Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewahimiza wananchi kudai fidia stahiki pale maeneo yao yanapotwaliwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya umma.

Akinukuu sheria za ardhi Na.4 na Na.5 za mwaka 1999, Waziri Tibaijuka amesema ardhi ya mwananchi inapotwaliwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya umma, mwananchi husika anastahili kulipwa fidia ya haki, kamilifu na inayolipwa kwa wakati.

 

Waziri ametoa msimamo huo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014 bungeni mjini Dodoma, juzi.

 

Amesema hadi Aprili, mwaka huu mali za wananchi 32,484 ambao maeneo yao yaliguswa na miradi mbalimbali nchini zilithaminiwa, kati ya lengo la kuthamini mali 15,000 kwa mwaka.

 

“Uthamini huo uliwezesha baadhi ya miradi ya uwekezaji kuanza kutekelezwa. Miradi hiyo ni pamoja na uwekezaji kwenye migodi, kilimo, viwanda na vituo vya biashara. Pia utekelezaji wa mipango miji kwa ajili ya upimaji wa viwanja vya matumizi mbalimbali nchini; utekelezaji wa miradi ya barabara chini ya TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania); miradi ya maji na umeme; ujenzi wa shule, vyuo na hospitali; upanuzi wa viwanja vya ndege na maeneo ya huduma za jamii.

 

“Kwa mwaka 2013/2014 Wizara inalenga kufanya uthamini wa mali za wananchi wapatao 40,000 kwa lengo la kulipa fidia katika miradi mbalimbali itakayotekelezwa nchini ukiwamo mradi wa kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam,” amesema.

 

Kwa upande mwingine, Profesa Tibaijuka amewakumbusha wenye miradi kwamba Wizara haitashughulikia miradi ambayo haina fidia kamili maana ni kero na usumbufu kwa wananchi na kwa Wizara kushughulika migogoro inayoibuka.

 

“Pia ninahimiza wananchi kuwa wakweli na kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu katika zoezi la fidia. Kinachotakiwa ni kujua haki zao na kudai fidia stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.

 

Katika kusimamia taaluma ya uthamini, amesema Wizara yake hiyo imeendelea kuhakikisha kuwa viwango vya bei ya soko kwa ajili ya ukadiriaji thamani ya ardhi na mazao kwa usahihi vinakuwepo.

 

“Kazi hiyo inalenga kujenga Hazina ya Takwimu za Uthamini (Valuation Data Bank). Vilevile, Wizara yangu ilikamilisha orodha ya viwango vya awali vya fidia ya ardhi na mali nyingine kama mazao na nyumba pamoja na mwongozo wa jinsi ya kuendesha kazi ya uthamini na vilisambazwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kwa ajili ya kuanza kuvitumia.

 

“Katika mwaka 2013/14, Wizara itaendelea kuhakiki na kufanya uchambuzi wa viwango vya awali vinavyoendelea kutumika sambamba na kuweka utaratibu endelevu wa uhuishaji wa viwango vya thamani,” amesema.

1276 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!