Askari wa Kitengo cha Intelijensia katika Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, wanatuhumiwa kumpiga na kumuua ndani ya mahabusu, mtuhumiwa Virigili Ludovick Mosha (52).

Moshi alikuwa mkazi wa Kijiji cha Mwasi Kusini, Kata ya Uru Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini.

Polisi walimkamata nyumbani kwake usiku wa manane, Machi 2, mwaka huu akituhumiwa kwa makosa ya jinai.

Kaka yake, Gaitani Mosha, amesema kuwa kifo cha mdogo wake kina utata kutokana na uchunguzi wa madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kubaini damu kwenye ubongo.

Anasema kuwa siku ya tukio, Mosha alikamatwa akiwa mzima kwani kutwa nzima alikuwa akiendesha shughuli zake bila kuwa na tatizo lolote la kiafya. Alikuwa akimiliki duka.

Amesema mdogo wake alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi. Anawatuhumu polisi kwa kujaribu kuficha ukweli.

Kutokana na utata huo, familia imekataa mwito wa Polisi wa kuitaka ichukue mwili kwa ajili ya mazishi. Familia inasisitiza ipewe taarifa sahihi ya chanzo cha kifo cha ndugu yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Mungi, amewatetea askari wake akisema kifo hicho ni cha kawaida.

“Kifo chake ni cha kawaida na hiyo taarifa tumeshaitoa siku nyingi, Polisi hatuhusiki na kifo hicho kama wanataka kuzika wakazike na kama hawataki, basi waache,” amesema Kamanda Mungi.

 

Mke wa marehemu anena

 Wakati Kamanda wa Mungi akiwatetea askari wake, mke wa Mosha, Bertha Faustine, ametaja chanzo cha kuuawa kwa mumewe.

Bertha anasema baada ya mumewe kukamatwa, alipigwa akishinikizwa awaonyeshe mahali alikoficha silaha.

Anasema alipokamatwa alifuatilia katika Kituo Kikuu cha Polisi, na alipojitambulisha aliwekwa chini ya ulinzi na kuwekwa mahabusu.

Anasema baadaye alitolewa na kuingizwa kwenye gari la polisi pamoja na mumewe na kwenda hadi nyumbani kwao kwa ajili ya upekuzi- ukiwa ni upekuzi wa pili baada ya ule uliofanywa usiku.

Anasema muda wote wakati wakienda nyumbani polisi walikuwa wakimpiga mumewe na hata kumkanyaga sehemu mbalimbali za mwili na kutishia kumuua kama hatawaonyesha alikoficha silaha.

Anasema walifanya upekuzi bila kupata silaha, lakini wakachukua pikipiki yaya Mosha auna ya Boxer yenye namba MC939ATE ambayo alikuwa akiitumia kwenye shughuli zake za kibiashara.

Anasema waliporejea kituoni waliwekwa rumande, na kwamba muda wote mumewe alikuwa akilalamika kutokana na maumivu makali yaliyosababishwa na kupigwa.

“Ilipofika saa nne usiku mahabusu wote wa kike waliondolewa na kupelekwa Kituo cha Polisi Majengo,” anasema.

Anasema asubuhi ya Machi 3, mwaka huu wakiwa katika Kituo cha Majengo, alipata taarifa kutoka kwa mahabusu wenzake wakisema kuna mahabusu mwanaume katika Kituo Kikuu cha Polisi amefariki dunia.

“Waliponiambia kuwa yule mahabusu mwanaumme amefariki dunia nilihisi ni mume wangu kutokana na jinsi alivyokuwa akilalamika maumivu tukiwa pamoja na hapo nilianza kupiga ukunga mpaka askari wakajaa kwenye mahabusu yetu ya wanawake na kuanza kunituliza,” alisema.

 

Polisi wahaha kusaka mwafaka

 Pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa kudai polisi hawahusiki kwa kifo cha Mosha, Jeshi hilo limeonekana kuweweseka likfanya kila namna kuhakikisha suala hilo linamalizwa kimya kimya.

Kuna vikao kadhaa vimeendelea kufanywa vikishirikisha maofisa wa vyeo vya juu kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa.

Taarifa kutoka ndani ya familia ya marehemu zimesema polisi wamekuwa katika heka heka za kuhakikisha familia hiyo inakubali kuuchukua mwili wa marehmu na kuuzika, huku wakiahidi kuchukua hatua stahiki kwa waliosababisha kifo cha Mosha. Kikao kingine kilitarajiwa kufanyika Njia Panda, Himo; Wilaya ya Moshi Vijijini.

Wakati vikao hivyo vikiendelea, familia hiyo imewasilisha malalamiko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoani Kilimanjaro ikiomba uchunguzi wa kina kuhusu kifo cha Mosha.

Barua ya familia hiyo ya Machi 11, mwaka huu iliyosainiwa na Gaitani Mosha, kwenda kwa Mwanasheria Mkuu inaeleza wasiwasi wao kuhusu mazingira ya kifo kicho, na kuushtumu uongozi wa Polisi kwa kuwakingia kifua askari wanaotuhumiwa kumuua Mosha. Mwili wa mfanyabiashara huo, hadi wiki iliyopita uliendelea kuhifadhiwa katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi.

By Jamhuri