TIRDO: Maabara za utafiti wa kukuza uchumi viwanda

DAR ES SALAAM
NA CLEMENT MAGEMBE
Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda nchini (TIRDO), limesema kwamba
mwaka huu linaendelea kufanya utafiti wa kina kuhusu uanzishaji wa viwanda na
kuipeleka nchi katika kukuza uchumi kwa njia ya viwanda.
Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema ili kufikia
malengo hayo kwa haraka wameanzisha maabara ya utafiti wa viwanda.
Amesema maabara ya kwanza ya utafiti wa viwanda ilianzishwa na Mmarekani
Thomas Edson, ambaye alikuwa mwanafalsafa aliyegundua balbu na maabara
zinazotumika kwa ajili ya mafunzo na tafiti za viwanda.
Edson alikuwa pia mfanyabiashara na mwekezaji mkubwa wa Marekani. Alizaliwa
Februari 11, 1847 na kufariki dunia Oktoba 18, 1931.
Aliingiza utafiti huo katika nchi nyingi za Ulaya na Marekani ambazo zilikuwa
zikitumia mifumo ya utafiti ndani ya viwanda. Hata hivyo, kwa mujibu wa TIRDO,
nchi nyingi zinazoendelea hazina vitengo vya utafiti ndani ya viwanda.
Profesa Mtambo amesema ni jukumu la Serikali ya Tanzania kuangalia ni kwa
namna gani taasisi za umma na binafsi zinaweza kutoa huduma za kitaalamu
katika kuendeleza viwanda vyetu vya ndani.
Kuhusu suala la ubora wa vyakula, wameshirikiana kwa ukaribu na Tume ya
Sayansi na Teknolojia ya kusini mwa dunia ambayo ni jumuiya ya kitaasisi ya
utafiti kusini.
Amesema wanakutana mara kwa mara na tume hiyo ambayo iliwapa chombo cha
kupimia ubora wa makaa ya mawe, chenye thamani ya zaidi ya dola 30,000 za
Marekani.
Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo lina maabara ambayo imehakikiwa
kimataifa, pia kitengo kinachoshughulikia mambo ya usindikaji wa vyakula na
mazingira ambacho nacho ni muhimu sana.
Kuhusu viwanda
Kuhusu ajenda ya viwanda, amesema nchi inaweza kuwa na viwanda ambavyo
vinazalisha bidhaa, lakini vinashindwa kukidhi masharti na vigezo vya kimazingira
na hivyo kuweza kufungiwa.
Amesema kufungiwa kwa kiwanda kunasababisha hasara kwa wawekezaji huku
sheria za kimataifa zikiangazia bidhaa ambazo hazikidhi viwango.
Pamoja na hayo, ameongeza kuwa shirika hilo lina kitengo cha nishati ambako
tafiti zinaendelea kufanyika, na kwa sasa wameanza kupima ubora wa makaa ya
mawe yanayotumika viwandani.
Akielezea kwa upande wa bidhaa za vyakula, amesema TIRDO inafanya utafiti na
kutoa huduma za kitaalamu katika maeneo ya ubora wa vyakula.

Ameongeza kuwa shirika hilo lina maabara ambayo imehakikiwa kimataifa, pia
kuna kitengo kinachoshughulikia mambo ya usindikaji wa vyakula na mazingira
ambacho nacho ni muhimu sana.
Pamoja na hayo, ameongeza kuwa shirika hilo lina na kitengo cha nishati ambako
tafiti zinafanyika na kwa sasa wameanza na makaa ya mawe.
Amesema Shirika la TIRDO lina uwezo mkubwa wa kusimamia na kuendeleza
maendeleo ya viwanda kwa maana ya rasilimali watu, likiwa na wataalamu
kuanzia ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu ambao wamebobea katika
maeneo yaliyolengwa.
“Kwa hiyo, kama shirika tunao uwezo kama muhimili mkuu katika kujenga uwezo
wa viwanda vya ushindani ndani na nje ya nchi.
“Tunashughulika pia vifaa vya kiuhandisi ambako ujenzi wa bomba la kwanza la
gesi hapa nchini, TIRDO ilihusika kwa kiasi kikubwa sana na ubora wa maungio
yake,” amesema.
Amesema mabomba hayo yaliyohakikiwa ubora wake yalikuwa na urefu wa zaidi
ya kilometa 25 kutoka Bahari ya Hindi.
Amesema pamoja na upimaji wa ubora wa mabomba ya gesi, wanahusika pia
kupima ubora wa mabomba ya maji.
Kuhusu kitengo cha ngozi kwa sasa wanatarajia kusimika mtambo wa kuchakata
taka za ngozi ambazo zitasaidia kupunguza athari za taka za ngozi kwenye
mazingira na kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi.
Amesema taka hizo za ngozi zitarejeshwa kutengeneza bidhaa kama mikanda,
mabegi na pochi.
Pamoja na hayo, amesema TIRDO kama taasisi nyingine za kisayansi inawawia
vigumu baadhi ya watu kuelewa nini kinafanyika na matokeo ya tafiti hizo ambayo
hawayaoni kwa haraka.
Teknolojia zilizoanzishwa
Akielezea teknolojia ya kwanza ya kuchakata taka za plastiki ambayo ililetwa na
TIRDO, amesema watu wengi wamejiajiri katika eneo hilo la kukusanya mabaki
ya taka hizo.
“Kutokana na teknolojia hiyo, TIRDO imesaidia kutengeneza ajira kwa sekta hii
ndogo na pia kupunguza athari za taka za plastiki kwenye mazingira na kuepuka
gharama kwa Serikali katika kusafisha mazingira.
“Teknolojia hii ilipoletwa TIRDO ilifundisha wajasiriamali zaidi ya 300 walioweza
kwenda huko baada ya kupata elimu wakanunua ile teknolojia ambayo ni kubwa
na sasa wanachakata taka za plastiki ambazo wanaziuza nje ya nchi kama
malighafi,” amesema Profesa Mtambo.
Amesema kwa hatua hiyo, Shirika limechangia kuondoa athari za mazingira kwa
kuondoa taka za plastiki na kuchangia kuongeza soko la ajira nchini.
Ameongeza kuwa licha ya kwamba wamechangia kuongezeka kwa ajira lakini
bado hawajafanya tathmini sahihi kuhusu idadi ya Watanzania waliojiajiri katika
sekta hii.
Hata hivyo, amesema ni vigumu kwa walionufaika na teknolojia hii kueleza
kwamba wameipata TIRDO.

Amesema kuhusu teknolojia ya ambayo chaki ilibuniwa na shirika hilo na
kupelekwa katika Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo nchini (SIDO) na
kuchangia kukuza ajira kwa watu mbalimbali wanaojihusisha na utengenezaji wa
chaki.
Pofesa Mtambo amesema teknolojia wanazobuni wamekuwa wakizipeleka SIDO
ambao ndiyo wadau wao wakubwa, kwa lengo la kuongeza kasi katika uibuaji wa
viwanda vidogo vidogo.
Pia ameongeza kuwa wameanzisha mradi mkubwa wa kujenga kiwanda kikubwa
cha kutengeneza chaki katika Mkoa wa Simiyu kwa ushirikiano na wataalamu
kutoka mkoani humo.
Amesema katika kuhakikisha kahawa ya Tanzania iliyodaiwa kuwa na sumu na
kusababisha isipate soko; TIRDO ilifanya utafiti na kugundua kiasi cha sumu
kilichokuweko na kutoa mapendekezo ya kufanya marekebisho na hivyo kahawa
yetu ikarejea tena kwenye soko.
Taasisi washirika
Amesema wanashirikiana na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki
cha Dar es Salaam katika teknolojia ya zao la uyoga na kutoa ajira kwa watu
wengi ambao wanazalisha uyoga majumbani na kuuza.
“Tunazalisha uyoga siyo kwa ajili ya chakula tu, pia kwa ajili ya dawa ambazo
zitazalishwa hapa hapa nchini na kutibu magonjwa mbalimbali.
“Kuna utafiti tulioufanya unaohusu ufuatiliaji wa bidhaa (traceability)
tangu inapozalishwa kiwandani hadi sokoni.
Amesema matokeo ya utafiti huo yalikuwa chimbuko la kuanzishwa kampuni
inayojulikana kwa jina la Global Standards One Tanzania (GSOT) ambayo ndiyo
inatengeneza (bar codes) alama za ubora wa bidhaa.
Amesema kampuni hiyo ndiyo pekee nchini inayotoa alama za ubora wa bidhaa
zinazozalishwa na viwanda vyetu na kuwezesha kutambuliwa nje ya nchi na
kupata soko.
Hata hivyo, amesema utafiti huo umechangia bidhaa zinazozalishwa nchini
kutambuliwa nje ya nchi, na huo pia ni mchango wa TIRDO katika kuibua tafiti
nyingi muhimu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Amesema TIRDO ilipoanzishwa mwaka 1979, viwanda vingi vilikuwa mali ya
Serikali na kupata fedha za utafiti kutoka serikalini huku ikiendelea na wajibu wake
wa kufanya tafiti na kutoa huduma kama taasisi.
Amesema hakukuwa na makubaliano yoyote ya kifedha kwa SIDO au viwanda
vinavyopewa teknolojia inayozalishwa na shirika hilo, lakini kwa sasa wanaandaa
utaratibu wa kunufaika na haki za ubunifu wao (intellectual property rights).
Pamoja na hayo, amesema katika majukumu yao wanashirikiana kwa karibu na
Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Shirika la Maendeleo ya Viwanda la
Umoja wa Mataifa (UNIDO) na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Kusini mwa
dunia.
Taasisi nyingine zinazoshirikiana nao ni DANIDA, Baraza la Sayansi na Utafiti wa
Viwanda la India (Council of Scientific of Industrial Research India) ambako
wataalamu wa TIRDO waliweza kwenda nchini India kwa ajili ya kupata utaalamu
zaidi.

Amesema taasisi nyingine za ndani ya nchi ambazo zinashirikiana na shirika hilo
ni Carmatec ya Arusha, SIDO, Benki ya Rasilimali (TIB), Temdo, Shrika la
Viwango Tanzania (TBS), Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC), Bohari ya
Madawa (MSD) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
mwisho