Karibu kila mdau wa michezo ninayezungumza naye kuhusu mustakabali wa maendeleo ya tasnia hiyo hapa Tanzania, anagusa uwekezaji kwa vijana. Nilivutwa na kuamini katika uwekezaji wa soka la vijana, baada ya serikali kumwajiri kocha wa timu ya Taifa, kutoka Brazil, Marcio Maximo.

Mbarazil huyo alifufua matumaini ya uwekezaji huo kutokana na sera yake ya kuamini katika soka la vijana, sawa na Mromania, Profesa Victor Stanslecu, aliyewahi kuinoa Yanga miaka ya ‘70 kabla ya kuondoka na kumwachia mikoba Tambwe Leya. Angalau Kim Polsen amezinduka katufumbua macho kuwa ni muumini wa soka la vijana ambao wanatamba leo kwenye vilabu.

 

Wakati Maximo akinoa Stars, alipenda kuwapa nafasi vijana kama makinda Jerry Tegete, Erasto Nyoni, Kiggi Makasi, Juma Jabu na wengineo. Ni kipindi hicho mashindano ya Copa Coca Cola yanayowahusisha vijana wenye umri chini ya miaka 17 yalipoanzishwa kwa lengo la kuibua vipaji vya soka na kuviendeleza. Baadaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaanzisha mashindano mengine ya vijana wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kuwania Kombe la Uhai (Uhai Cup).

 

Mpango wa uwekezaji huo unatia kichefuchefu huku miaka ikizidi kuyoyoma, tunaimba kila siku kwamba tunataka kuinua soka letu kwa kuwekeza kwenye soka la vijana wadogo. Akatika michuano ya kwanza ya Copa Coca Cola, wapo vijana walioibuliwa na kocha Marcus Tinoco, wakasafiri kwenda Brazil kushiriki mashindano wakarejea na kombe. Safari yao kisoka ikaishia hapo na hata kitalu cha michezo cha TSA cha TFF nacho kimekufa kifo cha aina yake.

 

Hivi leo ukiwauliza TFF wale vijana wa timu iliyokwenda Brazil wako wapi wataeleza nini, au vijana waliokuwa kituo cha TSA chini ya Rogasian Kaijage wako wapi? Dhamira ya uwekezaji soka la vijana iko wapi kama tunahitaji maendeleo ya mpira wa miguu? Pamoja na kuendesha michuano hiyo kila mwaka, vipaji vingi vinaonekana lakini mwisho wa siku vijana hao vipaji vyao vinapelekwa wapi ili waje kuwa wachezaji bora wa kutegemewa na Taifa?

 

TFF pamoja na kuzitaka timu za Ligi Kuu kuwa na timu za vijana, hakuna uratibu wa kueleweka wala ufuatiliaji kama timu hizo kweli zinamilikiwa na vilabu hivyo. Nasema hivyo kwa sababu haiwezekani timu za vijana wadogo zishindwe kucheza mechi za utangulizi badala yake zicheze ligi ya pekee yao. Kwangu mimi TFF bado haina dhamira ya dhati ya kuwekeza kwenye soka la vijana kwa sababu suala la udhamini liko ndani ya uwezo wake, tatizo ni mikataba wanayoingia na wadhamini hailengi uwekezaji wa soka la vijana.

 

Hili la uwekezaji soka la vijana hata vilabu vyetu vina ugonjwa huo, viko radhi kusajili mchezaji wa kigeni kwa Sh milioni 30 anayelipwa mshahara wa Sh milioni 1.5.  Yanga wana wachezaji watano, Simba pia wanao kadhaa. Timu hizi zinatumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni. Fedha hizo zingeweza kutumika kukusanya vijana wadogo wenye vipaji, kuwalea na baadaye kuwauza nje ya nchi wenye uwezo mkubwa zaidi na wengine kubaki kucheza vilabu vya hapa nyumbani.

 

Hao wachezaji ambao vilabu vyetu vinawalilia na kuwasajili kwa fedha nyingi walilelewa huko kwao kwa mtindo pengine tofauti na wetu, na leo ni lulu. Kwa sababu sisi ni wavivu wa kulima tunataka kuvuna bila kupanda, ndiyo maana tuko radhi tununue kuliko kulea chetu. Miaka ya ‘80 hatukupishana sana viwango vya uchezaji na nchi kama Ivory Coast, Togo, Nigeria, Guinea na nyinginezo za Afrika Magharibi. Senegal tuliwaacha nyuma lakini Senegal walikaa chini wakakubali matokeo, wakawekeza kwa vijana, waliporudi wakafuzu kucheza Kombe la Dunia. Leo wametuacha mbali.

 

Tanzania tulikuwa nchi ya kwanza kutoka Afrika Mashariki kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1980. Tukiiondoa Zambia iliyokuwa ikihitaji nafasi hiyo kwenye uwanja wa Uhuru mjini Lusaka, Zambia. Leo tumeshindwa kufanya hivyo kwa sababu tumeuzika mfumo wetu baada ya kushindwa kuwekeza kwenye soka la vijana.  Nchi nyingi zenye mafanikio ya soka zimepitia kwenye mfumo huu wa kukuza soka la vijana ikiwa ni pamoja na ufuatilaji wa karibu. Asec Mimosas ya Ivory Coast na Asante Kotoko ya Ghana ni mifano hai ya vilabu vyenye mafanikio kutokana na uwekezaji wa soka la vijana.

 

Soka la vijana duniani kokote ndiyo msingi wa timu kubwa na mataifa yaliyoendelea kisoka kwa timu zao za taifa. Hivyo ili tufanikiwe lazima tukubali kubeba mzigo huo kwa sababu mafanikio hayahitaji muda mfupi wa uwekezaji kwenye eneo husika. Kazi ya TFF iwe ni kusaka wadhamini na vilabu vyenyewe kwa upande mwingine. Leo tunalalamika hatuna wafungaji ama vioungo kama wachezaji wa kigeni waliopo hapa nchini kwa sasa, Kiptre Tchetche, Emannuel Okwi, Hamis Kiiza, Didier Kavumbangu na Haruna Niyonzima, wanakubalika kwao kutokana na kazi wanayofanya Tanzania na jinsi tunavyoamini wageni hao zaidi ya wachezaji wetu wazawa.

 

Enzi za miaka ya ‘70 hadi ‘80 nani asiyefahamu uwezo wa vikosi vya pili vya Yanga na Simba. Nani amewaloga kuamini kuwa hatuna vijana wenye vipaji na uwezo wa kucheza soka.

Sunday Manara na Kassim Manara ni Watanzania wa kwanza kucheza soka la kulipwa Ulaya (Australia ) ukanda wa Afrika Mashariki, ukiachilia mbali Eusabio.

 

Kimsingi tunapaswa kuzingatia uwekezaji wa kukuza soka la vijana, vinginevyo baada ya miaka kadhaa tutakuwa na ligi ya wageni na tutakuwa tumewazika wachezaji wazawa baada ya kushindwa kuzalisha na kulea wabadala wao.

Ndiyo maana nasema TFF, Simba na Yanga, ni vinara wa kuua soka la Tanzania. Wameshindwa kuwekeza kwenye soka la vijana ambao watachukua nafasi za akina Simon Msuva, Mrisho Ngassa, John Bocco, Juma Kaseja, Amir Maftaha, Kelvin Yondan, Salum Abubakar, Simon Msuva, Christopher Edward, Ramadhan Singano, Frank Domayo, Haruna Moshi na Shaaban Nditi.

mashakabar@yahoo.com


1135 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!