SAM_0603Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeingia katika kashfa nyingine baada ya kudaiwa kufanya makato makubwa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi yasiyojulikana yanapelekwa wapi.

Edrick Katano ni miongoni mwa wafanyakazi wengi waliokatwa makato yasiyo na maelezo. Kabla ya kuacha kazi kwa hiyari Desemba 31, 2013, anadai TPA imempunja mishahara, posho za kujikimu safarini, saa za ziada, posho ya nyumba na michango ya PPF.

Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali ambazo JAMHURI imeziona, Katano alianza kukatwa mshahara baada ya kuhamishwa ofisi. Alianza kazi Februari 5, 1989.

Anayo barua ya Juni 18, 2015 yenye Kumb. Na. CB 364/452/01/PART/28 inayohusu kupunjwa kwa mishahara.

Pia barua ya Mkurugenzi wa Utumishi wa TPA ya Aprili 23, 2013, yenye Kumb. S/HR/92965 na barua ya TPA ya Septemba 30, 2014 yenye Kumb. Na. S/HR/92965, nayo inahusu somo hilo.

Meneja Rasilimali Watu (HR) wa Bandari, Vitalis Kapinga, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa si msemaji, akimtaka mwandishi awasiliane na Mkurugenzi, Peter Gawile, ambaye kwa sasa amehamishiwa wizarani.

Gawile anasema alisaini barua zilizokwenda kwa Katano kama Mkurugenzi Rasilimali Watu na si mtu binafsi.

“Nakushauri uende TPA ndiyo wenye kumbukumbu sahihi tafadhali,” anasema Gawile ambaye aling’aka kuhojiwa juu ya kusaini barua zenye utata wa uamuzi dhidi ya Katano.

Madai ya Katano ambayo pia yapo kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), yanahusu kupunjwa mishahara, posho za kujikimu safarini, saa za ziada, posho ya nyumba na michango ya Mfuko wa Pensheni (PPF).

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Aprili 5, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kati ya saa 4.00 asubuhi na saa 6.00 mchana Machi 21, mwaka huu.

Kesi hiyo ilishindikana kutokana na mawakili wa Bandari kudai kutopata amri ya CMA iliyoagiza Mamlaka hiyo ipeleke nyaraka mbalimbali zilizohitajika kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo na kutokuwapo msuluhishi ofisini.

Katano anasema: “Sijakata tamaa, kesi yangu ipo CMA, lakini sijachoka kufuatilia haki zangu kwa viongozi wa Serikali.”

Katano anasema mbali ya suala hilo kuendelea CMA katika mazingira ambayo yanamuumiza kwa sababu linachukua muda mrefu wakati aliishaondoka kazini, pia alilifikisha Wizara ya Uchukuzi.

“Nimefika mpaka kwa Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shabaan Mwijaka (wakati ule), lakini hakunielewa. Kwa sasa namtafuta Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, nimwambie mambo ya ovyo ya Bandari.

“Hii yote ni kwamba sikubaliani na TPA na ndiyo maana nahangaika kutaka kumuona Prof. Mbarawa nimpe pia malalamiko yangu,” anasema Katano.

Katano anatoa wito kwa uongozi wa Wizara chini ya Mbarawa kuingilia kati na kuwaamuru TPA kufanya mchanganuo halisi na kumlipa mapunjo yote kwa thamani ya pesa ya sasa au kwa riba inayozaa kila mwaka kwa miaka yote mpaka tarehe ya kumlipa malimbikizo yote kwa ukamilifu.

Anasema aliajiriwa kama mfanyakazi wa mikono (Labourer) katika idara ya uhandisi.

Mei 15, 1993 kwa mujibu wa Katano na nyaraka zake, alipandishwa cheo na kuwa Mechanical Equipment Operator 1 (MEO 1).

Ikatokea mmoja wa madereva wa makao makuu wa TPA wakati huo THA, alikwenda likizo na yeye akaombwa akashike moja ya magari ya wakurugenzi.

“Nilifanya hivyo kwa sababu ya utii kazini,” anasema Katano na kuongeza: “Hapo ndipo palipoibuka mgogoro.”

Kwa kuwa alikwenda huko Desemba 27, 1993 alishushwa cheo na kuwa dereva wa kawaida (Staff Car Driver), kutoka kuwa MEO1.

“Sikuridhika na kitendo hicho cha kushushwa mshahara bila sababu yoyote, kitu ambacho ni kinyume cha sheria na taratibu za kazi, lakini pia kwanini unishushe cheo?” anahoji Katano.

Anasema hatua alizochukua ni kufuata taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandika barua kulalamikia kitendo hicho.

Ilipofika Juni 7, 1995, Meneja wa Bandari alimwandikia Mkurugenzi wa Utumishi barua yenye kumb Na. DPE/ETK/92965 na kumfahamisha kuwa uhamisho hauwezi kuwa sababu ya kushusha cheo na mshahara wa mfanyakazi.

Julai 21, 1995 Katibu na Mwanasheria wa Bandari naye aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Utumishi barua yenye kumb. Na. SL/1/2/38 na kusisitiza alipwe kwa kadiri ya stahili yake ili atulie na kuchapa kazi.

Katano anasema pamoja na ushauri wa Meneja wa Bandari na Mwanasheria wa Bandari uliotolewa Julai, 1995, hakulipwa chochote kwa zaidi ya miaka 15 hadi mwaka 2008 uongozi wa Bandari ulipoamua kumlipa kiasi cha Sh 6,056,287/59 kama tofauti ya mshahara, saa za ziada na posho ya nyumba.

Pia walimlipa Sh 710,000 kama tofauti ya posho ya kujikimu na usafiri kwa safari za kikazi.

“Lakini, uongozi wa Bandari hauelezi popote pale ni kwanini walipogundua kosa walilolifanya na waliposhauriwa kunilipa mshahara wangu wa kawaida tangu 1995 hawakunilipa hadi 2008?

“Kunilipa mwaka 2008 kiasi cha pesa kile kile walichopaswa kunilipa 1993 ni kuniadhibu bila makosa ambayo siyo yangu bali ni uzembe wao wenyewe!” anasema.

Kutokana na hatua hiyo, Katano anasema: “Sikukubaliana na mpaka sasa sikubaliani na kiasi nilicholipwa kwa sababu zisizopungua 10.

“Kwanza, kuhusiana na malipo ya saa za ziada (overtime): Kinyume na kilichosemwa kwenye barua ya Bandari ya Aprili 23, 2013 kwamba nimewahi kulipwa stahili hiyo.

“Sikuwahi kulipwa tofauti ya malipo kwa saa za ziada nilizofanya kazi kuanzia mwaka 1993 hadi 2008. Ukiangalia (anaonesha nyaraka ya ukokotoaji uliofanywa na Wahasibu wa Bandari) namna walivyokokotoa malipo ya mapunjo,” anasema.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo na maelezo ya Katano ni kwamba hakuna hata sehemu moja wanapoonesha kuwa tofauti ya malipo ya saa za ziada zilikokotolewa.

“Ndugu mwandishi, kumbuka kuwa kwa kushushwa ngazi ya mshahara, malipo yangu ya masaa ya ziada (saa za ziada) nayo yalishushwa na hilo halibishaniwi,” anasema.

Akifafanua kuhusu malipo ya PPF, Katano anasema licha ya kupunjwa malipo yake ya PPF kwa muda wa miaka 15, vilevile ni dhihaka kuwa mwajiri wake hakuwasilisha fedha yoyote kuanzia Februari 1989 hadi Agosti 1994.

Katano anazungumzia miezi 67 mfululizo tangu alipoajiriwa. Nyaraka za PPF zinaonesha mwajiri ambaye ni TPA hakupeleka chochote kwenye akaunti yake ya PPF.

Kadhalika, Katano anashangazwa kulipa fedha Sh 710,000 ikiwa ni malikimbizo ya posho ya kujikimu na usafiri kwa safari za kikazi.

“Ina maana ni kama nimelipwa posho ya siku 20 tu katika miaka 15. Ukweli ni kwamba mimi nimesafiri kikazi kwa zaidi ya siku 600 kwa makadirio ya chini. Hii ni kwa sababu nilikuwa dereva wa wakurugenzi na kwa hiyo nimesafiri kwa safari zote za mabosi wangu.

“Nimesafiri kwenye misiba mbalimbali iliyohusiana na wakurugenzi hapo bandarini kwa mfano, Bwana Mandali (Mkurugenzi wa Fedha) alipofiwa na mke wake (siku 7 Moshi). Pia alipofiwa na mama yake (siku 7 Moshi). Kadhalika alipofiwa na mdogo wake (siku 7 Moshi),” anasema.

Anafafanua zaidi akisema, kadhalika Kepteni Kwayu aliyekuwa Mkurugenzi wa Utekelezaji alipofiwa na mama yake. Safari ambayo pia ilichukua siku saba kama ilivyotokea tena alipofiwa baba yake pia mdogo wake, shemeji yake na kadhalika.

“Kaka nimesafiri kwa safari zote za michezo kama mwanamichezo mahiri wa Bandari. Nimesafiri kwa operesheni mbalimbali mikoani nikiambatana na bosi wangu.

“Nimeenda semina za kikazi mara mbili na kila semina moja kwa siku 14. Hivyo semina mbili ni siku 28…

“Nimekuwa mfanyakazi bora mara mbili na kila unapokuwa mfanyakazi bora unapelekwa mbugani kwa siku 7. Hivyo nimeenda mbugani kwa siku 14,” anasema.

Anasema alihamishiwa Kigoma na kupewa siku 14 za kukaa hotelini na kutafuta nyumba, hivyo posho ya kujikimu ya siku 14 kwa watu 6 wa familia yake nayo ilikuwa na mapunjo.

Anasimulia maisha ya Kigoma kwamba baada ya kupata nyumba alisafiri siku saba kufuata mizigo yake Dar es Salaam.

“Mapunjo ya mishahara na posho ya nyumba, nililipwa kiasi cha Sh 6,056,287 ingawa kwenye akaunti nilipewa Sh milioni nne (Sh 4,000,000 tu) kama tofauti ya mishahara, saa za ziada na posho ya nyumba kwa mchanganuo waliokokotoa TPA.

“Nasikitika kuona kuwa walinilipa kwa pesa ileile ambayo ningelipwa mwaka 1993 au 1994 na kuendelea. Mapendekezo yangu ni kuwa ili kufanya malipo yawe ya haki ninaomba nilipwe kwa thamani ya pesa ya sasa au malipo yafanyike pamoja na riba inayozaa (Compound Interest) ya asilimia 20 kwa kila mwaka kwa miaka yote 22 mpaka sasa  au  mpaka hapo malipo hayo yatakapofanyika kwa ukamilifu,” anasema.

Anasema deni lote likijumlishwa kwa wakati ule alipostaafu kwa hiyari angelipwa karibu Sh milioni 65, ila kwa sasa hilo likilipwa kwa utaratibu wa riba ya asilimia 20 kwa miaka 22, atapata fedha nyingi zaidi. Anaomba Serikali imsaidie kupata haki yake.

2953 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!