Ndoto ya wakazi wa vijiji vya Nyamboge na Nzera katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji imepotea.

Kupotea kwa ndoto hiyo kunatokana na matumizi mabaya ya Sh milioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa umwagiliaji katika vijiji hivyo.

 

Ujenzi wa mradi huo umegubikwa na utata mkubwa na kuzua maswali kama kweli utajengwa ili kuwakomboa wakazi wa vijiji hivyo waweze kuondokana na kilimo kisicho cha uhakika.

 

Utata huo unatokana na Sh milioni 200 zilizopokewa kwa ajili ya ujenzi huo, lakini Sh milioni 130 zikatumika kwa kile kilichoitwa kuwa ni upembuzi yakinifu huku matumizi ya Sh milioni 70 zilizodaiwa kuwa zingetumika kujenga ghala katika Kijiji cha Nyamboge kutokuwa wazi.

 

Kupotea kwa fedha hizo kumezua hisia kuwa fedha hizo ‘zimeliwa’ na wajanja wachache, ambapo tuhuma zimekuwa zikielekezwa kwa baadhi ya viongozi wa siasa na baadhi ya wakuu wa idara, ambao wamekuwa wakitoa majibu yasiyoridhisha kuhusu matumizi ya fedha hizo.

 

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Geita, Peter Mutagwaba, alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake kuhusu upotevu huo wa fedha alijibu; “Najua kuwa watu wamekutuma, wewe andika unavyoweza nitajibu mbele ya safari.”

 

Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipotembelea wilaya hiyo aliambiwa na Mutagwaba; “Tumepokea Sh milioni 200 kutoka DASIP (Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo wilayani) kujenga skimu ya umwagiliaji Nyamboge-Nzera, na tumetumia Sh milioni 130 kufanya upembuzi yakinifu na milioni 70 tunazipeleka kijijini kujenga ghala la kuhifadhi mazao.”

 

Kutokana na kuwapo kwa hisia za ubadhirifu wa fedha hizo, Mutagwaba alipohojiwa alisema kwamba Sh milioni 40 kati ya Sh milioni 70 zilizoelezwa kuwa zingetumika kujenga ghala la mazao kijijini, ndizo zilizopelekwa kijijini Nyamboge kwa shughuli hizo na kuwa Sh milioni 30 zilizobakia zimetumika kwa mambo mengine  aliyodai kuwa ni pamoja na kuandika mchanganuo wa mradi wa kujenga mradi huo wa umwagiliaji. Mchanganuo huo unaomba Sh bilioni 1.8  kwa ajili ya ujenzi huo.

 

Alipohojiwa sababu ya kutotekeleza maelezo aliyotoa kwa Waziri Mkuu kuwa Sh milioni 70 zilizosalia zingetumika kujenga ghala la mazao kijijini Nyamboge, Mutagwaba hakutaka kutoa taarifa zaidi ya kumtuhumu mwandishi kuwa anatumiwa.

 

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, alipohojiwa kuhusu mradi huo wa Nyamboge-Nzera alimwita Afisa Kilimo ili ampatie majibu ya mradi huo mbele ya mwandishi wa habari.

 

Alipotakiwa kutoa kauli  kama Mkuu wa Wilaya kuhusu matumizi ya fedha hizo zilizotolewa na DASIP kama alivyomsomea Waziri Mkuu wakati wa ziara yake wilayani, Mangochie alisema; “Mimi sisaini pesa, matumizi ya pesa hata rais hawezi kujua kila kitu. Tatizo lako unahisi Afisa Kilimo alipiga pesa halmashauri, subiri aje akupe majibu.”

 

Katika hali ya kutatanisha, alipofika mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mutagwaba alitoa majibu tofauti na yale aliyotoa awali kwa mwandishi. Akiwa mbele ya Mangochie alisema kuwa hizo Sh milioni 70 hazijatumika bado zipo benki zikisubiri nyingine ili wajenge skimu.

 

Mutagwaba aliendelea kudai mbele ya Mkuu wa Wilaya kuwa Sh milioni 40 zinazojenga ghala la mazao la Nyamboge zimepatikana sehemu nyingine.

 

“Zile Sh milioni 70 bado zipo benki ila tumetumia Sh milioni mbili tu kuandika andiko la mradi kuombea wakulima hao pesa za kujenga skimu kutoka Programu ya Uendelezaji Kilimo wilayani (ASDP) alisema.

 

Pamoja na madai hayo ya Afisa Kilimo, uchunguzi umebaini kuwa Juni 19, 2012 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita alitoa taarifa za benki kwa Baraza la Madiwani iliyoonesha kuwa katika akaunti ya kilimo kwenye mradi wa uwezeshaji katika kilimo wilayani, kulikuwa na Sh milioni 59.6 na si Sh milioni 70 kama alivyoelezwa Waziri Mkuu.

 

Katika utata huo huo unaouzunguka mradi wa Nyamboge-Nzera na katika hali isiyo ya kawaida, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Joseph   Musukuma, Machi 4, mwaka huu alitembelea mradi huo na kuandika kwenye kitabu cha wageni cha Kijiji cha Nyamboge kuwa alifika eneo hilo kuona mradi uliokataliwa na wakazi wa Nyamboge.

 

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamboge, Fugo Ablaisius, amekanusha maelezo ya Musukuma na kusema kuwa taarifa hiyo ni uongo mtupu. “Taarifa hiyo ya Musukuma ni ya uongo, sisi hapa hakuna mwanakijiji yeyote aliyekataa skimu ya umwagiliaji, tunaisubiri kwa hamu kubwa kwani kwetu ni mkombozi.”

 

Pamoja na kumpigia mara kadhaa na kumtumia ujumbe mfupi (SMS) kumuuliza kuhusu taarifa yake hiyo, Musukuma hakupokea simu wala kujibu ujumbe wa simu.

 

Aprili 4, 2013 wajumbe wa Kamati ya Fedha, Mipango na Uongozi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo, Leonard Kiganga na Marco Masusu wakiwa wamefuatana na fundi wa halmashauri, Tummomolele Msubisi, walikagua ujenzi wa ghala hilo katika kijiji hicho na kubaini kuwa msingi na jamvi la ghala hilo limepasuka na halifai.

 

Pamoja na madiwani hao kukagua na kuandika katika kitabu cha wageni cha Kijiji cha Nyamboge kuonesha kuwa wamebaini ujenzi mbovu wa msingi huo wa ghala, hakuna hatua zilizochukuliwa za kunusuru ujenzi huo ili uendelee kama kawaida kwa viwango vinavyotakiwa.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Elisha Lupuga, alipotakiwa kufafanua hatua zitakazochukuliwa kutokana na matokeo ya ukaguzi huo, anasema, “Tuna taarifa kuwa mkandarasi ameshindwa kazi, hivyo tunajiandaa kuvunja mkataba na mkandarasi huyo ili tumpe mwingine.”

 

Wakati kumekuwa na tetesi za kufujwa kwa fedha hizo za ujenzi wa ghala, Aprili 20, 2013 maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Frank Masilamba na Alfred John, walifika kijijini Nyamboge kufuatilia mradi huo.

 

Kamanda wa Takukuru wa Wilaya ya Geita, Suzan Mwende, alisema ofisi yake ilipata kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu matumizi ya kutia shaka ya fedha za mradi wa skimu ya Nyamboge-Nzera.

 

“Tulichunguza malalamiko hayo lakini watumishi wa kilimo walitwambia upembuzi yakinifu ni ghali na wananchi hawaelewi upembuzi. Tulikubaliana nao na hatukuendelea mbele zaidi ya hapo.  Hatukujua kama kuna mambo mengi kama hayo ya taarifa za hamashauri kutofautiana, lazima tufungue jalada la uchunguzi,” amesema.

 

Mwende aliahidi kufuatilia masuala yote mawili likiwamo la mradi wa maji wa umwagiliaji na ghala la mazao na kutoa taarifa ya uchunguzi wao.

 

Aidha, ilibainika kuwa Novemba 13, 2012 Mhandisi wa Halmashauri hiyo alikagua ujenzi wa ghala na kuagiza ubomolewe kutokana na kutokuwa wa viwango. Ghala hilo lililojengwa na Kampuni ya GOBI Enterprises ya mjini hapa, lilianza kupasuka wakati ujenzi ukiwa katika hatua ya ‘kumwaga jamvi’.

 

“Naagiza msingi ubomolewe, uchimbwe upya na tofali zitolewe eneo la kazi na ufyatuaji ufanyike baada ya kuthibitisha kuwa zimetolewa,” inasomeka sehemu ya maagizo ya mhandisi kwenda kwa mkandarasi na Kamati ya Ujenzi ya Kijiji iliyonakiliwa kwa Afisa Kilimo wa Wilaya.

 

Kephas Nzali, Meneja wa GOBI, alipohojiwa kuhusiana na ujenzi huo na kampuni yake kukaidi agizo la kubomoa ghala hilo hivyo  kusababishia wakulima ukosefu wa sehemu ya kutunzia mazao yao mwaka huu alisema, “Kwanini unanifuatafuata kwenye mambo yasiyokuhusu? Mambo ya ghala au wananchi yanakuhusu nini? Tena usirudie kunifuata.

 

“Tulimwandikia barua  (Nzali) kumtaka kufikia Mei 22, mwaka huu awe ameanza kujenga upya ghala letu, lakini mpaka sasa huyu jamaa hajaonekana wala hajatujibu,” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Salehe Shaghembe.

 

Juni mwaka huu, Takukuru  iliwapandisha mahakamani waliokuwa watumishi watano wa Hamashauri ya Wilaya ya Geita wakituhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za miradi na kuhujumu uchumi.

 

Kwa miaka ya fedha mitatu mfululizo: 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012, Wilaya ya Geita imepata hati zenye mashaka katika taarifa zake za hesabu kama zilivyokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo upotevu wa mamilioni ya shilingi katika miradi ya maendeleo ulibainishwa.

By Jamhuri