*Ni kisima cha maji kilichogharimu Sh mil 50
*Tajiri anataka apewe Sh mil 22 kukinusuru
Wakati Watanzania wengi wakikosa maji safi na salama, mradi wa kisima cha maji eneo la Mpeta katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, uliofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), uko hatarini kutoweka.
Mradi huo ambao ujenzi wake uligharimu Sh milioni 50 zilizotolewa na WB, hivi sasa unasongwa na ujenzi wa makazi ya watu yanayotishia uhai wake.
Wadau mbalimbali wanaamini kuwa vyoo vitakavyochimbwa katika makazi hayo, vitaingiliana na maji ya kisima hicho na hivyo kuhatarisha afya za watu zaidi ya 4,000 wanatumia maji yake.
Hivi karibuni, JAMHURI imetembelea eneo la mradi wa kisima hicho na kuzungumza na wakazi kadhaa wa Mpeta, ambapo wamelalamikia ujenzi wa makazi hayo wakisema ni dalili za kuutokomeza mradi huo.
Mwenyekiti wa Mradi wa Maji Mpeta, Ephraim Mtafya, anahofu kuwa ujenzi wa makazi ya watu kuusonga mradi huo, utaathiri moja kwa moja maji ya kisima hicho.
“Makazi yanajengwa karibu sana na mradi huu, ni wazi kuwa vyoo vitakavyojengwa vitaingiliana na maji ya kisima hiki, na huo utakuwa ndiyo mwisho wa mradi huu, maana watu wakilazimisha kutumia maji yake wataathirika afya.
“Tumeandika barua kulalamikia hatua hii, imepitia kwa uongozi wa Mtaa wa Sigara na Kata ya Yombo Vituka kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, lakini hatujajibiwa,” anasema Mtafya.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Issa Makangila, naye amelalamikia hatua ya ujenzi wa makazi hayo akisema, “Ni bora mtu mmoja au wawili [wanaojenga makazi hayo] wazuiwe kunusuru kisima hiki kinachotegemewa na maelfu ya wananchi.”
Kwa upande wake, Sauda Abdallah anasema kabla ya ujenzi wa mradi huo mwaka 2000, wakazi wa eneo hilo walilazimika kwenda kukinga maji kwenye kuta za mlima, ambayo yaliwasababisha baadhi ya watumiaji kuugua homa za matumbo na kuhara kwani hayakuwa salama.
“Tunaomba Serikali iingilie kati kwa kuzuia ujenzi wa makazi haya kwa sababu vyoo vitakavyochimbwa vitaathiri kisima hiki,” anasema Sauda.
Asha Kasim naye anasisitiza kuwa mradi wa kisima hicho ukitoweka, wakazi wa Kata ya Yombo Vituka watakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama, na hivyo, kurudia adha ya kusaka huduma hiyo kwenye kuta za mlima.
Mwanaharusi Athumani anasema, “Mradi huu [kisima] ukifa na sisi tutakufa maana tumeuzoea na unatusaidia sana.”
Katibu wa mradi wa kisima hicho, Jeremiah Mbembela, ameeleza kushangazwa na mtu aliyekwenda eneo hilo akijitambulisha kuwa ni Mhandisi wa Manispaa ya Temeke na kutoa kauli ya kubariki ujenzi wa makazi ya watu kuusonga mradi huo.
“Alikuja mtu mmoja akajitambulisha kuwa ni Mhandisi wa Manispaa ya Temeke akasema ujenzi wa nyumba hizi uendelee, hakujali maelfu ya wananchi wanaotegemea maji ya kisima hiki,” anasema.
Mbembela amedokeza kuwa Benki ya Dunia kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) iliridhia kufadhili ujenzi wa kisima hicho, kwa sharti la wananchi husika kuchangia asilimia mbili ya Sh milioni 50 zilizotumika kuugharimia.
“Mradi huu una vituo vinane vinavyohudumia wananchi kuchota maji rejareja kwa bei ya Sh 40 kwa lita 20, pia tuna wateja 30 waliofungiwa mabomba ya maji nyumbani ambao hulipia huduma hiyo Sh 15,000 kwa mwezi,’ anafafanua.
Jane Mushi ndiye anayelalamikiwa zaidi kuuweka mradi huo katika hatari ya kutoweka, kwa kuanza ujenzi wa nyumba ya kuishi jirani na kisima cha maji.
Hata hivyo, katika mazungumzo na JAMHURI, Jane anajiona kuwa hana kosa kwa vile aliuziwa eneo hilo kwa njia ya uwazi na hajagusa eneo la mradi wa kisima hicho.
“Nimeuziwa kiwanja hiki mwaka juzi, tuliandikiana kwa Mjumbe wa Shina na Mwenyekiti wa Maradi alikuwapo. Niliwaomba wakazi wa huku tuutafutie mradi huu [kisima] eneo jingine wakakataa.
“Juni 2012 nilianza kufyatua matofali wananiangalia, niliwaomba wakasimamia mabomba ya maji yasikatwe wakati wa ujenzi wa msingi. Aliyeniuzia kiwanja ndiye aliyewauzia na wao wakajenga mradi wa kisima.
“Lakini sidhani kama makazi ninayojenga yataathiri kisima, maana nitajenga choo pembeni. Unajua tukichunguza visima vyote vya maji tutakuta vimeingiliana na vyoo.
“Hata hivyo, wakinipatia fedha taslimu Sh milioni 22 nitawaachia kiwanja kwa sababu sitaki matatizo na mtu, siwezi kugombania ardhi,” anasema Jane.
Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, alipoulizwa na JAMHURI iwapo wanatambua tatizo hilo na kama kuna juhudi zozote wanazofanya kulitatua, amesema
“Ni kweli wakazi wa Yombo Vituka wamekuja kwa Mkurugenzi [wa Manispaa ya Temeke], lakini wanaojenga nyumba jirani na kile kisima hawajaingilia eneo la mradi.
“Tatizo hapa ni kwamba waliochimba kisima ni wengine na waliotoa kibali cha kujenga nyumba jirani na kisima hicho ni wengine, lakini suala hilo linazuilika. Kamati ya mradi ilete maombi ya kukwepesha vyoo visichimbwe jirani na kisima.
“Tutawafuata [wanaojenga nyumba] kuwaelekeza wasichimbe vyoo jirani na kisima, maana ule mradi wameukuta, ni mkubwa na umefadhiliwa na World Bank (Benki ya Dunia).”