magufuli88Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba Dk. John Magufuli anafanikiwa kuwahudumia Watanzania.

Rais Dk. Magufuli katika kampeni zake na dhamira yake ya kuwatumikia Watanzania, alitaka Watanzania kufaidi rasilimali ambako aliahidi elimu ya msingi na sekondari bure.

Ili kufanikisha hatua hiyo, amedhibiti mapato na safari ambazo si za lazima kwa watumishi wa Serikali, huku akiagiza mamlaka husika kama TRA kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Tangu kuingia madarakani kwa Dk. Magufuli, kumekuwapo na ongezeko la zaidi ya Sh bilioni 700 kwa miezi mitatu ya Desemba hadi Februari. Magufuli alianza rasmi urais Novemba 5, mwaka jana.

Katika utawala wa Serikali iliyopita chini ya Jakaya Kikwete, wastani wa makusanyo ya kodi kwa kiwango cha juu kwa mwezi yalikuwa Sh bilioni 900 tu.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumatano iliyopita.

Katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya TRA, Kidata anasema katika kipindi cha Desemba 2015, TRA imevuka lengo kwa kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh. trilioni 1.4 sawa na ongezeko la wastani wa Sh. bilioni 490 kwa mwezi.

Kidata anasema kiasi hicho ni kikubwa kikilinganishwa na wastani wa makusanyo kwa mwezi Julai hadi Novemba mwaka jana, ambapo ilikuwa ni Sh. bilioni 900 kwa mwezi.

Kidata anasema kutokana na mkakati wa Serikali ya Rais Magufuli ya kuhakikisha mapato ya nchi hayapotei, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 8.5 kwa kipindi cha mwezi Julai mwaka jana hadi Februari, mwaka huu.

Anasema makusanyo ni sawa na asilimia 99 ikilinganishwa na lengo la Sh. trilioni 8.6 na kwamba TRA imejiwekea mikakati mizuri ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato bandarini mwezi Februari, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar walifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.04 ambazo ni sawa na asilimia 101.18 ya lengo la Sh. trilioni 1.02.

Katika kipindi cha mwezi Januari kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar walikusanya Sh. trilioni 1.07 ambazo ni sawa na asilimia 102 ya lengo la Sh. trilioni 1.05.

Katika kipindi cha Desemba 2015, pia TRA iliweza kuvuka lengo kwa kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh trilioni 1.4, mapato ambayo ni sawa na ongezeko la wastani wa Sh. bilioni 490 kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa makusanyo kwa mwezi Julai hadi Novemba ambayo yalikuwa Sh. bilioni 900.

Anasema makusanyo hayo yametokana na uthubutu ambao TRA umejiwekea katika kusimamia na kuhakikisha inaendelea kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.

Pia TRA imeweka mazingira rafiki kwa mlipakodi kulipa kwa wakati na urahisi kwa kutumia mifumo mbalimbali iliyopo na kwamba itafanya vema Machi hadi Juni, mwaka huu.

“Ili kujihakikisha tunaendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi, kufichua wakwepa kodi, kupambana na rushwa na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa,” anasema.

Pia Kidata anasisitiza utumiaji wa mashine za EFD kwa ajili ya kutoa risiti na kwamba kinyume cha hapo wafanyabiashara watachukuliwa hatua.

Kadhalika, Kidata anasema Mamlaka hiyo imefuta bei elekezi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutokana na kuwa ipo kinyume na sheria, huku ikilenga kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ili haki itendeke katika suala zima la ulipaji wa kodi.

By Jamhuri