Rais Donald Trump wa Marekani amesitisha sera yake uhamiaji iliyokuwa inalazimu kuzitenganisha familia za wahamiaji wanaobainika kuvuka mipaka kinyume cha sheria na watoto wao.

Pamoja na kulegeza msimamo huo kutokana na kulalamikiwa kwa sera hiyo ndani na nje ya taifa hilo, Trump amesisitiza kwamba bado ataendelea kuilinda mipaka yake.

Rais Trump ambaye tangu kuingia kwake madarakani alionekana kuhitaji sheria kali zaidi ya kukomesha suala la uhamiaji haramu, amejikuta matatani, safari na hasa baada ya picha zenye mguso za watoto waliotenganishwa na wazazi wao katika mpaka wa Marekani na Mexico kuanza kusambaa na kuleta mshituko mkubwa kwa raia wa Marekani.

Bunge, makundi ya haki za binadamu na hata Bi.Melania Trump yaani mkewe rais Trump mwenyewe na wake wa marais wastaafu.

Haki miliki ya picha Reuters

Hata hivyo bado kuna mashaka kama amri hiyo mpya ya Rais Trump dhidi ya sera yake hiyo kama itawawezesha wanafamilia kuwa pamoja kwa zaidi ya siku 20, na bunge leo siku ya alhamisi linatarajiwa kuipigia kura miswada miwili ambayo inalenga kuondoa utata huo wa kuziumiza familia na mapendekezo mengine ya masuala ya kiuhamiaji.

Akiwahutubia wanachama wake huko Minnesota, rais Trump amesema atatekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni zake ya kujenga ukuta kati yake na Mexico kwa kile alichodai ni jitihada za kulinda mipaka yake.

“Tunapaswa kuwa na mipaka imara, hatuwezi kukatishwa tamaa na masuala ya kipuuzi. Lakini wakati huo huo tunayafanya hayo kwa uangalifu mkubwa.

Nimesaini amri ya kuhakikisha familia zinakuwa pamoja, kwa sababu naona ni jambo muhimu kuamua hivyo. Lakini hatutaacha, tupo imara katika suala la mipaka ,tunahitaji kuwa na ukuta na ni lazima ujengwe” amesema Trump.

Hata hivyo amri hiyo ya rais Trump bado haitoi muda maalumu wa utekelezwaji wake na haionyeshi ni kwa namna gani Zaidi ya watoto 2,00 waliotenganishwa na familia zao watakutanishwa.

Waziri wa afya na huduma za kibinadam Alex Azar amesema idara yake itaanza kuwarejesha watoto kutoka katika maeneo waliyowekwa na kuwaunganisha na wazazi wao lakini hajabainisha ni lini suala ambalo linaleta mashaka kwamba huenda ikawa ni kauli ya kisiasa tu.

By Jamhuri