Zimepita wiki tano bila mimi kuandika safu hii ya SITANII. Nilikuwa na jukumu zito la kuuhabarisha umma juu ya mbinu za aina yake zinazotumiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL Group) kuepuka kodi. Katika habari hizo nimefanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa kampuni hiyo inatumia udhaifu wa kisheria kutolipa kodi stahiki.

 Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), tayari imeanzisha uchunguzi baada ya kusoma habari nilizochapisha na kuona tofauti ya bei wanayouza bidhaa za TBL nchini Kenya kwa kampuni tanzu ya Crown Beverage iko chini kwa asilimia 30, ikilinganishwa na bei wanayoiuzia Kampuni ya Kapari Limited, nayo ya nchini Kenya.

Bei ya katoni ya konyagi kwa mfano, wakati Kapari Limited wanamuuzia kwa dola 24.78, wakijiuzia kupitia kampuni dada ya Crown Beverage iliyopo Kenya, wanajiuzia kwa dola 15.52. Hii ina maana kiasi cha dola 9.26, kinachepushwa hakiingii kwenye vitabu vya mapato na hivyo kupunguza faida wanayopata mwisho wa mwaka.

Sitanii, bia kama Castle Milk Stout, wanajiuzia kupitia Crown Beverage kwa wastani wa dola 4.7 (Sh 10,340) kwa kreti badala ya dola 15 (Sh 33,000). Hii ina maana wanachepusha kiasi cha Sh 22,660 kwa kila kreti ambacho iwapo kingeingizwa kwenye vitabu vya hesabu mwisho wa mwaka TBL ingepata faida kubwa na hivyo kulipa kodi kubwa zaidi ya kampuni wakati wa kufunga hesabu zake.

KRA tayari imewaandikia barua TBL ikiwataka walipe tofauti ya kodi wanayochepusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendesha uchunguzi mkali dhidi ya TBL Group inayomiliki kampuni za Tanzania Distillers Limited (TDL), Dar Brew, wazalishaji wa Kibuku (Chibuku) na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) nao tayari wanaichunguza TBL Group kuona uchepushaji huu wa mapato unalipotezea taifa kodi kiasi gani.

Kimsing kinachotokea ni kuwa wawekezaji walionunua hisa kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) TBL kwa kutumia utaratibu huu wa kuuza bidhaa zake nje ya nchi kwa bei ya ‘kutupa’ wanawatia hasara wanahisa na Serikali inapoteza mapato kwa njia ya kodi ya mashirika, ambayo ingetokana na faida kubwa inayofichwa.

Sitanii, napenda kuishukuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Simba. Wakubwa hawa wa TBL walipoona mambo yao yanaanza kubumburuka, wakaamua kukimbilia mahakamani kuomba wasaidiwe kuzuia JAMHURI lisiendelee kuchapisha habari hizi.

Kwa weledi wa hali ya juu wa kisheria, Hakimu Mkazi Mkuu Simba akawapa TBL amri inayolizuia Gazeti la JAMHURI kuchapisha kashfa na habari za uongo dhidi ya TBL. Uongozi wa JAMHURI uliishukuru Makahama ya Kisutu kwa amri hiyo na ukasema haukuanzisha gazeti hili kuandika kashfa, uongo na uzushi, hivyo kwa kuwa kinachoandikwa dhidi ya TBL ni ukweli, na ukweli tupu usiotiliwa shaka, basi tutaendelea kuheshimu amri hiyo ya zuio la muda kwa kuendelea kuandika ukweli.

 Kauli ya kampuni ya JAMHURI, iliihakikishia Mahakama na hapa nami naomba kusisitiza kuwa milele hatutaandika na wala hatujawahi kuandika kashfa, uongo au uzushi si tu dhidi ya TBL, bali hata watu binafsi, kampuni, mashirika, taasisi na mamlaka mbalimbali kama tulivyofanya kwa Bandari, Maliasili, wauzaji wa dawa za kulevya, watakatisha madini, UDA na nyingine nyingi.

 Tutaendelea kutimiza wajibu wetu. Naomba mtuunge mkono katika kipindi hiki cha majaribu, ambacho watu na baadhi ya taasisi hazitaki ukweli usemwe. Kwa msimamo huu tuliouchukua wa kutetea rasilimali za taifa na kuwataka watu na kampuni zilipe kodi tumepata vitisho vingi, ila ulinzi wetu upo mikononi mwa Mungu na wananchi tunaowatumikia.

 Nakiri kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, kuwa idadi ya simu zinazopigwa kwangu kila tunapochapisha habari kubwa, nyingine zikitutia moyo na nyingine zikitujengea hofu ni nyingi, ila nasisitiza mlinzi wetu ni Mungu na kwa kuwa tunafanya kazi halali bila kumwonea mtu, naamini tuko salama. Mungu hawezi kuacha haki ikaangushwa na waovu!

Sitanii, leo nawianisha mada hii na tukio la wiki iliyopita ambapo Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) limesitisha msaada wa Shilingi trilioni 1 kwa miaka 5 sawa na Sh bilioni 200 kila mwaka kwa Tanzania. Sababu kuu mbili zilizotolewa ni; kuvurugwa kwa uchaguzi wa Zanzibar na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni.

Nikiri mapema kuwa sikubaliani na utaratibu wa nchi tajiri au mashirika yenye ukwasi mkubwa kutumia misaada kama fimbo ya kuchapia wanyonge. Ni kutokana na imani hii nimekuwa nikiandika habari kubwa bila woga, hata pale wahusika wanapotoa vitisho dhidi ya maisha yangu na familia yangu.

 Nimepata kumwambia rafiki yangu mmoja kuwa pale Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuna ukuta, walinzi, dawa, manesi na madaktari, lakini siku ya mwanadamu kufa ikifika, wengi wanafia mikononi mwa madaktari pale hospitalini. Tena wakati mwingine si kwa uzembe kama tunavyosikia mara kwa mara, lakini kutokana na mapenzi ya Mungu au tarehe kuwadia.

 Natoa mfano mwingine, kuwa kama ulinzi ungekuwa ngao ya kifo, basi Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Laurent Kabila asingeuawa mikononi mwa kundi kubwa la walinzi wake. Mimi huamini kuwa siku ya kufa ikifika, kuizuia ni sawa na kujidanganya kuwa unaweka milango na madirisha manene kuzuia baridi isiingie ndani.

 Sitanii, napingana na dhana ya misaada kutumia kama fimbo kufifisha utu wa watu katika dunia hii. Nchi kama Marekani inapofika mahala Mkurugenzi wa Shirika kama MCC tu, akataka Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli afunge safari kwenda kumbembeleza kwa ajili ya kulipatia taifa letu Sh bilioni 200 kwa mwaka Napata kichefuchefu.

 Nasisitiza, ni lazima tulinde heshima ya nchi yetu. Lazima tuwe tayari kulinda uhuru wetu kwa gharama yoyote. Waasisi wetu walipigania uhuru, ila mengi waliyoyapinga sasa yanarejea kwa kasi kupitia kapu la misaada (ukoloni mamboleo). Maafisa wadogo tu kutoka nchi zinazosema zimeendelea, wanataka waingie Ikulu yetu kama chumbani kwao, hili nasema hapana.

 Matokeo ya kujirahisisha, tumeshuhudia aibu ya jina la barabara ya lango la kuingilia Ikulu ikiitwa Barack Obama. Naamini Dk. Magufuli atafuta aibu hii. Hii iendelee kuitwa Barabara ya Bagamoyo, na Obama ikibidi atafutiwe mtaa maeneo ya Buguruni au Tandika. Si, kwenye uso kwa Ikulu. Hapana. Hapana. Hapana.

Hata hivyo, wakati tunalalama na kujiandaa kulinda heshima ya taifa letu kwa mishale, upinde, risasi, kisiasa na kiutamaduni, lazima tujiulize wenzetu hawa wamefikiaje hatua hiyo. Binafsi sina utamaduni wa kuuma maneno. Tanzania inaanza kupotea njia.

 Mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alijitahidi kujenga mambo makuu mawili katika miaka yake 23 ya uongozi akiwa Ikulu. Mambo haya ni kujitegemea, alipojenga viwanda na mashirika yapatayo 500, ila watangulizi wetu wakayatumbua kama hayawahusu, kwa dhana kuwa ni mali ya umma. Hapa Mwalimu Nyerere alilenga tujikomboe kiuchumi kama taifa.

 Jambo la pili alilotenda Mwalimu Nyerere na mara kwa mara amekuwa akilirudia ni utawala wa sheria. Mwalimu Nyerere kwa wanaosikiliza hotuba zake, mara kwa mara anasema nchi inapaswa kutawaliwa kwa mujibu wa sheria za nchi ambazo msingi wake ni Katiba anayoapa kuilinda na kuitetea Rais anayeingia madarakani.

 Sheria ya Uchaguzi Na 11 ya Zanzibar, pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2010, hakuna sehemu yoyote inapompa Mwenyekiti Huru Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), mamlaka ya kufuta uchaguzi. Tumeshuhudia, Jecha Salim Jecha, akifuta matokeo ya uchaguzi huru na wa haki ya Oktoba 25, 2015 na akatangaza uchaguzi ambao CCM ilishindana yenyewe Machi 20, 2016. CUF hawakushiriki.

 Leo naona juhudi kubwa watu wanataka kupotosha hata Katiba ya Zanzibar, kwa njaa tu, wanataka atumie Ibara ya 40 kuteua Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hata mgomba wa ADC, Hamad Rashid nasikia amemwandikia barua Rais Ali Mohamed Shein, kuhoji hatima yake kuteuliwa kushika nafasi hiyo, japo anajua fika kuwa hana sifa.

 Sitanii, CCM chukua kioo mjiangalie. Wapinzani nanyi chukueni kioo mjiangalie. Kioo hiki kitawaonyesha uhalisia wa sura zenu. Zanzibar najua lipo tatizo la kutoaminiana. Nimesema mara kadhaa na nadhani si kosa nikirudia kuwa inahitajika Tume ya Maridhiano Zanzibar.

 Najua Katiba ya Zanzibar inazuia kuhoji ushindi wa Rais aliyetangazwa na Tume, lakini misingi ya sheria hairuhusu mtu aliyepata ushindi kwa goli la mkono ushindi wake usihojiwe. Watanzania watendelea kuhoji, kuhoji, kuhoji na kuhoji, hadi hapo tabia hizi za kutafsiri sheria itimizie matakwa ya watu binafsi au chama chenye hamu ya kuendelea kuwa madarakani hata kwa goli la mkono ikome.

 Kauli na matendo yetu, yameisukuma nchi yetu kwenye kona mbaya. Utawala wa sheria, ni zaidi ya polisi na jeshi kutanda mitaani. Sura iliyoko Zanzibar bila shaka kwa mwelekeo huu itahamia hata Bara baada ya miaka si mingi. Ikiwa huo ndiyo mpango mzima, ni bora tutangaze mapema tu, kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 ndiyo wa mwisho, hadi CCM itakapochoka kushinda ikaamua yenyewe kuondoka madarakani.

Mimi si muumini wa misaada yenye mashart. Kiasi kisicholipwa na kampuni kama TBL ni asilimia 25 ya hizo Sh bilioni 200 tulizonyimwa na tunatweta. Leo tukizibana kampuni za madini, utalii, wafanyabiashara wakubwa, Bandari magendo ikadhibitiwa, reli ikafanya kazi, benki zikashusha riba, Wizara yenye dhamana na ardhi ikapimia wananchi ardhi na kuwapa hati, tunafuta umaskini na utegemezi ndani ya miaka miwili. Tutafikiaje hapo, usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo.

Please follow and like us:
Pin Share