MTAZAMO.

NA ALEX KAZENGA

Wakati bunge likijadili kupitisha bajeti ya Sh trilioni 1.4 iliyoletwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2018/19, wabunge waliochangia bajeti hiyo wameonya kuhusu ubora na viwango vya elimu visivyoridhisha.

Katika bajeti hiyo wizara imepanga kutekeleza vipaumbele 17, moja ya vipaumbele hivyo ni pamoja na kukarabati shule kongwe 25 za sekondari na kujenga mpya saba.

Bila shaka, ukarabati wa shule hizo kongwe na kujenga nyingine saba utaenda sambamba na kuboresha shule nyingi za msingi ambazo nyingi majengo yake yamechakaa.

Ujenzi huo na ukarabati wa shule za sekondari unaangukia katika kiasi cha Sh bilioni 930 zilizopangwa katika bajeti hiyo kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Ni jambo la heri, wabunge wa bajeti hiyo wamesema serikali ihakikishe inawekeza katika ubora wa elimu na siyo bora elimu, wameitaka serikali kupeleka walimu wa kutosha shuleni na mitaala iliyo bora.

Kwa namna moja ama nyingine hayo ni mapendekezo mazuri yanatakiwa kufanyiwa kazi bila kuupuzwa, kwani elimu iliyo bora ndiyo njia pekee ya kulifikisha taifa letu katika kilele cha mafanikio.

Viongozi wanapaswa kujua kuna gharama kumuongoza mtu mwelevu, lakini kuna gharama zaidi ya mara mbili kumwongoza mtu mbumbu asiyejua hili wala lile.

Nafikiri hilo wameanza kuliona hata viongozi wenyewe, nasema hivyo nikimaanisha tabia na mienendo isiyovumilika ya baadhi ya vijana siku hizi ni matokeo ya elimu isiyokidhi wanayopata katika shule zetu.

Kwa miaka kadhaa sekta ya elimu imekuwa ikipigiwa kelele, watu wamelalamika juu ya viwango vya elimu inayotolewa, changamoto nyingi zimeibuliwa, chache zikafanyiwa kazi na nyingi zikaachwa bila majibu.

Hakuna barabara isiyo na kona, namini kwa kipindi ambacho sekta ya elimu imeonekana kushuka viwango kilikuwa ni kipindi cha kukata kona halafu baadaye tuendelee na safari.

Hakuna safari isiyo na vikwazo, huu sasa ni muda wa kumaliza vikwazo hivyo, sera na mitaala ya elimu viandaliwe kitaalamu badala ya kukumbatia mihemko ya kisiasa, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumejitendea haki na watoto wetu.

Ili kutimiza azma hiyo suala la utoro reja reja na ule wa kudumu kwa wanafunzi hasa wa shule za msingi zilizo vijijini linatakiwa kukomeshwa kwani nalo linakwamisha sekta ya elimu.

Vilevile zipo jamii zisizo na mwamko wa elimu hasa jamii za wafugaji, hizo nazo zinatakiwa kuwekewa mikakati ya kuhakikisha watoto wao wanakuwa wanufaika bila kuachwa nyuma.

Nazisema jamii hizo kwa sababu zinaongoza kwa utumikishaji watoto katika kazi za kuchunga mifugo na biashara ndogo ndogo kama kuuza maziwa kipindi cha masomo.

Mbaya zaidi baadhi ya familia katika jamii hizo huwaachisha shule watoto wa kike na kuwaozesha ndoa za utotoni jambo ambalo linakiuka haki ya motto ya kupata elimu.

Tunapaswa kukomesha vitendo hivyo kama njia rahisi ya kuboresha sekta ya elimu, na kuwa na uhakika wa kuzalisha taifa la wasomi ambao ni nguvu kazi kwa uchumi wa taifa.

Hivyo katika mwaka wa fedha unaotarajia kuanza Julai 2018/19 serikali ihakikishe inasimamia sera ya elimu bila malipo kwa uhakika iwalipe vyema walimu, itoe ajira kwa walimu wapya maana waliopo hawatoshi, ilete mitaala yenye ubora na kukomesha vitendo vya utoro hasa shule za misingi.

876 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!