Katika kikao kimojawapo cha KAMATI KUU ya TANU, Sheikh Takadiri alidiriki kusema hivi “mtu huyu hatakuja kuwapendelea waislamu” (This man will never come to favour us, he would come to favouri his brethren); Mwalimu aliumizwa kwa mashtaka namna ile hata akalia machozi hadharani katika kikao kile. Hili linatuonesha namna Mwalimu alivyoumizwa na sumu ya udini. 

Sote tunakumbuka siku za nyuma nchini mwetu tulipata msukosuko sana wa udini. Kulizuka kikundi cha wanaharakati wa kiislam wakidai haki fulani fulani. Kulikuwa na jukwaa la wakristo na kikundi kikijiita Biblia ni Jibu, wakidai walindwe na Serikali kiimani zao, kulitokea kikundi cha uamsho nacho kilisikika sana kule visiwani hasa Unguja kikidai Serikali ya kiislamu. 

Hao wote walikuwa na shabaha moja tu nayo ni kueneza SUMU, kwa dai hili au lile ili mradi watanzania tufarakane na amani itoweke. Hii maana yake tugawanyike na umoja wa kitaifa ufe.

Mimi Napata faraja kuona uislamu na ukristo havigombani ingawa Uarabu na Uzungu unatofautiana sana kiutamaduni. Pia nafarijika kujua Waziri Mkuu wa Zanzibar, enzi za Sultani, Bwana Ali Muhsin na kiongozi wa ZNP wakati ule alimakatalia Katibu wa AMNUT, Abdulwahid AbdulKarimu kuchanganya udini na Serikali. 

Ali Muhsin alisema “did not believe Christianity posed any danger to Muslim majority in Tanganyika” akasema “AMNUT perceived a divisive policy and therefore was not in the interest of the people” Mohamed Said book pg 251).

Kwa bahati nzuri wimbi lile tukalivuka.Nchi yetu ikawa imara hatukufarakana.Viongozi wa dini zote waliwarudi wafuasi wao, wakawatuliza munkari, tumeweza kulinda AMANI na UTULIVU  wetu Watanzania – mpaka leo hii tuko shwari. 

 

Sumu nyingine ni ya UKABILA. Sumu hii imeenezwa sana na wale ambao mikoa yao haikupata shule za kutosha. Inaonekana wazi Wachaga, Wahaya na Wanyakyusa wamenyoshewa vidole kuwa wana ukabila kweli kweli. 

Kwenye Bima ya Taifa wengi wamelalamika Unyanyusa. Wamediriki hata kusema Amon Nsekala alijijengea himaya yake katika Taasisi hii ya Bima ya Taifa. Wahaya wanajulikana kwa namna wanavyotumia lugha yao kubebana katika idara mbalimbali za Serikali na mashirika.Kuna wakati iliaminika Mzee Katibu Mkuu wa Maji akiitwa Fred Rwegarulila amejijengea himaya huko hata Chuo cha maji pale Mlimani kikaitwa kwa jina lake. 

Wachaga, hatusemi. Watu wanasema hawa ndio Waibo wa Tanganyika. Kila mahali wapo, kila kazi wamo, hivyo huonekana ni watu wengi sana hapa Tanzania. Ingawa kiuhalisia wa sense wachaga siyo wengi sana kama wasukuma hapa nchini.  

Mara tu baada ya Uhuru wetu Mwalimu alitoa angalizo hili, namnukuu “…..For this reason, there is a very real risk that the economic division can lead to racial enmity between our African and Non – African citizens. But this sort of enmity would be just as unreasonable as, for example the enmity between Muslims and Christian (Taz. Nyerere: Uhuru na Umoja sura 40 uk. 179). 

Kwa tafsiri yangu ni kwamba sumu ya ukabila inaweza kutokea kwa msingi wa mbari za raia wa nchi hii. Lakini uadui kutokana na mbari za raia siyo hatari kubwa sana kama vile uadui (au sumu) utakaoibuliwa na wakorofi (evil minded) kuhusu ukabila na udini.

Lalamiko lililozuka lilikuwa mbona kila ofisi unawakuta hao hao tu? Huku wahaya, kule wachaga huko wanyakyusa “kwani sisi wengine hatuziwezi kazi hizo? Hao waliokizusha hayo Mwalimu aliwaita “evil minded citizens” wakorofi wenye roho mbaya.  Na ni kweli kwa kusema sema vile nchi ingeweza kulipuka na kusema mbona sisi wa makabila mengine hatupati kazi kwani sisi siiyo watanzania kama hao?

Mwalimu alizima sumu hii pale alipobuni mpango wa watoto kusoma shule zote alipotaifisha shule. Sasa mtu wa Rwanga aliweza kupelekwa Kagera huko Kahororo, mchaga akaenda Songea, Mfipa akaenda Ilboru na kuanzia mchanganyiko ule wa elimu, lile dhana la ubaguzi wa makabila likafifia.

Leo hii tunaelewana sana watanzania. Hayupo anayegoma kwenda kusini na wala hayupo anayeshangaa kwenda Kilimanjaro. Tumepona sumu hii ya ukabila. Tusiianzishe tena wakati huu kwa wanasiasa kudai ukanda wa Kaskazini. 

Ipo sumu inayoweza kutugawanisha hata tukasambaratika hapa nchini. Hii ni sumu ya ELIMU. Hili la tofauti ya elimu limekuwa sumu kali sana ikatugawa watanzania. Sumu hii inaelezeka kihistoria tu katika nchi yetu. 

Sumu ya elimu ilianza kusikika wakati wa harakati za kudai Uhuru. Yapo makabila, wakoloni waliyapendelea na mazingira ya kijiografiai yaliwafaa wakapata mashule mengi toka madhehebu za dini. 

Wamiosionari walijitahidi kuvutia wafuasi kwa kuwajengea vivutio wafuasi wao. Wakawajengea vivutio vya afya (dispensary) na elimu (mashule). Inaonekana Kilimanjaro, Kagera, Mbeya na Ubondei kule Tanga walifanikiwa sana. Lakini ukanda wote wa Pwani,Umasaini,Ugogoni au Uyaoni kule Tunduru hapakuwa na mashule namna hiyo. Baada ya Uhuru, wasomi wengi waliopata kazi za madaraka ni waliotoka Uchagani, Uhayani na Unyakyusani.Sumu hii ya elimu Baba wa Taifa aliiongelea Bungeni mara tu baada ya Uhuru. 

Alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika Disemba 1962 Mwalimu alitamka hofu yake kwa maneno haya, namnukuu “there is no easy way to remove the existing disparity in EDUCATION between Christian and Muslims or between the educated few and the majority of our people; there is no short cut by which the Masai and the Wagogo can become Wahaya and Wachaga and Wanyakyusa, In short there is no magic by which we can transform this Tanganyika overnight into the Tanganyika we have to  build” (Tazama Freedom and Unity by Nyerere pg 181). 

Wasomi wote wa historia wanajua kuwa Waarabu walifika pwani ya Afrika Mashariki kuanzia mwaka 957. Ni waarabu kutoka Yemeni na Persia siku hizi Iran. 

Hawa walikuwa wafanya biashara waliita nchi yetu Pwani ya Azania. Kumbe waarabu (ukoloni wa kiarabu) nao waliponogewa na biashara wakaja kukaa kabisa. Tunasoma kuna Sultani aliitwa Ali Bin Al-Hassan alivamia Kilwa na kutawala Umatumbi tangu mwaka huo 957 (soma orodha ya masultani wa Kilwa uk. 4 toka Historical Dictionary of Tanzania by Laura S Kurtz kimechapishwa na Carescrow Press Inc. Metuchen N. J. G. London 1978).

Kuanzia miaka hiyo ya 957 mpaka mwaka 1652 waliopofika waarabu wa Omani Pwani ya Afrika Mashariki wananchi wa Pwani yote wakajikuta wamechanganyika na Waarabu. 

Makabila ya Pwani wakabobea mila na tamaduni za kiarabu. Wakaoana na kuzaliana wakapatikana waswahili wa Pwani ya Azania.Hivyo Pwani kukaonekana ni sehemu ya Arabuni. 

Wazungu wamefika Pwani ya Afrika Mashariki kuanzia pale Wareno walipokuja enzi za Vasco Da Gama mwaka 1499 hivi. Hata hivyo Waarabu wa Oman wakawatimua Wareno wale kutoka Zanzibar na Kilwa. Kuanzia mwaka 1824 Sultan Said wa Oman akanogewa na kutawala Zanzibar.

Basi usultani wa Oman ulihamia kabisa visiwani Zanzibar mwaka 1840. Historia hii imeandikwa waziwazi na inaweza kusomwa toka vitabu mbalimbali kimoja cha vitabu hivyo ni hiyo “Historia Dictionary of Tanzania” by Laura S Kurtz nimekijata hapo mwanzoni. 

Muda huo wote historia haisemi popote kuwa utawala wa Waarabu ulijenga kituo cha Afya au Shule kusomesha wakazi wa Zanzibar au Kilwa au Mafia au Dar es Salaam. Huduma za jamii hazikuandaliwa.

Lakini huyo huyo Sultani wa Zanzibar aliwakaribisha wamisionari wazungu mwaka 1837 (Dr.David Livingston) wakati wakatoliki walifika Zanzibar mwaka 1860 wakitokea visiwa vya Re Union – Bahari ya Hindi.

Kwa utamaduni wao wamisionari hawa Wazungu walidhamiria kukomesha biashara ya utumwa uliokiendeshwa na utawala wa Waarabu.

Wakawajengea vituo vya afya, na shule Watumwa wale waliowakomboa na kuanzia hapo lengo la ukombozi likawa kuendeleza shughuli za kijamii kwa watumwa na wananchi wa asili wa Pwani ya Afrika Mashariki. Ndiyo mwanzo wa kuwepo na shule za kikristo katika nchi hii.

Kutokana na mitazamo tofauti ya kiutamaduni  kati ya waarabu wafanya biashara na wamisionari wakombozi wa utumwa kukatokea mtafaruku wa kutokuelewana kati ya wageni waarabu na wazungu. 

Wakazi wa Pwani wakaelezwa na watawala waarabu kuwa watalishwa nguruwe na kuingizwa katika ukristo. Hilo liliwaudhi sana wakazi wa Pwani na ndicho kisa wakazikacha shule za misheni ukanda wote wa Pwani.

Nimetoa historia hiyo fupi sana ya udini kuhusu sumu ya elimu kwa lalamiko kuwa mfumo kristo unawapendelea wakristo na kuwakandamiza waislamu.

By Jamhuri