magufuli88Kabla ya Jumamosi iliyopita, hata mimi nilikuwa mtumwa wa mawazo. Nilikubaliana na waliosema Rais John Pombe Magufuli anapaswa kuingilia uchaguzi wa Zanzibar kunusuru hali. Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli alisema wazi kuwa hataingilia Zanzibar kwa hoja moja tu ya msingi, kuwa akiingilia uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) utakuwa hatarini.

Rais Magufuli alisema: “Kuhusu suala la uchaguzi Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, nafikiri ni  kifungu namba 112 au 115 lakini kama ilivyo kawaida kwa Tume za Uchaguzi zilizo huru duniani, haiwezi ikaingiliwa na Rais yeyote. Ni kama ilivyo NEC ya Tanzania na ZEC ya Zanzibar na ndiyo maana tume zote za uchaguzi duniani huwa ni huru. Huwezi upande mmoja pakawa huru upande mwingine pakawa siyo huru. Ninapenda kuheshimu sheria.

“Kwa hiyo ZEC ina uhuru wa kuamua mambo yake, na haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote. Lakini kama kuna tafsiri yoyote ambayo ni mbaya, ambaye anayetaka kuitafuta hiyo tafsiri aende mahakamani. Mahakama iko hapo hutaki kwenda halafu unamwambia Magufuli ingilia… si nenda mahakamani wakatoe tafsiri iliyo ya haki? Kwa hiyo siingilii, nitaendelea kukaa kimya.

“Jukumu langu kama Amiri Jeshi Mkuu ni kuhakikisha usalama wa Zanzibar na Pemba unaimarika, yeyote atakayeleta fyoko fyoko mahali popote, iwe Ukerewe, iwe Nachingwea, iwe Dodoma, iwe Dar es Salaam, iwe Pemba, iwe Zanzibar wajue vyombo vya usalama vipo kwa ajili ya kuwashughulikia hawa.”

Sitanii, kimsingi, Rais Magufuli amejenga hoja yake katika msingi wa kuheshimu Utawala wa Sheria. Tangu mwaka 1848, Mfaransa Charles Montesquieu alianzisha dhana ya mgawanyo wa madaraka. Mwanasheria huyu nguli aliitaka serikali kugawanywa katika makundi makuu matatu; Bunge, Mahakama na Utawala

Akapendekeza Bunge liwe na kazi ya kutunga sheria, Mahakama ifanye kazi ya kutafsiri sheria na Utawala (inayoitwa na wengi kuwa ni serikali) isimamie sheria. Ni kwa mantiki hiyo, Rais Magufuli amewaeleza Chama cha Wananchi (CUF) cha kufanya ikiwa wanaona wanayo hoja.

Wiki moja iliyopita, nilieleza kuwa Rais anahusika na kuwajibika Zanzibar kwa yanayoendelea. Nilikuwa nazungumza katika kipindi kinachorushwa na Star TV cha kila Jumamosi asubuhi kupitia utendaji wa magazeti nchini.

Sitanii, nilijenga hoja, kuwa kama Rais hahusiki basi aondoe polisi, majeshi na usalama wa taifa Zanzibar kwani vyombo hivi viko chini yake. Jioni hiyo hiyo naona Rais Magufuli alijibu nilichosema. Jeshi, Polisi na Usalama wa Taifa, hawajasema hawatasimamia hukumu itakayotolewa na Mahakama.

Nimejiuliza baada ya hotuba ya Rais Magufuli na nikapata simu kadhaa zikihoji Rais alimaanisha nini, na hapa leo naomba nikushirikishe swali nililojihoji. Kwamba, hivi ni kweli CUF hawajui hoja ya utengano wa madaraka?

Majibu niliyopata ni kwamba CUF mpaka dakika hii wanao uwezo wa kuzuia uchaguzi wa marudio usiwepo Zanzibar. Nafahamu Ibara ya 36(7) ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 inasema: “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa kifungu hiki, basi hakuna Mahkama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Sitanii, inawezekana kifungu hiki ndicho kinachowapofusha CUF. Lakini lipo kubwa jingine. Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Mwaka 1984 ya Zanzibar kama ilivyorekebishwa mwaka 2010, haizungumzi chochote juu ya kupinga mchakato wa urais kabla ya kutangaza matokeo. Sheria inaruhusu kufungua mashitaka kwenye ubunge na udiwani.

Hata hivyo, changamoto hii inajibiwa na Ibara ya 93(1) ya Katiba ya Zanzibar inayosema: “Kutakuwa na Mahkama Kuu ya Zanzibar ambayo itakuwa ndio Mahkama ya kumbukumbu na kuwa na mamlaka yote ya kesi za jinai na madai na nguvu nyengine zitazopewa kwa mujibu wa Katiba hii au Sheria nyengine yoyote.”

Ibara hii inakaribisha kila dai kufunguliwa mahakamani. Naamini Rais Magufuli aliona ngoja awaelekeze CUF, kama hawakumwelewa basi hiyo itakuwa tabu. Kwa kuwa mshindi wa urais hajatangazwa, wanaweza kupeleka maombi kuitaka Mahakama iiagize ZEC imalizie kutangaza matokeo.

Sasa naomba kuwa wazi zaidi hapa. Historia ya Zanzibar hatupaswi kuipuuza. Hawa watu wanaogopana kutokana na waliyotendeana miaka ya 1950 na wakati wa Mapinduzi Matukufu mwaka 1964. Sina uhakika sana, ila siamini kwamba wafuasi wa CCM wako tayari kuondoka madarakani. Ingawa ni uungwana ukishindwa kuondoka kwa heshima, naamini wanatafuta nguzo ya mazungumzo kama walishindwa.

Kwamba kama CCM waliona wanaelekea kushindwa wakakataa matokeo, najiuliza CUF wakishiriki uchaguzi wa marudio wakaona wanaelekea kushindwa nao wakikataa matokeo uchaguzi utarudiwa tena? Tukiacha hayo, naamini CUF busara iwasukume kufungua kesi ya kuzuia uchaguzi mahakamani, kisha wapate tafsiri ya kisheria juu ya mchakato mzima wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Sitanii, tulikwishasikia kauli kwamba nchi haitolewi kwa makaratasi. Kauli hii na nyingine za kibaguzi zilizotolewa hivi karibuni kwa kurejea rangi za ngozi za Wazanzibari, zinanifanya niamini kuwa kuna jambo kubwa zaidi linastahili kutendwa Zanzibar.

Jambo hili si jingine, tunapaswa kuanzisha mchakato wa kuponya vidonda vya siku nyingi kwa Serikali kuunda Tume ya Maridhiano. Afrika Kusini walikuwa na tatizo sawa na la Zanzibar. Ubaguzi wa rangi (apartheid) uliofanywa na makaburu wa Afrika Kusini ulikuwa wa kutisha.

Watu walipigwa risasi hadharani bila kosa. Watu walifananishwa na mijusi. Watu walitengwa na kutoruhusiwa kuchimba hata vyoo wakaishi maisha ya ‘mtondoo’ ndani ya vibanda vyao. Ukiangalia mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1976 pale Soweto kwenye makumbusho unatokwa machozi.

Nilipata fursa ya kufika nyumbani kwa Nelson Mandela mwaka 2006 Soweto na Gauteng mjini Johannesburg. Nyumba ya Mandela ya Soweto ni jirani na nyumba ya Winnie Mandela na iko mkabala na nyumba ya Askofu Mkuu, Desmond Tutu.

Sitanii, ukiingia kwenye makumbusho ya Soweto ukaona Wazungu walivyokuwa wanaua Waafrika kama digidigi, hata kama ni mgumu kiasi gani ni lazima utamwaga chozi. Watoto wadogo walipigwa risasi. Filamu ya Sarafina inachokionyesha ukizungumza na wazawa ni cha kweli, tena kweli tupu.

Hili nimewahi kulisema na sasa nalirudia. Mimi ndiye niliyeandika habari ya CUF watoa siku 90 mwezi Novemba, mwaka 2000 baada ya kuhojiana na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Wilfred Lwakatari (sasa mbunge wa Chadema – Bukoba Mjini).

Nafahamu mauaji yaliyotokea Januari 26 na 27, mwaka 2001 na kwa mara ya kwanza Tanzania ikazalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni, Kenya. Mwaka huo nilikwenda Pemba na Unguja na nikakaa kwenye maskani nyingi. Nakumbuka walivyokuwa wanasusiana harusi na misiba Wazanzibari.

Sitanii, nakumbuka milipuko ya hapa na pale. Nakumbuka vinyesi kumwagwa kwenye visima vya maji na watu kumwagiwa tindikali. Ukiniuliza tufanyeje, nitakwambia maneno yafuatayo. Zanzibar waienzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika kuelekea kwenye Tume ya Maridhiano kama aliyoiongoza Askofu Tutu nchini Afrika Kusini.

Nashauri CUF wakafungue kesi ya kuzuia uchaguzi mahakamani. Nashauri CCM wasiruhusu hisia na kusahau uchungu ilioupitia Zanzibar mwaka 2001. Ni kwa njia hii pakee, Zanzibar itabaki salama. Ikiwa Mahakama nayo itawachakachua bila kutoa sababu sahihi sawa na alivyofanya Jecha Salim Jecha, siwashauri cha kufanya, bali akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako. Mungu ibariki Zanzibar. Mungu ibariki Tanzania.

2037 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!