NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

 

Wakati michezo kadhaa ya Kombe la Dunia ikiwa imepigwa katika viwanja mbalimbali nchini Urusi, timu kutoka barani Afrika hazioneshi kulitetea vema bara hili kama baadhi yake zilivyotamba wakati zikielekea Urusi.

 

Hadi Jumapili iliyopita, timu za Misri, Morocco na Nigeria zilikuwa zimecheza mechi zake za kwanza kwenye makundi yao huku zote zikipoteza michezo hiyo. Misri ilipotezza mchezo wake kwa Uruguay, kwa kufungwa goli moja na José Giménez katika dakika ya 89.

 

Matumaini ya Waafrika wengi yalikuwa kwa Mafarao wa Misri, baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 wamejiweka katika wakati mgumu katika kundi A, lenye wenyeji Urusi, Uruguay na Saudi Arabia.

 

Tayari wenyeji Urusi wanaongoza kundi hilo baada ya kuwaangamiza Waarabu kutoka Saudi Arabia kwa mabao matano kwa nunge, wakifuatiwa na Uruguay ambao wote wana alama tatu, wakitofautiana idadi ya magoli ya kufunga. Mafarao na Saudi Arabia hawana pointi.

 

Wakati maumivu ya Waafrika yakiwa hayajapona, Morocco wakayazidisha kwa kufungwa bao moja na Iran – kwa bao la kujifunga katika dakika za majeruhi. Beki wa Morocco Aziz Bouhaddouz, alipiga kichwa krosi ya Ehsan Hajsafi na kuukwamisha mpira wavuni.

Morocco iko kundi B ambalo linaonekana kuwa gumu, kutokana na timu zinazoliunda zikiwa ni pamoja na Ureno, Hispania na Iran.

Timu inayoongoza kundi hilo ni Iran, huku timu za Hispania na Ureno zikiwa nafasi ya pili na tatu, baada ya kutoka sare ya mabao matatu kwa matatu, katika kile kilichookana kama ilikuwa mechi kati ya Cristiano Ronaldo na Hispania.

 

Katika mechi hiyo iliyopigwa Ijumaa ya wiki iliyopita, Ronaldo aliingia katika historia nyingine kwenye Kombe la Dunia kwa kuwafuata Pele wa Brazil, Miloslav Klose wa Ujerumani kwa kufunga mabao matatu katika mechi moja (hat-trick).

 

Kazi waliyonayo Morocco kubadili matokeo na kusonga mbele katika hatua ya 16 bora ni ngumu kama kuyapandisha maji mlima.

 

Baada ya timu hizo mbili kutoka Afrika Kaskazini kuanza vibaya mashindano ya Kombe la Dunia, matarajio makubwa yakabaki kwa Nigeria, Senegal na Tunisia. Jumamosi Nigeria imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Croatia.

 

Mabao ya Croatia yalifungwa na Luca Modric pamoja na moja ambalo kiungo wa Nigeria, Oghenekaro Etebo, alijifunga katika dakika ya 32.

 

Safu ya ushambuliaji ya Nigeria ilionekana kuwa butu. Ighalo na Iwobi walijitahidi kuhakikisha wanapata bao, lakini ngome ya Croatia iliyoongozwa na beki kisiki wa klabu ya Liverpool ya nchini Uingereza, Dejan Lovren, ilizima mashambulizi yote.

Kulingana na orodha ya wachezaji walioko benchi ya timu hiyo, Ahmed Musa na Kelechi Iheanacho ndio wafungaji wa kutegemewa, lakini hawakuanzishwa kwenye mechi hiyo na badala yake kocha Mjerumani Gernot Rohr, aliwatumia Alexandre Iwobi pamoja na Ighalo.

 

Hali kadhalika Nigeria, bado ina kibarua kigumu kutokana na timu za Croatia na Denmark kushinda michezo yake ya ufunguzi.

Macho na masikisio ya Waafrika yakabaki kwenye michezo ya Tunisia dhidi ya Uingereza (jana), na Senegal dhidi ya Poland, itakayochezwa leo.

Itakumbukwa kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika iliyopata mafanikio walau ‘makubwa’ ni Cameroon mwaka 1990 ilipokuwa ya kwanza kutoka katika bara hilo kufikia hatua ya robo fainali. Ilitolewa na Uingereza katika dakika za nyongeza.

1280 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!