Mwanamke pekee msaidizi wa waziri

Ni asubuhi na mapema siku ya Jumatano napata wazo la kuonana na Msaidizi wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Teodensia Mbunda.

Sababu ya kutaka kuonana na mwanamke huyo ni baada ya kupata habari kuwa ndiye mwanamke pekee aliye msaidizi wa waziri katika Baraza la Mawaziri kwa zaidi ya miaka saba.

 

Nashawishika kujua ni kwanini awe mmoja katika sekta hiyo na si wengi kama ilivyo katika sekta au idara nyingine za Serikali, je, ina maana wanawake hawezi kufanya kazi hiyo?

 

Napiga moyo konde natafuta namba yake, naipata kutoka kwa rafiki yake wa karibu. Nampigia na tunapanga siku ya kuonana, tunakubaliana iwe baada ya kwisha kwa mkutano wa 10 wa kikao cha 12 cha Bunge kwa kuwa alikuwa Dodoma kuhudhuria mkutano huo.

 

Siku inafika tuliyokubaliana, nafika Ofisi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Hapo nakutana na watu wengi tena wa kawaida, wengi wao ni wale walio na kipato cha chini kabisa – wanawake kwa watoto ndiyo wengi – wakisubiri kumuona waziri ili kutoa shida mbalimbali zinazowakabili.

 

Haraka haraka natambua wizara hii ni mtambuka ni wizara kiunganishi cha jamii na Serikali. Kosa moja litakalofanywa na wizara hii ni sawa na kuliangamiza Taifa la kesho kwani ndiyo inayoshughulika na maendeleo ya jamii.

 

Pia ndiyo inayoshughulikia na matatizo ya kawaida ya jamii, hususan watoto wa mitaani, watu wenye shida mbalimbali za kifamilia, wagonjwa na mambo mengine ya kijamii.

 

Katika ofisi anatokea mama wa makamo na kuniuliza shida yangu, nami bila ajizi najieleza na kujibiwa kuwa nisubiri kwa kuwa mhusika ninayemtafuta yuko kwa waziri.

 

Mara mlango wa Ofisi ya Waziri Sophia Simba unafunguliwa, anatoka mwanamke mwenye umbo la wastani, kwa akili ya haraka haraka, natambua kuwa ndiye mhusika ninayemtafuta.  Namfuata na kujitambulisha kwake naye ananipokea kwa furaha tunaingia ofisini baada ya utambulisho huo na tunaanza mahojiano.

 

Mbunda ni mwanamke mcheshi, mchangamfu na, mwenye huruma kwa wageni wake, anaanza kunieleza kazi katika majukumu yake kama msadizi wa waziri.

Anasema kuwa unapozungumzia ufanisi mzuri katika wizara yoyote, basi utakuwa hujatenda haki kama usipomtaja katibu wa waziri.

 

Anasema kazi ya katibu wa waziri ni kuwa kiungo kati ya wizara na viongozi wa idara mbalimbali za wizara wakiwamo Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu, wakurugenzi na watu wanaotaka kumuona waziri.

 

Ameitaja kazi nyingine kuwa ni kumshauri waziri katika mambo mbalimbali ya kisheria na utekelezaji wa mambo yaliyopangwa na wizara.

 

“Unajua kuwa nafasi ya uwaziri ni nafasi ya kisiasa, si kila kitu waziri anajua kuhusu sera na sheria, hivyo mimi kazi yangu ni kuhakikisha kuwa namshauri  waziri kuhusu hilo. Kuna kazi na sera zinazotakiwa kutekelezwa na pia kumkumbusha waziri mambo mbalimbali muhimu yahusuyo wizara,” amesema.

 

Amesema kazi nyingine ni kupanga na kuratibu ratiba ya waziri pia kuchukua maelezo ya wageni katika vikao vinavyofanywa na waziri, wageni wote wanaingia katika ofisi ya wizara kwa nia ya kumuona waziri, nayo pia ni miongoni mwa kazi zake kupanga jinsi ya mtu anavyoweza kumuona waziri au kiongozi mwingine hapo wizarani.

 

Anaitaja kazi nyingine kuwa ni kukusanya majibu yanayoulizwa na wabunge kutoka katika mashirika na idara mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali.

 

“Kazi nyingine ni kusikiliza shida za wageni wote bila kujali ukwasi wao, mfano hapa katika wizara yetu kuna wageni wengi kama unavyoona, kuna watoto wa mitaani, kuna wanawake, wote wanakuja hapa tunawasikiliza na kuwasaidia, kuna wakati inakubidi kutoa fedha yako mfukoni kwa ajili ya kuwasaidia.

 

“Nakumbuka mwaka jana kuna mama alikuja hapa akiwa anaugua ugonjwa wa saratani ukimuona unaogopa, akaniambia kuwa alifikia kwa ndugu zake Mabibo.

 

“Nia yake ni kupata msaada wa nauli ili arudi kwao Shinyanga kwa kuwa alipofikia sasa wameanza kumtenga. Kwa kuwa wizara haina bajeti kwa ajili ya watu hao ilinilazimu kutoa fedha yangu mfukoni ili aondoke, nikampa shilingi laki moja,” amesema.

 

Amesema kuwa watu wanaofika hapo wanaanzia kwake na kuelezea shida zao na yeye hupima uzito wa shida hizo na kutoa uamuzi.

 

Aliipataje kazi hiyo

Mbunda anasema alipata kazi hiyo baada katibu aliyekuwa anafanya kazi hiyo kuhamishiwa katika idara nyingine, hivyo waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, Sophia Simba, alimwomba amsaidie kufanya kazi hiyo.

 

Amesema kuwa kwa mara ya kwanza alikwenda na Waziri Simba katika mkutano wa nchi za Afrika uliohusu ukatili wa mtoto wa kike na kufanyika, Addis Ababa, Ethiopia.

 

Anasema baada ya kurudi kutoka katika mkutano huo aliandika taarifa iliyompendeza  Simba, hivyo alimwomba aendelee kufanya kazi hiyo.  Aliendelea kufanya kazi na  Simba kwa muda mrefu na hatimaye alimtaka aandike barua ili kuomba kujaza nafasi hiyo.

 

“Aliniomba niandike barua ili kujaza nafasi ya kazi hiyo, nilifanya hivyo na nikaidhinishwa rasmi kuwa msaidizi wa waziri. Tangu siku hiyo nimekuwa msaidizi wa Simba na tumekuwa tunahama naye.

 

“Nilihama naye Ikulu nikakaa naye miaka mitatu na sasa niko naye hapa watu wanashangaa kuona tunavyofanya kazi,” amesema Mbunda.

 

Majukumu ya Wizara

Amesema majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto  ni kuandaa sera za wizara, kuzisimamia, kuziratibu na kutathmini utekelezaji wake.

 

Kueneza na kuendeleza dhana ya maendeleo ya jamii kwa kuwashirikisha wananchi wote, kutayarisha mikakati na mifumo ya utekelezaji ili kuchochea maendeleo ya jamii.

 

Kuwajengea uwezo wanawake na wanaume ili waweze kushiriki katika ngazi zote za utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo na kufaidika sawa katika maendeleo hayo.

 

Amesema majukumu mengine ni kuendeleza, kuhamasisha na kuwezesha jamii, kuwapatia watoto haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kutobaguliwa na kushiriki katika maendeleo ya Taifa, pia kuratibu shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali na kuyawezesha kufanya kazi kwa uwazi na ufanisi zaidi.

 

Kusimamia utendaji kazi wizarani kwa misingi ya uadilifu, haki na utawala bora na kusimamia utoaji wa mafunzo ya taaluma ya Maendeleo ya Jamii katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na mafunzo ya maarifa, ujuzi na stadi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

 

Anayataja majukumu mengine kuwa kusimamia na kutekeleza majukumu hayo, wizara inaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II) na Malengo ya Milenia.

 

Mbunda amesema kuwa kutokana na utekelezaji wa majukumu hayo, wizara imefanikisha kupunguza ndoa za utotoni kwa kiasi kikubwa, ukatili wa mtoto wa kike nao umepungua kwa kiasi kikubwa.

 

Matatizo

Mbunda amesema kila kazi ina ugumu wake, lakini kazi hiyo ni ngumu kuliko kazi nyingine.  Ugumu wa kazi hiyo ni kuwa inamhusisha mtu na mtu na si mtu na taasisi au idara.

 

“Unajua kuwa mimi nashughulika na mtu si idara au sekta Fulani, kama ukiwa na dawati lako unaweza kusema nimefunga kazi nitafanya kesho, huo ndiyo ugumu.

 

“Lakini msaidizi wa waziri unashughulika na waziri, yeye ndiyo mwenye ratiba yako, akiondoka na wewe ndiyo muda wa kuondoka tofauti kama ungekuwa mkuu wa kitengo au idara fulani, uvumilivu ni kitu cha muhimu unapofanya kazi na mkuu wako ambaye ni waziri,” amesema.

Amsema tatizo jingine ni lawama kutoka kwa wafanyakazi wenzake.

 

“Kuna lawama nyingi, kwa mfano, ikionekana kuwa kuna tatizo katika wizara na tatizo hilo linafanywa kuwa siri, ili waziri asijue lakini baada ya muda akajua basi wafanyakazi wote wa wizara wataelekeza macho yote kwako kuwa ndiyo uliyemwambia. Hilo ni tatizo kwetu sisi makatibu wa mawaziri,” amesema Mbunda.

 

Mbunda amevipongeza vyombo vya habari kwa kuibua matatizo ya Watanzania, hali inayoifanya wizara hiyo kufanya kazi kwa urahisi. Amesema si kazi rahisi kwa wizara hiyo kuwafikia watu wote kwa wakati mmoja, lakini vyombo vya habari vimefanya kazi nzuri.

 

“Sasa ona kama hapa kuna habari inayoeleza mtoto wa miaka saba kuwalea watoto wenzake, nimeisoma habari hii na kufuatilia lakini tumebaini watoto hawa wana baba yao lakini anashikiliwa kwa kosa la kujifanya mwanasheria. Alipofikishwa mahakamani kwa ajili ya kumtetea mshtakiwa alishindwa kujieleza hivyo hakimu alimwamuru kuwekwa ndani.

 

“Hivyo yuko ndani na kawaacha watoto wakiwa hawana mbele wala nyuma, tumewasiliana na ndugu zao na kupata ufumbuzi, hii kama si vyombo vya habari nani angejua haya?” amesema Mbunda.

 

Mbunda anatoa wito kwa mawaziri wengine kuiga mfano wa Waziri Sophia Simba kwa kuajiri wasaidizi wanawake, ili kuondoa dhana iliyojengeka kuwa wanawake wakifanya kazi pamoja maendeleo huwa duni.

 

“Kuna dhana imejengeka miongoni mwa wanawake wenzangu kuwa wanawake wakifanya kazi pamoja, maendeleo huwa duni kutokana na kutopendana, lakini sisi hakuna hilo, tumekaa kwa miaka zaidi ya saba, tunapendana na kazi zetu zinafanyika vizuri mno,” anamalizia Mbunda.

By Jamhuri