kwa vile ni ndugu zao ila wajue haya maisha yana mwisho. Tangu jana (Jumatano iliyopita) kulikuwa na ukaguzi na sijui ni wa nini maana wanatuficha wakifika wakaguzi, hatuambiwi ukweli tunaambiwa tusiende kazini, sasa sijui wanaogopa nini,” alisema kibarua mwingine.

Kibarua mwingine naye alisema pesa wanayolipwa haitoshi: “Wanatudhulumu wanashiba wao, wanabadilisha magari mazuri kila siku. Serikali isipoingilia kati hili suala hata kodi wataacha kulipa. Wanajiamini balaa. Wakikuona kimbelembele wanakufukuza kazi… sisi tumekuwa watu wa kuomba misaada kwa ndugu wakati tunafanya kazi kwenye kampuni kubwa.”

Mwingine aliliambia JAMHURI: “Kaka nakupongeza kwa habari zako nzuri juu ya TBL. Tanzania ni ya kwetu, hao wageni wasitake kutuvuruga. Waziri alione hili atusaidie, walipe kodi tupate haki za wafanyakazi. Nakupongeza kwa leo habari zako zimewafanya Wazungu wanaotutambia muda wote wachanganyikiwe,” alisema mfanyakazi mwingine aliyekuwa na furaha baada ya kusoma JAMHURI Jumanne ya Machi Mosi.

Mfanyakazi mwingine, alisema: “Walivyosikia kuna gazeti limetoka, wakawatuma watu kutoka ndani harakaharaka wakalilete walisome vizuri. Hapo hapo, tukaambiwa turudi nyumbani kazi hakuna,” alisema kibarua mwingine.

Katika hatua nyingine, wafanyakazi wamelalamikia hatua ya vizibo vya bia zinazozalishwa na TBL kununuliwa nchini Kenya ingawa hapa Tanzania kuna viwanda viwili vya kutengeneza vizibo.

“Kwa nia ya kuwapa ajira Watanzania vizibo na bidhaa nyingine zingekuwa zinanunuliwa hapa nchini. Kununua vizibo kutoka Kenya ni kupunguza ajira za Watanzania,” alisema mmoja wa wafanyakazi.

 

Uhamiaji kuwavamia TBL

Kamishna wa Mipaka na Operation, Abdulla Abdalla, ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa jana Idara ya Uhamiaji ingevamia TBL kwa ajili ya kuchunguza wafanyakazi wa kutoka nchini Afrika Kusini, wanaofanya kazi  bila vibali.

“Kuna msamaria mwema ambaye ametupa taarifa hizo, hivyo nimemwagiza RMO (Regional Immigration Officer) wa Dar es Salaam kuhakikisha hiyo ndiyo inakuwa kazi ya kwanza kufanyika Jumatatu,” alisema.

Hadi tunakwenda mitamboni, ilikuwa hatujapata taarifa iwapo kazi hiyo imefanyika kwa ufanisi au la. Taarifa kamili gazeti litaitoa Jumanne ijayo.

 

ActionAid waanika wanavyokwepa kodi

Tangu lilipochapishwa kwa mara ya kwanza Novemba, 2010 Calling Time, limekuwa jarida mrejeo katika mjadala unaozidi kukua juu ya ukwepaji kodi kwa kampuni za kimataifa katika nchi zinazoendelea. Yafuatayo ni maelezo kwa ufupi juu ya kinachoendelea.

Chapisho hili lilichapishwa mwaka mwaka 2012 lakini kwa nguvu ya aina yake limeendelea kutoonekana hadharani, hadi gazeti la JAMHURI lilipofanya uchunguzi wa kina na kubaini uwapo wa jarida hili linalofichwa kama almasi.

 

Lilivyopokelewa Africa

Calling time, limewavutia maafisa kodi kwa bara lote la Afrika na nje ya Afrika. Mwezi Juni, mwaka 2011, idadi kadhaa ya mamlaka za kodi kutoka nchi za Afrika walikutana nchini Afrika Kusini na katika taarifa yao, walieleza nia ya kufanyia kazi taarifa zilizochapishwa na jarida hili. Katika mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Wasimamizi wa Kodi barani Africa (ATAF), mjadala ulijikita katika utamaduni wa kampuni za kimataifa kuuziana bidhaa kwa kufuata bei za soko (arms lengthy theory or transfer pricing) badala ya kupunguza bei kwa kuziuzia kampuni tanzu.

Kutokana na sababu za kisheria, mkutano huo haujadili masuala mahususi yanayoihusu SABmiller na ulipaji kodi, lakini mkutano ulizaa mkataba wa kimataifa wa kodi, uliowasilishwa kwenye Baraza la ATAF, lililofanyika Februari, 2012.

Mkataba huu unaziwezesha nchi za Afrika kufanya kazi pamoja kuchunguza masuala ya kodi kwa kampuni za kimataifa zinazofanya kazi barani humo, hatua ambayo ni ukombozi mkubwa katika kupambana na ukwepaji kodi na hivyo kuongeza mapato (ya serikali za Kiafrika).

ActionAid imekuwa ikifanya kazi na mamlaka za kodi na serikali katika nchi mbalimbali zinazoendelea kujadili masuala yaliyoibuliwa katika jarida la Calling time. Nchini Ghana, ambako ripoti hii imejikita (huku ikitoa mifano halisi kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwamo Tanzania), tulifanya kazi na wadau kuandaa matukio mawili; kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari waweze kuchunguza na kuandika masuala ya kodi, na kuandaa mjadala wa ukwepaji kodi kwa kampuni za kimataifa.

Mjadala huu ulihudhuriwa na maafisa kutoka Mamlaka ya Kodi ya Ghana (GRA) na Mwakilishi wa Ghana katika Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kodi.

Kwa Afrika Kusini, ambako ni nyumbani na chimbuko la Kampuni ya SABmiller, ActioAid imefanya kazi na wenyeji kuandaa semina ambayo kwa mara ya kwanza ilikutanisha mafiasa wa kodi na vyama vya kijamii nchini humo. Maafisa Kodi katika baadhi ya nchi za Amerika ya Kusini, ambako SABmiller imehodhi soko la bia, wameonyesha shauku kubwa ya kujifunza kutokana na utafiti wetu.

 

Mjadala wa Kimataifa

Kodi katika nchi zinazoendelea, na ukwepaji kodi wa kimkakati, sasa unakuwa mjadala mkubwa katika maendeleo ya kimataifa. Ushahidi na uchambuzi katika Calling time, vimekuwa mjadala mkubwa katika mikutano ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kodi, ATAF na OECD, ambayo kanuni zake za kudhibiti ukwepaji wa kisheria zimechambuliwa katika ripoti hii.

Shirika la Fedha Duniani (IMF), nalo limeonyesha nia ya kutumia Calling time kama kielelezo jinsi nchi zinazoendelea zinavyopaswa kujengewa uwezo. Makala iliyochapishwa na mmoja wa maafisa wake, ambaye awali alikuwa mkaguzi wa kodi nchini Mexico, aliuchambua uchunguzi kwa kina na kusema chapisho hili limeonyesha “mpango wa shari wa kodi” ambao “unaziwezesha kampuni za kimataifa kuweka mfumo wa kuhamishia faida nje ya nchi na kukwepa kodi katika nchi zinazoendelea.” Akaongeza, ripoti hii inaibuka suala zito lisiloweza kufumbiwa macho.

Jarida la International Tax Review, limeitaja Calling time kama “wanamapinduzi waliovuta hisia za jamii, na likaiweka ActionAid katika orodha ya watu au taasisi 50 duniani zenye uwezo wa kuhamasisha ulipaji kodi.

Zaidi ya watu 10,000 duniani wemechukua hatua, wameitaka SABmiller kuwajibika zaidi katika masuala ya kodi kwa nchi zinazoendelea. Kampuni imehojiwa kupitia mahojiano ya vyombo vya habari, na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Edinburg, Uingereza wamepiga kura kuzuia bia za SABmiller zisiuzwe katika kantini ya wanafunzi chuoni hapo.

Wamesema ukwepaji unaofanywa huzunguka katika nchi za Australia, Sweden, Uholanzi, Ghana, Afrika kusini, Senegal na Marekani. SABmiller kwa upande wao wamejibu kilio hiki kwa njia ya kukanusha na kufumba midomo.

Katika majibu yao kwa Calling time, wamesema kodi ya kampuni “ni njia dhaifu ya kupima mchango wa kodi yote waliyochangia kwa nchi kama Ghana.” Accra Brewery inatajwa kuchangia paundi milioni 7 (Sh bilioni 22) kama mchango wa jumla wa kodi nchini Ghana. Kiwango hiki kinapotosha. Kinajumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru, kodi ambazo hulipwa na wananchi wa kawaida, lakini inakusanywa na kiwanda kutoka kwa wateja wa rejareja (hili ndilo wanalofanya Tanzania pia).

Kama inavyoonyesha Calling time, Kiwanda cha Bia cha Accra hakijalipa kodi ya mapato hata chembe kwa mwaka 2009, kutokana na malipo wanayofanya kwenda nchi ambazo ni pepo kwa kodi (tax havens).

Hatufahamu iwapo Accra Brewery wameishalipa kodi yoyote tangu taarifa hii ilipochapishwa, wala iwapo malipo ya nchi zinazofahamika kama pepo ya kodi yameendelea, maana mwishoni mwa mwaka 2010 SABmiller iliwanunua wanahisa wadogo katika kiwanda hicho, ikakiondoa kiwanda hicho kwenye Soko la Hisa la Ghana na hivyo kukwepa wajibu wa kutoa taarifa kwa umma.

Hesabu za kampuni tanzu za SABmiller nchini Tanzania, Zambia na Msumbiji, zinaonyesha kupungua kwa kazi zinazofanywa na kampuni dada ya SABmiller iliyopo Mauritius (Mubex) katika kampuni hizo, ila zinaonyesha ongezeko la malipo ya mrahaba na tozo za usimamizi zinazolipwa katika nchi zifahamikazo kama pepo ya kodi.

Kwa kipindi cha miezi 18 tangu jarida la Calling time lichapishwe dunia imeshuhudia kukua kwa mjadala wa ukwepaji kodi kisheria (tax avoidance) kwa watu kufanya maandamano katika miji mbalimbali duniani.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa nchini Uingereza kuhusiana na ukwepaji kodi, asilimia 72 ya waliohojiwa walisema, “kampuni zinapaswa kulipa kodi yote, na haikubaliki kwao kutumia upungufu wa kisheria kuepuka kutimiza wajibu wao.”

Kampuni za kimataifa, sasa zimeanza kuchukua mkondo mpya kwa kukubali ukweli huu, ikirejewa andiko lao la hivi karibuni lililotolewa na Shirikisho la Wenye Viwanda Uingereza, lililosema: “Moyo wa mashirika kuelekea kodi umebadilika – kampuni zinaendelea kufahamu masuala ya heshima [yao juu ya ukwepaji kodi] na zinaendelea kujihusisha kwa karibu juu ya usimamizi wa masuala ya kodi.”

Kwa kushindwa kukiri kuwa inakwepa kodi, Kampuni ya SABmiller (inayoimiliki TBL Group kwa Tanzania) inajiweka katika hatari ya kuachwa nyuma kadri utamaduni wa kuwajibika katika kulipa kodi unavyokua duniani.

 

Muhtasari

Ghana inajivunia kuwa mwaka 1957, ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupata uhuru. Mwaka 2010, nchi hii inachukuliwa na wengi kama mfano wa uchumi na uongozi bora, na kwamba inafanya vizuri katika suala la kutimiza malengo ya Milenia. Lakini, kama nchi nyingine barani Afrika, serikali yake inahitaji kodi nyingi zaidi kutoa huduma za msingi za jamii kumaliza umaskini.

Katika karne ya 20, Ghana ilipata jambo jingine la kuifanya kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika, kwa mji wa Accra kujenga kiwanda cha kwanza cha bia, ambacho sasa kinamilikiwa na kampuni kubwa ya kimataifa iitwayo SABmiller.

Accra Brewery imechukuliwa kama mfano wa mbinu za zinazofanywa na wafanyabiashara wakubwa kuepuka kodi ya mapato. Haijalipa kodi ya mapato kwa miaka miwili, lakini imehamisha mamilioni ya pauni kwenda kampuni dada zilizoko katika nchi zijulikanazo kama pepo ya kodi. Kampuni ya SABmiller inapata faida ya pauni bilioni 2 (karibu Sh trilioni 7) kwa mwaka.

Uchunguzi wa ActionAid ulitumia hesabu zilizokaguliwa, mahojiano na maofisa wa Serikali na mbinu za kiuchunguzi zilizobainisha jinsi SABmiller inavyoepuka kodi kwa Afrika nzima na dunia. Gharama kwa Serikali zilizoathiriwa zinaweza kufikia hadi pauni milioni 20 (Karibu Sh bilioni 70) kwa mwaka.

Kodi hulipia huduma kwa ajili ya maisha yetu ambayo hujumlisha shule, hospitali na barabara kwa mfano. Kama jamiii inatuunganisha kimkataba na Serikali ambako tunalipa na tunatarajia wazitumie vema. Kodi ni takwa la msingi kwa kila nchi ambayo pia ni msingi wa ukuaji wa uchumi na ulinzi wa haki za binadamu.

Kampuni za kimataifa zinazotengeneza mabilioni ya pauni katika nchi zinazoendelea kila mwaka, pia zinahitaji shule, hospitali na barabara zinazojengwa na walipa kodi sawa na wenyeji wa nchi wanakofanyia biashara.

Hata hivyo, ukwepwaji wa kodi umekuwa sehemu ya maisha ya uwekezaji katika nchi zinazoendelea. Umoja wa Ushirikiano wa Maendeleo na Uchumi (OECD), ulioteuliwa na mataifa tajiri kama kituo cha kupiga vita ukwepaji kodi, unakisia kwamba Afrika inapoteza kodi nyingi zinazochepushwa kwenda nchi zijulikanazo kama pepo za kodi kuliko misaada inayopata kwa mwaka.

Mbinu chafu za kutafuta jinsi ya kulipa kidogo, kutengeneza mifumo isiyotabirika ya mashirika, kuhamisha fedha kupitia kampuni hewa za nchi nyingine na kuajiri wataalamu wanaolipwa fedha nyingi zimebainika kuwa mbinu zinatumika kisheria, kupoteza mapato katika nchi zinazoendelea. Hakika hili limekuwa ni jambo la kawaida na linalokubalika kama njia ya kawaida ya kufanya biashara. Njia hii inazipa kampuni za kimataifa faida ya kipekee ikilinganishwa na kampuni za ndani wanazoshindana nazo.

Kuna ishara kwamba wimbi linageuka kwenda kinyume na ukwepaji kodi katika nchi zinazoendelea. Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini, ameuelezea mpango wa kuepuka kodi kama kansa ya hatari inayokula nguzo ya mapato kwa nchi nyingi.

Mshirika Mwandamizi wa Uhasibu katika Shirika la PriceWaterhouse Coopers ameliambia gazeti la Daily Telegraph kwamba suala la kodi na nchi zinazoendelea ni ajenda na kampuni zilizojipanga vema yazipasa kuifikiria.

SABmiller ni Kampuni ya Bia ya pili kwa ukubwa duniani inayofanya kazi katika mabara yote sita ya ulimwengu huu. Baadhi ya bidhaa inazouza ni zenye majina makubwa kimataifa kama Grolsch, Peroni na Miller. Pia inauza bia ya kwanza kutengenezwa barani Afrika Castle na Stone Lager. Wanauza vinywaji baridi. Afrika ni nyumbani ilikoanzia biashara yake ambako pia ina viwanda vingi vya bia.

Hata hivyo, kampuni inamiliki kampuni 65 zilizoko katika nchi zijulikanazo kama pepo ya kodi ambazo idadi ya kampuni ni nyingi kuliko idadi ya viwanda ilivyonavyo barani Afrika. Uchunguzi wetu unaonesha kwamba mbinu za kiufundi za kihasibu zinaiwezesha SABmiller kuhamisha faida kutoka kampuni za Afrika na India (ikiwamo TBL ya Tanzania) kwenda katika nchi ambazo ni pepo ya kodi. Utaratibu huu unaonesha wazi kuwa SABmiller inajijengea mazingira angalau ya kutolipa 1/5 ya kodi ya kampuni kwa nchi za Afrika.

 

Nani analipa zaidi?

Ghana imepata ufanisi mkubwa kijamii na kiuchumi katika miaka 20 iliyopita. Tangu mwaka 1990 idadi ya Waghana ambao wanakosa chakula imepunguzwa kwa robo tatu, na wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi wameongezeka na kufikia watoto nane kwa 10 kati ya wasichana na wavulana. Nchi sasa imekuwa na uchaguzi huru na wa haki mara tano.

Mwaka 2010, timu yao ya taifa ilifikia robo fainali ya Kombe la Dunia na Ghana imefanya maendeleo ya kweli katika ukusanyaji wa kodi kwa sasa ikikusanya asilimia 22 ya pato la taifa ambayo ni juu kuliko nchi jirani yoyote ingawa haijafikia lengo la kidunia ambayo ni wastani wa asilimia 36.

Hata hivyo, Ghana inahitaji kuongeza nguvu ili ifute umasikini. Wanawake wa Ghana wana hatari ya kufariki mara 70 zaidi wakati wa kujifungua ikilinganishwa na wenzao wa Uingereza. Watoto wa Ghana wako katika hatari ya kufariki mara 13 zaidi kabla ya kufikisha miaka mitano ikilinganishwa na watoto wa Uingereza.

Theluthi moja ya Waghana hupata ugonjwa wa Malaria kila mwaka. Kuna mambo mengi ambayo Ghana ingeweza kuyafanya kuboresha maisha ya wananchi iwapo tu ingepata fedha kutokana na kodi inayokusanywa kama kampuni hizi zingekuwa hazikwepi.

 

Mwanamama alipa kodi kuliko kiwanda

Kiwanda cha Bia cha Accra nchini Ghana kinachomilikiwa na SABmiller ambacho ni kikubwa kuliko vyote nchini humo chenye kuzalisha bia zenye thamani ya pauni milioni 29 (karibu Sh bilioni 80) na bado kinakua katika miaka miwili iliyopita hesabu zake zinaonesha kimepata hasara na katika miaka minne (2007-2010) kimelipa kodi mwaka mmoja tu.

“Haaa! Siamini,” anasema Marta Luttgrodt alipoambiwa ukweli huo. Marta anauza bia za SABMiller katika mgahawa mdogo wa chakula na vinywaji, akitumia mwamvuli uliotengenezwa na kiwanda hicho wenye kuuzwa 90p (Sh 2,500). Yeye na wafanyakazi wake watatu hufanya kazi kwa bidii waweze kufanikiwa. Huanza kuandaa chakula saa 12.30 asubuhi kila siku na kufunga mgahawa wao (Kijiwe cha Mamam Ntilie), kila saa 2 usiku.

Biashara ya Marta hupata faida ya pauni 220 (Wastani wa Sh 630,000) kwa mwezi. Kama mlipa kodi anapaswa kupata na kutunza stempu mbili za ushuru wa mapato kama uthibitisho kwamba amelipa kodi ya pauni 11 (Karibu Sh 30,800) kila mwaka anazolipa kwa Mamlaka ya Manispaa ya Accra. Pia analipa pauni 9 (Karibu Sh 25,200) kila robo ya mwaka kwa Mamlaka ya Mapato ya Ghana (GRA). Kwa GRA jumla analipa wastani wa Sh 100,800 kwa mwaka zikijumlishwa  na za kodi za jiji la Accra kwa mwaka analipa jumla ya shilingi za Kitanzania 131,600.

Kodi anayolipa Marta inaweza kuonekana kuwa ni ndogo kwa kila viwango, lakini kwa njia ya kushangaza amelipa kodi kubwa ya mapato katika miaka iliyopita kuliko jirani yake (Kiwanda cha Bia cha Accra) na bosi wake ambayo ni kiwanda hicho kinachomuuzia bia na kulipa kodi yeye, lakini chenyewe hakilipi kodi ya mapato. SABmiller ni kampuni yenye ukwasi mkubwa duniani.

Serikali ya Ghana inakimbizana na wachuuzi kama akina Marta kuwataka waingie katika mfumo rasmi wa kulipa kodi na inachukulia hatua kali wasiolipa kodi. “Sisi wafanyabiashara wadogo tunasulubiwa na mamlaka, ikiwa hutalipa wanakuja na makufuli,” anasema Marta.

Je, unajua mbinu nne kuu zinazotumiwa na Kampuni ya SABmiller inayomiliki TBL kukwepa kodi hapa nchini na nje ya nchi? Usikose JAMHURI wiki ijayo upate mwendelezo.

3454 Total Views 1 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!