*Ni mhitimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam

*Anauza kahawa stendi ya mabasi Ubungo

*Awaasa wasomi kutodharau kazi, aeleza mazito

Wakati vijana wengi waliohitimu elimu ya chuo kikuu wakikumbatia dhana ya kutarajia kuajiriwa serikalini na kwenye kampuni kubwa, hali ni tofauti kwa Tony Alfred Kirita, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Bila kujali hadhi yake ya kumiliki Shahada ya Biashara katika Masoko (Bachelor of Commerce in Marketing), kijana huyu ameanzisha biashara ndogo ya kuuza kahawa ya kunywa kwenye vikombe kwa wasafiri katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo (UBT).

 

Matunda ya ujasiriamali yameanza kumjenga kijana huyu kimaisha. Kwa sasa anajitegemea kuendesha maisha yake, tofauti na wahitimu wengi wa chuo kikuu wanaoendelea kuwategemea wazazi wao katika mahitaji muhimu yakiwamo ya chakula, mavazi na malazi.

 

Kijana huyu anawatazama vijana wanaochagua kazi kama watu wanaolazimisha elimu yao kuwa mzigo na kikwazo cha kutumia uwezo wao kutafuta mafanikio maishani.

 

Leo huwezi kuzungumzia huduma bora ya kahawa inayopatikana katika stendi ya Ubungo bila kumtaja kijana Kirita. Usafi wa vifaa vya kazi na kauli nzuri za wahudumu anaosaidiana nao ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwavutia wateja wengi.

 

Masoud Kijasho ni mkazi wa jijini Dar es Salaamu na mmoja wa wateja wanaosifia huduma ya kahawa inayoiuza Kirita.

 

“Kila ninapofika Ubungo kwa ajiri ya safari zangu za mikoani lazima nimchangie kijana huyu. Kahawa yake inaandaliwa vizuri, huduma zake zinaridhisha,” anasena Kijasho.

Katika mahojiano na JAMHURI Dar es Salaam wiki iliyopita, Kirita ameeleza kilichomsukuma, mafanikio, namna anavyokabili vikwazo vya biashara hiyo, ndoto na mipango yake ya baadaye.

 

Kilichomsukuma kuuza kahawa

 

Kirita alianza kuuza kahawa mwaka jana akiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu UDSM. Alifikia uamuzi huo baada ya kuona huduma hiyo licha ya kuhitajiwa na wengi haikuwa inapatikana katika kituo hicho cha mabasi yaendayo mikoani.

 

“Siku moja nilikuwa nasafiri. Nilipokuwa stendi ya mabasi ya Ubungo majira ya alfajiri nikahitaji kupata kifungua kinywa, lakini sikupata huduma hiyo. Nilitafakari sana, hasa nilipoona wasafiri wakinunua na kutumia vinywaji baridi.

 

“Nikaona umuhimu wa kuanzisha huduma ya kuuza kahawa ya moto kwa wasafiri hapa Ubungo. Nilitumia fedha ya posho tunayolipwa chuoni kama mtaji wa kuanzisha biashara hii,” anasema.

 

Hatua ya kwanza alifikiria kununua vikombe vilivyotengenezwa kwa kutumia karatasi (paper cups) kwa ajili ya kunyweya, ambavyo hata hivyo anasema kwa wakati huo havikuwa vinapatikana hapa nchini.

 

“Nilimwomba rafiki yangu wa nchini Kenya akakubali nikamtumia shilingi 169,000 akaninunulia vikombe hivyo huko na kunitumia huku Dar es Salaam.

 

“Lakini wakati huo bado nilikuwa sijapata eneo la kuweka ofisi ya biashara ya kuuza kahawa hapa Ubungo. Hivyo nikatunza vikombe hivyo kwa muda wa miezi mitano nikisubiri kupata mtaji,” anaongeza.

 

Wepesi wake wa kuchangamkia fursa hatimaye ulimfikisha kwenye mafanikio ya kupata mtaji wa kuanzisha mradi huu wa kuuza kahawa.

Kirita daima anakumbuka mchango wa mashindano ya kuandika mawazo ya biashara yaliyotangazwa na INDIAFRICA kwani ndiyo yaliyompatia mtaji wa biashara hii.

 

“Nilishiriki mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi 14, nikafanikiwa kuwa miongoni mwa washindi 18 kutoka Afrika waliopata kila mmoja zawadi ya dola 1,000 za Marekani (sawa na Sh milioni 1.6 za Tanzania),” anasema Kirita.

 

Alitumia sehemu ya fedha hizo kukodi eneo la kuweka ofisi ndogo na kununua vifaa muhimu kama vile majagi, majiko na meza kwa ajili ya kuendeshea mradi wa kuuza kahawa.

 

Aliajiri wasaidizi watano, wote wanawake na kwamba siku ya kwanza waliuza vikombe 35 ambavyo hata hivyo mauzo yake hayakurudisha gharama walizotumia kutoa huduma hiyo kwa siku hiyo.

 

“Nimeamua kuajiri wanawake wanaonisaidia kuendesha mradi huu kwa sababu ni watu ambao ni responsible (wawajibikaji),” anasema.

 

Anawalipa wasaidizi wake hao Sh 2,500 kila mmoja kwa muda wa saa tatu na nusu wanazokuwa kazini. Wanauza kahawa kwenye kikombe chenye ujazo wa mililita 350 kwa bei ya Sh 500. Muda wa kutoa huduma hiyo ni kati ya saa 11 alfajiri na saa 1:30 asubuhi kila siku.

 

Ataja mafanikio yake

Kwa mujibu wa Kirita, idadi ya wateja wake wa kahawa katika stendi hiyo ya Ubungo imeongezeka kutoka watu 35 hadi 200 kwa muda wanaotoa huduma hiyo.

 

“Kwa sasa ninaona mafanikio. Ninapata faida ya wastani wa Sh 20,000 kwa muda tunaotoa huduma hii ya kuuza kahawa. Wateja wangu wengi ni watu wenye kipato cha kati,” anasema na kuongeza:

 

“Kupitia biashara hii nimepata uwezo wa kujitegemea, nimepanga chumba cha kuishi na ninajigharamia mahitaji mengine muhimu, imenisaidia kuanza maisha ya kujitegemea baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu.

 

“Pia biashara hii imeniepushia msukosuko wa kukaa bila kazi ikilinganishwa na wahitimu wenzangu wengi ambao bado wanaishi kwa kuwategemea wazazi na walezi wao.”

 

Hivi karibuni, Kirita alishiriki na kufanikiwa kuibuka mshindi wa kwanza katika shindano la tweets bora zinazoweza kusaidia Watanzania kuondokana na umaskini lililoanzishwa na linalofadhiliwa na Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi.

 

Kijana huyu alitangazwa mshindi wa kwanza aliyejibu vizuri zaidi swali la Julai mwaka huu, lililoulizwa na Dk. Mengi “Kijana asiyekuwa na ajira wala fedha anawezaje kuanza kujijenga kiuchumi?”

 

Kirita aliibuka mshindi wa kwanza na kuzawadiwa Sh milioni moja taslimu na Dk. Mengi kutokana na jibu la swali hilo. Alijibu hivi: “Kama kijana fikiria katika hali iliyopo ni nini unachoweza kufanyia jamii yako, ukipata jibu huo ndiyo mtaji na ajira yako.”

 

“Ninatumia zawadi hii ya shilingi milioni moja kuimarisha biashara yangu ya kuuza kahawa,” anasema Kirita.

 

Vikwazo anavyokumbana navyo

Askari wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakilalamikiwa kwa kukwaza wafanyabiashara ndogondogo. Kirita naye amepata kuonja adha kutoka kwa askari hao kiasi cha kuwataja kama kikwazo kikubwa alichokumbana nacho katika biashara yake ya kuuza kahawa.

 

“Sitasahau tukio la wasaidizi wangu watatu kukamatwa na askari wa jiji. Nilipata taarifa za tukio hilo nikaenda kushughulikia mipango ya kuwatoa mahabusu ya Ubungo,” anaeleza.

 

Anasema tukio hilo liliyumbisha mtaji wa biashara yake kwani alilazimika kutumia fedha nyingi kuwatoa mahabusu, lakini pia baada ya kuwatoa walikataa kuendelea na kazi kutokana na hofu ya kukamatwa tena.

 

“Tulisimama bila kuendesha mradi huu kwa muda wa mwezi na nusu hivi, na hata wasaidizi wangu walipokubali kurudi kazini biashara ilichelewa kurudi katika hatua nzuri tuliyokuwa tumefikia,” anasema Kirita.

 

Hata hivyo, kijana huyu anasema ubunifu, bidii na ari ya kufanya kazi imeirejesha biashara hiyo katika hali ya kutia matumaini hadi leo. Amekuwa na ujasiri wa kupuuza mawazo ya watu wanaomshangaa kwa jinsi anavyoendelea kujikita katika biashara ya kuuza kahawa wakidai haifai kwa kijana mwenye elimu ya chuo kikuu.

 

Mipango, ndoto yake

Mhitimu huyu wa chuo kikuu ana ndoto ya kuwa mfanyabiashara maarufu anayemiliki biashara kubwa, itakayowezesha ajira kwa watu wengi wakiwamo vijana na wanawake hapa nchini.

 

“Napenda kutumia taaluma yangu kujiajiri kufanya biashara kubwa kuliko kutegemea kuajiriwa. Kujiajiri kuna mafanikio makubwa kuliko kuajiriwa,” anasema na kuendelea:

 

“Mwisho wa siku ninatamani kufanya biashara kubwa ya kudumu, yenye mtaji mkubwa na itakayowezesha ajira kwa watu wengi hapa Tanzania.”

 

Anasisitiza kuwa hana mpango wa kuacha biashara ya kuuza kahawa bali ana ndoto ya kuipanua kwa kuanzisha matawi katika maeneo mengine. “Ninataka kuboresha biashara hii ya kuuza kahawa na kuijengea heshima katika jamii,” anasisitiza.

 

Kwa upande mwingine, Kirita anatamani kuwa mfanyabiashara maarufu hapa nchini kama Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi. “Dk. Mengi amedumu katika biashara inayokua kila siku,” anasema.

 

Awaasa vijana wasomi

“Nionavyo mimi, usomi usiwe mzigo kwa kijana kiasi cha kushindwa kutumia uwezo wake kutafuta mafanikio. Tatizo la ukosefu wa ajira lisimkatishe tamaa kijana.

 

“Kabla ya kuanza kufikiri kupata ajira na mkopo ni vizuri kijana akaanza kuonesha uwezo wake kwenye biashara ndogondogo au kazi mbalimbali.

 

“Vijana wasidharau kazi na wasionee aibu fedha zinazotafutwa kihalali. Vijana wengi wanalalamika kuwa hakuna ajira, lakini wengi wao wanadharau na kupuuza fursa mbalimbali kwa kuziona kuwa ni ngumu. Ninawashauri vijana wasichoke kujaribu kila fursa inayojitokeza,” anasisitiza.

 

Kirita anaongeza kuwa vijana wasomi kama yeye wanapaswa kutumia maarifa waliyoyapata kuonesha utofauti na ubunifu wa shughuli halali za maendeleo katika jamii.

 

Wito kwa Serikali, jamii

Kijana huyu anaamini kuwa Serikali ina wajibu wa kuwandaa vijana tangu shuleni waweze kujiajiri baada ya kuhitimu masomo badala ya kutegemea kuajiriwa.

 

“Serikali isisitize elimu kwa vitendo na kuwezesha matokeo bora shuleni, lakini pia iwe karibu na wananchi katika kuanzisha shughuli na miradi mbalimbali katika ngazi ya chini,” anasema.

 

Kwa upande mwingine, anatoa wito kwa jamii nzima kuanzia ngazi ya familia kujenga utamaduni wa kuwaamini vijana na kuwasaidia kila wanapoonesha nia ya kuchangamkia fursa za maendeleo zinazojitokeza.

 

Alikozaliwa, alikosoma

Tony Alfred Kirita alizaliwa mwaka 1990 katika Kitongoji cha Ngulelo mkoani Arusha. Alianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kimandolu mwaka 2003.

 

Alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Arusha kati ya mwaka 2004 na mwaka 2007 alipohitimu kidato cha nne. Baadaye alijiunga na Sekondari ya Juu ya Longido kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2010 alipohitimu kidato cha sita kabla ya kuchaguliwa kujiunga UDSM baadaye mwaka huo huo wa 2010. Kirita amehitimu masomo UDSM mwaka huu.

 

Hakika kijana Kirita ni msomi anayepinga kasumba ya wasomi kuchagua na kudharau kazi. Ameonesha ubunifu na umahiri mkubwa katika kuchangamkia fursa za kujijenga kiuchumi na kimaisha. Ni mfano mzuri wa kuigwa katika jamii.

By Jamhuri