Katika toleo lililopita la Septemba 24-30, 2013 kwenye ukurasa huu, kulikuwa na barua iliyoeleza ufisadi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

 

Barua hiyo ilikwenda mbali zaidi na kuigusa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kumlenga Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa TANAPA, Pascal Shelutete.

 

Miongoni mwa madai potofu yaliyotolewa ni juu ya utajiri wake na sifa za elimu zinazomuwezesha kushika wadhifa huo.

 

Tumeweza kufuatilia kwa kina taarifa hizo na kubaini kuwa ukwasi alionao Shelutete ni halali na unaotokana na nafasi yake. Madai kwamba Shelutete ana nyumba katika kila mkoa, ni ya uzushi. Tanzania ina jumla ya mikoa 30. Mikoa 25 ipo Tanzania Bara na mikoa mitano ipo Zanzibar. Tumejiridhisha kuwa taarifa hiyo ililenga kumpaka matope yeye binafsi na kutia doa uadilifu wake.

 

Kuhusu elimu, tumejiridhisha pasi na shaka kuwa Shelutete ni miongoni mwa wasomi wenye sifa stahiki wanazopaswa kuwa nazo watu wa cheo cha aina yake. Pamoja na kuwa na elimu ya juu, Shelutete amekuwa akijiendeleza kwa masomo ya aina mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya nchi, akiamini kuwa elimu haina mwisho.

 

Kwa yote hayo, tunachukua fursa hii kumpa pole yeye binafsi, familia, ndugu, jamaa na marafiki zake ambao wamekwazwa na habari hiyo. Tunamwomba radhi kwa usumbufu alioupata.

 

Kwa taarifa hii, tunatamka kuwa barua iliyochapishwa katika ukurasa huu kwenye toleo lililotangulia, imetenguliwa rasmi.

 

Mhariri

 

By Jamhuri