Tume ya maridhiano muhimu Zanzibar

Leo ni Jumanne. Ni February 23, 2016. Zimebakia wiki 4 na siku 4 Zanzibar kufanya uchaguzi wa marudio. Wiki iliyopita niliandika kueleza jinsi nilivyomwelewa Rais John Mafuguli baada ya ufafanuzi wake wa kisheria juu ya msimamo wake wa kutoingilia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Kwa ruhusa yako naomba kurudia nilichosema, na kuanzia hapo nijenge hoja ya leo.

“Kabla ya Jumamosi iliyopita, hata mimi nilikuwa mtumwa wa mawazo. Nilikubaliana na waliosema Rais John Pombe Magufuli anapaswa kuingilia uchaguzi wa Zanzibar kunusuru hali. Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli alisema wazi kuwa hataingilia Zanzibar kwa hoja moja tu ya msingi, kuwa akiingilia uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) utakuwa hatarini.

“Rais Magufuli alisema: ‘Kuhusu suala la uchaguzi Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, nafikiri ni  kifungu namba 112 au 115 lakini kama ilivyo kawaida kwa Tume za Uchaguzi zilizo huru duniani, haiwezi ikaingiliwa na Rais yeyote. Ni kama ilivyo NEC ya Tanzania na ZEC ya Zanzibar na ndiyo maana tume zote za uchaguzi duniani huwa ni huru. Huwezi upande mmoja pakawa huru upande mwingine pakawa siyo huru. Ninapenda kuheshimu sheria.

‘Kwa hiyo ZEC ina uhuru wa kuamua mambo yake, na haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote. Lakini kama kuna tafsiri yoyote ambayo ni mbaya, ambaye anayetaka kuitafuta hiyo tafsiri aende mahakamani. Mahakama iko hapo hutaki kwenda halafu unamwambia Magufuli ingilia… si nenda mahakamani wakatoe tafsiri iliyo ya haki? Kwa hiyo siingilii, nitaendelea kukaa kimya.

‘Jukumu langu kama Amiri Jeshi Mkuu ni kuhakikisha usalama wa Zanzibar na Pemba unaimarika, yeyote atakayeleta fyoko fyoko mahali popote, iwe Ukerewe, iwe Nachingwea, iwe Dodoma, iwe Dar es Salaam, iwe Pemba, iwe Zanzibar wajue vyombo vya usalama vipo kwa ajili ya kuwashughulikia hawa.’

“Sitanii, kimsingi, Rais Magufuli amejenga hoja yake katika msingi wa kuheshimu Utawala wa Sheria. Tangu mwaka 1848, Mfaransa Charles Montesquieu alianzisha dhana ya mgawanyo wa madaraka. Mwanasheria huyu nguli aliitaka serikali kugawanywa katika makundi makuu matatu; Bunge, Mahakama na Utawala

“Akapendekeza Bunge liwe na kazi ya kutunga sheria, Mahakama ifanye kazi ya kutafsiri sheria na Utawala (inayoitwa na wengi kuwa ni serikali) isimamie sheria. Ni kwa mantiki hiyo, Rais Magufuli amewaeleza Chama cha Wananchi (CUF) cha kufanya ikiwa wanaona wanayo hoja.” Mwisho wa kujinukuu.

Sitanii, baada ya makala hii nimepata simu, ujumbe na barua pepe nyingi. Naseme naheshimu mawazo ya kila aliyewasiliana na mimi. Ni kutokana na hoja ya kuunda Tume ya Maridhiano Zanzibar, ambayo nayo niliizungumzia hivi:

“Sitanii, tulikwishasikia kauli kwamba nchi haitolewi kwa makaratasi. Kauli hii na nyingine za kibaguzi zilizotolewa hivi karibuni kwa kurejea rangi za ngozi za Wazanzibari, zinanifanya niamini kuwa kuna jambo kubwa zaidi linastahili kutendwa Zanzibar.

“Jambo hili si jingine, tunapaswa kuanzisha mchakato wa kuponya vidonda vya siku nyingi kwa Serikali kuunda Tume ya Maridhiano. Afrika Kusini walikuwa na tatizo sawa na la Zanzibar. Ubaguzi wa rangi (apartheid) uliofanywa na makaburu wa Afrika Kusini ulikuwa wa kutisha.

“Watu walipigwa risasi hadharani bila kosa. Watu walifananishwa na mijusi. Watu walitengwa na kutoruhusiwa kuchimba hata vyoo wakaishi maisha ya ‘mtondoo’ ndani ya vibanda vyao. Ukiangalia mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1976 pale Soweto kwenye makumbusho unatokwa machozi.

“Nilipata fursa ya kufika nyumbani kwa Nelson Mandela mwaka 2006, Soweto na Gauteng mjini Johannesburg. Nyumba ya Mandela ya Soweto ni jirani na nyumba ya Winnie Mandela na iko mkabala na nyumba ya Askofu Mkuu, Desmond Tutu.

“Sitanii, ukiingia kwenye makumbusho ya Soweto ukaona Wazungu walivyokuwa wanaua Waafrika kama digidigi, hata kama ni mgumu kiasi gani ni lazima utamwaga chozi. Watoto wadogo walipigwa risasi. Filamu ya Sarafina inachokionyesha ukizungumza na wazawa ni cha kweli, tena kweli tupu.

“Hili nimewahi kulisema na sasa nalirudia. Mimi ndiye niliyeandika habari ya CUF watoa siku 90 mwezi Novemba, mwaka 2000 baada ya kuhojiana na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Wilfred Lwakatare (sasa mbunge wa Chadema – Bukoba Mjini).

“Nafahamu mauaji yaliyotokea Januari 26 na 27, mwaka 2001 na kwa mara ya kwanza Tanzania ikazalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni, Kenya. Mwaka huo nilikwenda Pemba na Unguja na nikakaa kwenye maskani nyingi. Nakumbuka walivyokuwa wanasusiana harusi na misiba Wazanzibari.

“Sitanii, nakumbuka milipuko ya hapa na pale. Nakumbuka vinyesi kumwagwa kwenye visima vya maji na watu kumwagiwa tindikali. Ukiniuliza tufanyeje, nitakwambia maneno yafuatayo. Zanzibar waienzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika kuelekea kwenye Tume ya Maridhiano kama aliyoiongoza Askofu Tutu nchini Afrika Kusini.

“Nashauri CUF wakafungue kesi ya kuzuia uchaguzi mahakamani. Nashauri CCM wasiruhusu hisia na kusahau uchungu ilioupitia Zanzibar mwaka 2001. Ni kwa njia hii pakee, Zanzibar itabaki salama. Ikiwa Mahakama nayo itawachakachua bila kutoa sababu sahihi sawa na alivyofanya Jecha Salim Jecha, siwashauri cha kufanya, bali akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako. Mungu ibariki Zanzibar. Mungu ibariki Tanzania.”

Sitanii, naomba uniwie radhi msomaji wangu kwa kujinukuu kwa urefu. Wengi wa wasomaji wa safu hii, walitaka niirudie safu yote neno kwa neno. Niliposoma hoja na uzito wa maneno yao, si tu niliiona hatari iliyopo mbele ya Zanzibar, bali nikauona kwa jicho pana umuhimu wa Wazanzibari kukaa wakazungumza lugha moja; MARIDHIANO, bila kuibiana haki!

Ashakumu si matusi. Maneno haya yanazungumzwa, na ni vigumu kumfunda binadamu, bila kubainisha katazo. Maneno haya mawili nimeyapata kutoka kwa wasomaji wengi hadi nikaona niombe radhi kabla ya kuyatumia, na kiungwana niyatumie kwa nia ya kuyatoa kama kielelezo cha mpasuko. Maneno haya si mengine, bali ni GOZI na CHOTARA. Yameigwa Zanzibar.

Tatizo kubwa kila kila upande unaamini upande wa pili unatumia maneno haya kutukana mwingine. Hisia ni nyingi kuliko uhalisia. Wapo wanaomani hata Sulutani atarejea ikiwa chama fulani kitashinda. Wamekwenda mbali zaidi wakanieleza maneno yasiyo na mantiki, eti fulani ni mwanaharamu, hivyo kumpa nchi ni kuinajisi kwani si mtoto wa ndoa!

Sitanii, kwa uhalisia, hisia ziko juu. Nimetangulia kusema hapo awali na naomba kurejea. Nafahamu wapo wenye kuifahamu Zanzibar sifikii hata tone katika ndoo juu ya nikijuacho mbele yao. Nashauri tuangalie hali ya Zanzibar baada ya Amani Abeid Karume na Maalim Seifu Shariff Hamad kuridhia uanzishwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na miaka michache kabla ya hapo.

Katika maridhiano ninayopendekeza, ni vyema mno tukafikia hatua ya kuanzisha maridhiano ya wananchi wa kawaida kwanza badala ya viongozi. Mwafaka uliofikiwa wakati wa SUK mwaka 2010 ungekuwa ni wa wananchi, leo hata kama viongozi wangefarakana wananchi wangeweka historia sawa kwa kuwakumbusha. Ni bahati mbaya SUK umekuwa mwafaka wa viongozi zaidi na matokeo yake tunayaona.

Sitanii na nahitimisha. Rais John Pombe Magufuli, basi usiingilie uchaguzi wa Zanzibar, lakini ingiliza kwa kuanzisha mchakato wa kuundwa kwa Tume ya Maridhiano Zanzibar, itakayotoa tiba ya kudumu kama walivyofanya Afrika ya Kusini. Mungu ibariki Zanzibar. Mungu ibariki Tanzania.