Malinzi 1Wiki iliyopita, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania

(TFF), ilitangaza kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (KIFA) kwa kile wanachosema kuwa haukufuata utaratibu.

Kamati hiyo ya TFF, iliyo chini ya Mwenyekiti Wakili Revocatus Kuul ilifikia hatua hiyo baada ya kugundua kuwa uchaguzi huo uligubikwa na madudu mengi.

KIFA ilifanya uchaguzi wa marudio wiki mbili zilizopita katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi Oysterbay, Dar es Salaam na kupata viongozi wapya, ambao ni Mwenyekiti Michael Lupiana, Makamu Mwenyekiti wa Kwanza; Salum Mwaking’ida, Hamisi Jendaheka, Makamu Mwenyekiti wa pili; Katibu Mkuu, Funua Funua.

Riziki Shao alichaguliwa kuwa Mjumbe Mwakilishi wa Klabu, Mjumbe Mwakilishi wa Mkoa, Siri Gongo, huku nafasi ya Mweka Hazina ikikosa kiongozi kutokana na Khalid Kamguna aliyewania peke yake kutopata kura za kutosha.

Lakini uamuzi huu unashtusha na kushindwa kabisa kueleweka kwanini TFF inasigina katiba yake wazi wazi hivi!

Ukiangalia, KIFA si mwanachama wa TFF bali ni mwanachama wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), sasa wanapata wapi kiburi cha kuingilia uchaguzi huo?

Ni dhahiri uamuzi uliofanywa na TFF wa kufuta matokeo halali ya uchaguzi wa KIFA uliofanyika Juni 12, mwaka huu kama una maslahi kwa baadhi ya viongozi.

Haiwezekani kabisa na haiingii akilini kwa TFF ambao ni baba wa soka la hapa Tanzania, kuingilia uchaguzi uliofanyika huru na haki na wanachama wenyewe wameridhika.

Kwa hili, TFF imevunja katiba yake, ya DRFA na KIFA pamoja na kanuni zake ambazo ndiyo mwongozo wa mpira wetu hasa katika upatikanaji wa mamlaka za uendeshaji wa soka kwenye ngazi mbalimbali za Taifa, mkoa na wilaya.

Katiba ya TFF ibara ya 52(2) na ibara ya 52(6) (a) zinaeleza wazi kazi na majukumu ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kusimamia uchaguzi wa TFF na wanachama wake ambao ni vyama vya mikoa, klabu za Ligi Kuu, Bodi ya Ligi pamoja na kuishauri Kamati ya Utendaji.

Lakini pia, kwa mujibu wa katiba hiyo ya TFF ya 2013, Kamati yake ya Uchaguzi haiwajibiki na lolote kwa vyama vya soka vya wilaya ambao si wanachama wa TFF.

Ukiangalia pia, ibara ya 3(i) ya kanuni za uchaguzi wa TFF za 2013,

inaeleza kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF itaendesha na kusimamia uchaguzi wa TFF na Bodi ya Ligi.

Wakati huo huo, ibara ya 6 ya kanuni za uchaguzi za TFF za 2013,

inaeleza majukumu ya kamati ya uchaguzi na katika majukumu yake hakuna sehemu yoyote inayoeleza mamlaka ya kusimamia na kutolea uamuzi wa chaguzi za vyama vya soka vya wilaya ambavyo si wanachama wa TFF.

Lakini ukiangalia Katiba ya KIFA ibara ya 47 ya kanuni za uchaguzi

kipengele (b), inasema Kamati ya Uchaguzi ya KIFA itafanya kazi kwa kushirikiana na sekretariati ya chama ikiwa chini ya uangalizi na miongozo ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA.

Kwa hiyo, hapa wenye jukumu ni kamati ya uchaguzi ya DRFA kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na kama utavurundwa wao (DRFA) walipaswa kuufuta ama la!

Lakini pia, Katiba hiyo KIFA katika kanuni zake za uchaguzi 5 (h)

inaeleza kuwa rufaa zote zinazohusu uchaguzi zitawasilishwa kwenye Kamati ya Rufaa ya Wilaya na kama mrufani hakuridhika atapeleka malalamiko yake Kamati ya Rufaa ya Mkoa ambao uamuzi wake utakuwa ndiyo wa mwsho.

Kwa hiyo, uporaji huu wa madaraka ya mwanachama wa TFF ni hatari, batili na kinyume na utaratibu tuliojiwekea na ni hatari katika uhai wa tasnia hii ya mpira wa miguu.

Inauma kuona TFF iwe chanzo cha kutibua na kuingiza migongano ndani ya vyama vya michezo ama klabu wakati wao ndiyo wasimamizi wakuu katika soka hapa Tanzania.

Haipendezi; mkubwa kusemwa kila siku, inaonekana TFF wanafanya hivi labda kuna maslahi ya watu binafsi kiasi cha kuanza kutibua hali ya hewa kwa wanachama wake ama hata visivyowahusu kama KIFA.

Ikumbukwe, TFF walitaka kuharibu hali ya hewa katika uchaguzi wa Yanga na wameendelea kuukoroga uchaguzi wa Stand United waliotakiwa kufanya Jumapili iliyopita.

Lakini waliutibua uchaguzi wa Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (TEFA) wakati wala hauwahusu kutokana na wao si wanachama wake.

Kilichobaki ni kujitafakari kwa TFF, licha waliopo madarakani wanataka viongozi wao ili waweze kujitengezea ngome kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo

1218 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!