Wiki iliyopita sikuandika katika safu hii. Kwenye tanbihi, nilieleza kuwa ilikuwa nashughulikia habari nzito inayoendelea kuchapishwa na gazeti hili kuhusu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kutolipa kodi sahihi. Wiki moja kabla ya wiki iliyopita, ilikuwa nimezungumzia suala la nchi hii kuandaa misingi ya kuacha utegemezi wa misaada.

Ninachofanya kuhusu TBL ni kwa maslahi ya Taifa hili. Wapo baadhi ya watu wamenijia, wakaniambia kwa nini tusiachane na habari ya TBL tukaelewana nao, wakatupa matangazo! Nimewaza na kuwazua. Nimejiuliza kama nchi hii ina watu wanaoumia kodi zinapokwepwa au nchi kuingia mikataba isiyo na maslahi kwa Taifa.

Wakati tukiendelea na mapambano dhidi ya TBL kuitaka ilipe kodi stahiki badala ya kutumia udhaifu wa kisheria kulipa kidogo, ndipo likatokea hili la Shirika la Marekani la Misaada la Changamoto za Milenia (MCC) kusitisha misaada kwa Tanzania. Msaada uliositishwa ni sawa na Sh tirilioni 1, sawa na Sh bilioni 200 kwa mwaka.

 Nimeulizwa na viongozi wengi juu ya ni jinsi gani kodi inapotea. Nimewafafanulia na hapa narudia, kwamba TBL wakati inauza vinywaji kama Konyagi kwa kampuni ya Kapari Limited ya Kenya, wanauza katoni moja ya Konyagi kwa dola 24.78 (sawa na Sh 54,516), wanajiuzia kupitia kampuni yao ya Crown Beverage ya Kenya kwa dola 15.52 (Sh 34,144).

 Hii maana yake ni nini? Kwa mfano, TBL wanapouza katoni 1,000 kwa mwezi kupitia Crown Beverage ambayo ni kampuni yao, wanapata Sh 34,144,000. Kama mauzo haya gharama za uendeshaji zingekuwa Sh 25,000,000, ina maana wangetozwa kodi kwenye faida ya Sh 9,144,000. Kwa faida hii wangetozwa kodi ya Sh 2,743,200.

 Iwapo Konyagi kiasi hicho hicho ingeuzwa kwa bei halali ya soko kama wanayowauzia Kapari Limited, kwa idadi hiyo hiyo ya katoni 1,000, TBL wangepata 54,516,000. Kwa kuwa gharama za uendeshaji ni zilezile, wangepunguza Sh milioni 25 za uendeshaji na kutoza kodi ya kampuni ya asilimia 30 ya kiasi kinachobaki kama faida, ambacho ni 29,516,000. Hapa wangelipa kodi ya Sh 8,854,800.

 Sitanii, kwa hesabu hizo fupi tu, ukiangalia mchezo unaofanywa na TBL, bidhaa moja tu kama Konyagi, tayari Serikali inapoteza 6,111,600. Hapo nimeweka idadi ndogo. Ankara za malipo nilizonazo kutoka TBL kwenye Crown Beverage ya Kenya, zinaonesha wakati mwingine wanapeleka hadi wastano wa katoni 1,300 kwa mwezi. Hiyo ni Konyagi tu. Hujagusa bia, wala vinywaji vingine wanavyopeleka kama mvua.

 Nimeona nifafanue zaidi, kwa mfano, kwa nini tunaibana TBL, tukiamini uchunguzi unaofanywa na Serikali utaendeshwa kwa kasi inayostahili uweze kufungua milango ya wakubwa hawa kulipa kodi stahiki ili kiasi kilichokwepwa kiende kikahudumie jamii. Nimeusikia mpango wa baadhi ya kampuni kubwa kuwa zikidaiwa kodi zitakimbilia mahakama za nje, si wa kupuuzwa, ila kama wanadaiwa kwa haki, watalipa tu.

 Mwezi huu, tunaanza mchakato wa bajeti. Tunalenga nchi yetu kuweka mpango kazi utakaoliwezesha Taifa kujitegemea kiuchumi. Nimevutiwa na mpango wa Serikali wa kuanza kulipa madeni. Imelipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wastani wa Sh bilioni 173 hadi Machi, mwaka huu. Hapana shaka hata na sisi taasisi tunazozidai kwa miaka zaidi ya minne sasa kama Zimamoto nazo zitajihimu kutulipa.

 Sitanii, nilisema kama tunataka kuendeleza uchumi wa Taifa hili, tusiangalie nchi kama Marekani, Uingereza, Canada na nyingine. Huko tutapoteza muda. Bajeti ya mwaka huu inapaswa kujikita katika kuwekeza wazawa. Wakati tukizungumza na wenzetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya kuanzisha kiwanda cha magari, twende katika nchi kama India na China kuiga utaalamu.

 Katika nchi hizi kuna kitu kinachoitwa viwanda vidogo vidogo. Hivi karibuni nilizungumza na mtu mmoja mzito aliyeniambia kuwa unaweza kuanzisha kiwanda cha kutengeneza misumari ukiwa na mtaji usiozidi Sh milioni 4. Kuna viwanda vidogo vya kusindika maziwa, matunda, kuranda mbao, kutengeneza samani, vifaa vya ujenzi kama vigae, matofali na bidhaa nyingine tunazotumia kila kukicha.

Viwanda hivi na vingine kama vya kukoboa kahawa, kubangua korosho, kukamua ufuta, alizeti, karanga, pamba au kusindika maharage kwenye makopo, tende, njegere, mbaazi na bidhaa nyingine nyingi za kilimo,  viwanda vyake havizidi Sh milioni 10 pamoja na kufunga umeme.

 Sitanii, ni katika msingi huo nasema kama Serikali inataka kupata fedha, basi ihakikishe inawawezesha wajasiriamali wa Kitanzania kupata hivyo viwanda vidogo vidogo. Hawa wakiishaanzisha hivi viwanda vingi vidogo, wataajiri watu ambao ukiacha pato watakaloingiza, mwisho wa siku watakuwa na ajira. Watalipa kodi ya mapato na hawa wenye viwanda watalipa kodi ya Serikali.

Inawezekana katika mwaka wa kwanza hadi wa tatu tusione faida ya viwanda hivi, lakini kadiri wenye viwanda watakavyopata uzoefu na mzunguko wa fedha ukaongezeka, ndivyo Taifa litakavyoingiza pato kubwa zaidi. Kwa sasa nasikia kuna idara ya uwekezaji, nasema nasikia, ila idara hii inawaza wageni.

 Rais John Magufuli, naomba kukuhakikishia kuwa huwezi kuendesha uchumi kwa kutegemea wageni. Wafanyabiashara kama Reginald Mengi, Said Salim Bakharesa, Gulam Dawji, Yusuf Manji, Rostam Aziz, Ali Mfuruki na wengine ambao biashara zao ziko hapa nchini, ni muhimu kuliko kampuni kama SABmiller yenye nia ya kuchuma na kulipa wanahisa wake huko Johannesburg na London.

 Serikali ina uwezo wa kwenda kwenye ofisi za kampuni za wazawa zilizoko nchini na kujiridhisha kiwango cha kodi kinacholipwa, lakini haina fursa hiyo kwenda Mauritius, Amsterdam au Zurich kukagua kampuni tanzu za SABmiller. Tukijenga wazawa wengi wenye uwezo, nchi hii itakuwa na uhakika wa kukusanya kodi na kuendesha mambo yake bila kutegemea misaada.

Mungu apishie mbali, nasikia asilimia 90 ya dawa tunazotumia nchini zinalipiwa na wafadhili. Rais Magufuli, kwa heshima ya pekee nakuomba, nchi hii haiwezi kuendelea kutegemea wafadhili kwa tiba ya watu wetu. Nakisi hii inapaswa kupunguzwa kwa kiwango kikubwa. Unakumbuka mwaka mmoja uliopita walipotishia kusitisha misaada katika eneo hili, watu walianza kufa kama kuku hospitalini!

Sitanii, hainiingii akilini kuona hadi leo tunapiga magoti kuomba misaada kwa wafadhili eti tupate madawati ya watoto wetu. Serikali ipitishe waraka wenye kufuta udhaifu huu. Hazina itenge fungu na kulisimamia. Sheria ya Ununuzi wa Umma inayopandisha bei ya dawati hadi Sh 200,000 wakati inapitiwa, hili liangaliwe.

 Nawafahamu mafundi wa vijiweni, wanaosema dawati zuri kama la zamani, si viti na meza za ujanjaujanja wanazotengeneza sasa, linaweza kutengenezwa likakalimika kwa Sh 45,000. Rais ameagiza samani zisitoke nje ya nchi na hiyo ni fursa. Tuwapatie kazi hizi vijana wetu walio kwenye vijiwe vya useremala badala ya kutafuta matajiri walioshiba fedha.

Mchezo wa kununua kalamu kwa Sh 3,000, ambayo uraiani inauzwa Sh 200, eti kwa sababu tu imepitia kwenye zabuni, ufutwe. Tunaitaka Tanzania inayotumia fedha kwa uangalifu, nchi inayowezesha watu wake kujitegemea. Sera ya Taifa hili japo haijaelezwa wazi, ilikuwa ni Ujamaa na Kujitegemea.

 Mimi hili la Ujamaa sitalizungumzia maana linahitaji mjadala mrefu, ila hili la Kujitegemea nililiunga mkono jana, naliunga leo na nitaliunga mkono kesho. Nakubaliana kabisa na msemo kuwa ‘mtegemea cha ndugu hufa masikini’. Kwamba haiwezekani leo nchi ikaendelea kuwa tegemezi huku tukiwekeza katika sherehe.

 Tunateketeza hata kiasi kidogo cha fedha tulichonacho kwa kupalilia matumizi yasiyo ya lazima. Leo, ni jambo la kawaida kusikia watu wanaandaa harusi ya Sh milioni 50 au milioni 80, lakini bwana na bibi harusi hawana hata kiwanja. Kuna watu ni wenyeviti wa kudumu wa harusi mbalimbali. Imefika mahali sasa watu wameanza kufuru. Eti kadi ya mtu mmoja (single) Sh 50,000 na mke na mume (double) Sh 100,000.

 Kinachoendelea ni ufisadi tu, na wala hakuna cha maana unachokishuhudia katika harusi za aina hii. Wajumbe wa kamati wana vikampuni vyao uchwara, wanashadidia kuhamasisha watu wachange mamilioni wao waweze kuyafisadi. Mara nyingi watu wenye kuchangia fedha nyingi kiasi hicho, hurejea nyumbani wakilalamika kwa kukosa vinywaji na kupewa chakula kilichopoa au kisicho na kitoweo.

 Sitanii, Rais Magufuli amekuwa na utaratibu mzuri wa kuahirisha sherehe za kitaifa, natamani na kupitia safu hii namshauri kwamba kama alivyoahirisha sherehe za kitaifa mara mbili sasa, basi Rais Magufuli, kwa mamlaka aliyopewa, atangaze vita ya uchumi. Tanzania sasa ivae viatu vya kupambana na umasikini na kwa kuanzia atangaze kuahirisha sherehe za aina yoyote katika nchi hii hadi hapo uchumi wa Taifa letu utakapotengemaa. Tukutane wiki ijayo.

1512 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!